Social Icons

Sunday 1 November 2015

Wasomi wampongeza Dkt John Pombe Magufuli


WASOMI na wananchi wa kawaida wamesema ushindi wa Dk John Magufuli ni halali kwani matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi yanafanana na hali halisi na mapenzi waliyonayo Watanzania kwa mwanasiasa huyo.

Hivyo wametoa mwito kwa vyama vya upinzani kumpa ushirikiano wa kutosha kiongozi huyo mpya wa Tanzania ili atekeleze ahadi zake alizowaahidi Watanzania katika kampeni ili aipeleke nchi katika uchumi wa kati.

Mkurugenzi wa asasi inayoshughulikia Utafiti wa Masuala ya Umasikini na Uchumi (Repoa), Profesa Samuel Wangwe, alisema Dk Magufuli alistahili kushinda kwa sababu ya ahadi zake alizozitoa hasa ya kujenga viwanda ambavyo vinaongeza ajira kwa vijana.

Alisema Dk Magufuli anachotakiwa kukifanya ili kutekeleza ahadi zake kwanza ni kuhakikisha anarejesha imani kwa wawekezaji kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji ili yawe rafiki kwa watu wanaoleta mitaji yao nchini.

Alisema kwa kipindi cha miaka 10, mazingira ya uwekezaji yalizidi kudorora na hivyo kufanya uwekezaji kutoka nje kupungua, jambo ambalo alisema Dk Magufuli atatimiza ndoto yake ya kujenga viwanda kama ataboresha mazingira hayo ili kuwavutia wawekezaji wa nje na ndani.

“Tuna imani kuwa ataweka jambo hili sawa,” alisema Profesa Wangwe na kuongeza kwamba uwekezaji uliofanyika kwenye umeme hasa wa gesi pia utasaidia kujengwa kwa viwanda nchini.

Alisema Dk Magufuli ni mtu mwenye maamuzi hivyo atawasukuma watu katika serikali kufanya kazi kwa bidii na wafanyabiashara watalipa kodi sahihi na wakwepa kodi watapungua.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana kwa upande wake alisema ushindi wa Dk Magufuli ni ushindi wa Watanzania wote na pia ni ushindi wa demokrasia kwani kura alizopata zinaakisi mapenzi ya Watanzania waliyo nayo kwake.

Alisema Watanzania wameamua kupitia sanduku la kura hivyo ushindi wake uheshimiwe na alitoa mwito kwa wapinzani kuyakubali matokeo hayo kwa kile alichosema kuwa kwa mtu makini aliyefuatilia kampeni, alitambua kuwa ushindi ungeenda kwa Dk Magufuli.

Hata hivyo, alisema mgombea wa Chadema, Edward Lowassa anapaswa kupongezwa kwa kuwa ni mtu ambaye ameufanya uchaguzi wa mwaka huu kuwa na ushindani mkubwa, hali ambayo inadhihirisha kuwepo kwa kukomaa kwa demokrasia nchini.

“Kusema kweli Lowassa amebadilisha sura ya siasa nchini, ameleta siasa za ushindani na amesaidia kuongezeka kwa viti vya ubunge na udiwani kwa vyama vya upinzani,” alisema Dk Bana.

Pia alisema Lowassa anapaswa kupongezwa kwa kuwa aliendesha kampeni za kistaarabu tangu mwanzo jambo linalodhihirisha kuwa alikuwa kipenzi cha watu bahati mbaya kura zake hazikutosha. Aliongeza kuwa Lowassa na wenzake wanapaswa kuyakubali matokeo na kumpa ushirikiano wa kutosha Dk Magufuli.

Alishauri mambo ambayo Dk Magufuli anatakiwa kuanza nayo akiapishwa ni kuhakikisha kunakuwepo na lugha ya upatanisho kwani kampeni zimewajeruhi wapinzani wake kutokana na kuitana majina mabaya kama fisadi. Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Gratian Mukoba alimpongeza Dk Magufuli kwa ushindi wake kuwa umepatikana kidemokrasia kupitia sanduku la kura.

Alisema yeye kama kiongozi wa walimu anasubiri Dk Magufuli aapishwe, ataomba ahadi ili aende akamwone amweleze matarajio ya walimu kwa serikali yake mpya.

Chanzo. Habari leo

No comments:

 
 
Blogger Templates