Social Icons

Wednesday 9 December 2015

Nani nguvu ya soda?

WAKATI bado Rais Dk. John Magufuli akiendelea kuunda serikali yake, kwa upande wetu tunaendelea kukumbuka uchangamfu wa wadau mbalimbali nchini katika vita dhidi ya ufisadi kwa kipindi cha mwaka mmoja kurudi nyuma. 

Tunakumbuka matamko mbalimbali yaliyokuwa yakitolewa na wadau hao, iwe ni taasisi binafsi au za umma, iwe NGOs, vyama vya siasa na hata wanasiasa mmoja mmoja, bila kusahau taasisi maalumu rasmi za vyama vya siasa. 

Tumewahi kusikia matamko ya NGOs kama Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) dhidi ya matukio ya kukera ya ufisadi nchini, tumewahi vile vile kusikia taasisi za vijana ndani ya vyama vya siasa kama Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), 

Tume ya Haki za Binadamu Tanzania, taasisi za viongozi mbalimbali wa dini nchini, lakini pia tumekuwa tukisikia matamko ya makundi mengine ya wanataaluma iwe katika vyuo vikuu au ngazi nyingine za elimu. 

Kwa ujumla, matamko hayo ambayo yamekuwa yakitolewa kwa nyakati tofauti kulingana na mlipuko wa matukio ya ufisadi, kuanzia utoroshwaji wa wanyamahai kwenda nchi za nje, ufisadi wa uchotwaji wa mabilioni ya fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) Benki Kuu ya Tanzania au ule ufisadi wa Akaunti ya Tegeta Escrow. 

Matamko haya yaliungwa mkono kwa nguvu kubwa ya umma dhidi ya mafisadi wachache, kelele za kuzomea zilikuwa za kiwango cha juu kiasi kwamba baadhi ya viongozi wa serikali kujikuta katika shinikizo la kujiuzulu- japo kuna wakati mwingine upepo husika wa shinikizo umekuwa ukizoa hata wasiohusika. 

Kwa sasa, hali ni tofauti angalau kwa hizi siku za awali za mwanzo wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli. Kwa upande wetu, angalau tumekuwa tukitarajia juhudi za Magufuli na viongozi wenzake kukabiliana na wimbi la ufisadi zipewe msisitizo na wadau wale wale wa awali. 

Unaweza kuwa msisitizo wa kuonyesha kwamba bado zinahitajika juhudi zaidi au vinginevyo, lakini kinyume chake, inashangaza kuona wengi wa wadau hao wakibaki wamepigwa butwaa, utadhani baadhi yao matamko yao hayakuwa ya dhati kwa wakati ule wa kushamiri kwa ufisadi na serikali kufumbia macho vitendo hivyo. Je, wadau wa mapambano dhidi ya ufisadi ndiyo nguvu ya soda? 

Chanzo. Raiamwema

No comments:

 
 
Blogger Templates