Social Icons

Tuesday 5 January 2016

CCM itakuwa historia ikiendekeza upuuzi huu.



WIKI iliyopita nilisema kwamba haiwezekani kuwa na chama cha siasa ambacho kinataka ridhaa ya kuwaongoza watu walio masikini halafu kiwe kinajiendesha kama chama cha matajiri. Kwa muda mrefu sasa CCM kimekuwa kikiendesha mambo yake ya kisiasa kama vile hakijui umuhimu wa wale wanaoongozwa au waliokipatia ridhaa ya kutawala.

Chama ambacho kimeamua kuachana na itikadi yake ya ukombozi na kujitumbukiza katika itikadi ya utajirisho kwa wachache hakiwezi kuendelea kufanya hivyo milele kwa sababu wanaoamua kiwepo ama kisiwepo madarakani ndio wenye uamuzi wa mwisho.

Kwa miaka kadhaa kumekuwapo na mvutano ndani ya chama tawala kuhusu nini hasa kinachotakiwa kufanyika katika kila nyanja iwe ni kisiasa, kiuchumi au kijamii. Mvutano uliokuwapo na ambao bado utaendelea kuwapo ndiyo hasa uliosababisha hali ambayo tuliishuhudia katika kampeni za uchaguzi mkuu ulioiingiza madarakani Serikali ya Awamu ya Tano ya Dk John Magufuli.

Hapana shaka hata kidogo kwamba wanaojiita wanaCCM damu wanalitambua hilo na wamekwisha kufanya tathmini ya kujua ni kwa nini chama ambacho mgombea wake alikuwa akishinda kwa kishindo miaka iliyopita ghafla amejikuta akipata ushindi wa asilimia 58 ambacho ni kiashiria cha kuporomoka kwa umaarufu wa chama hicho.

Hakuna ubishi hata kidogo kwamba mbinu aliyoitumia Dk Magufuli wakati wa kampeni ya kujinadi bila kuegemea chama chake ilikuwa ni nzuri na iliyobuniwa kwa weledi wa kisiasa. Najua kuna baadhi watakaokuwa hawafurahishwi sana na ukweli huo kwamba ilimbidi mgombea huyo ajinadi yeye kama yeye lakini ukweli utabakia ukweli na hilo ndilo lililomfanya mgombea huyo akaibuka na ushindi.

Baada ya ushindi huo suala moja linakuwa wazi na muhimu sana kwa CCM nalo ni kwamba baada ya hilo kutokea nini kinafuata? Je, chama hicho kina jeuri ya kukaa kimya na kujifanya kwamba hakijaona kilichotokea? Je, kama kimeona kilichotokea sasa njia gani ni sahihi kukihakikishia kuendelea kubaki madarakani kama chama tawala katika chaguzi zijazo?

Tathmini ya hali ilivyokuwa na matarajio ya chama hicho siku za usoni ni jambo muhimu linalotakiwa kufanyika na vichwa tulivu bila ya papara wala mawenge.

Ikumbukwe kwamba CCM kabla ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kurejeshwa hapa nchini kilikuwa ni chama dola. Maana ya chama dola ni mfumo wa siasa ambao chama kinakuwa ni kimoja tu katika siasa za nchi husika. Chama hicho ndicho kinachoisimamia serikali kutekeleza sera zinazotokana na itikadi ya chama.

Chama kinakuwa na usemi wa mwisho katika kila suala la maisha ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi husika. Hakuna kinachofanywa na serikali ambacho chama haijakiridhia.
Mfumo huo wa utawala ulihakikisha kwamba chama kinakuwa na nguvu na uwezo mkubwa pengine kuzidi hata serikali katika kila sekta na ndiyo sababu ziliundwa sekretariati mbalimbali za uchumi, ulinzi, fedha n.k.

Sekretariati zilikuwa ni vitengo vikuu vya chama ambavyo tunaweza kuvilinganisha na kile kinachojulikana kama majopo ya wabunguabongo (think tanks). Hizi ni timu ambazo zinakuwa na wataalamu walio na uwezo mkubwa wa kutunga sera ambazo zinapelekwa kwa watendaji wa serikali kuzitafsiri kwa vitendo.

Chama kushika hatamu za uongozi wa serikali maana yake ni kwamba hakuna ambacho hakijapatiwa baraka za chama kinachoweza kutekelezwa katika nchi. Hivyo ndivyo hali ilivyokuwa kabla ya mageuzi ya kisiasa ya nchi yetu katika miaka tisini na kwa hakika hitimisho lilikuwa katika marekebisho ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo yalikubali kurejeshwa kwa mfumo wa siasa wa vyama vingi hapa nchini.

Ni wazi kwamba CCM hakikuwa kimejiandaa kuingia katika mfumo wa siasa wa vyama vingi na matokeo yake ni kwamba mambo mengi yakaachwa kujiendea tu bila ya utaratibu mzuri ambao ungelikihakikishia umadhubuti hata katika mazingira ya ushindani wa kisiasa.

Chama ambacho kilikuwa na itikadi inayosimamia maslahi ya wanyonge, wakulima na wafanyakazi kikaachiwa kutumbikia katika mikono ya mawakala wa ubepari na ukoloni mamboleo. Hilo lilifanyika katika mazingira ambayo ubepari wa kimataifa ulikuwa umechachamaa kote duniani na kulikuwa na kila aina ya shinikizo kuhakikisha vyama vya siasa vya itikadi ya mrengo wa kushoto kama kilivyokuwa Chama cha Mapinduzi vinatii amri na kukimbia vivuli vyao. CCM ikajikuta ikipata kigugumizi katika jambo la msingi sana yaani itikadi.

Badala ya kubakia katika itikadi ya ujamaa na kujitegemea ambayo ndiyo iliyokuwa ikikipembua miongoni mwa vyama vya siasa CCM ikajitumbukiza katika kundi la vyama vya siasa visivyokuwa na itikadi yoyote kama ambavyo vingi vimekuwa vikitaka kutambulika hivyo. Kwamba huwezi kuwa na chama cha siasa kinachodai kuwatetea wanyonge halafu usiwe na itikadi ya kisiasa inayotamka wazi kwamba hiyo ndiyo dhamira na lengo kuu.

CCM kilipofungua milango kwa kila aina ya bepari, kabaila na bepari uchwara sio tu kuwa mwanachama bali kuwa kiongozi wa chama hicho hapo ndipo mwanzo wa kifo chake ulipowadia na kuanza kutekelezwa.

Tunachokishuhudia hivi sasa ni chama kilichokuwa kikiwatetea walalahoi kutekwa na wanyonyaji na kugeuzwa chombo cha kujipatia madaraka ya kisiasa ambayo yanawawezesha kunyonya bila ya kubughudhiwa na yeyote.

Katika mazingira ambayo wananchi wa kawaida wamejikuta kuwa yatima wasio na mtetezi anayetambulika na mwenye msimamo ni wazi kwamba hakuna njia nyingine isipokuwa kumjaribu mwingine ye yote atayeonekana kuwa ni mkombozi ili kuziba ombwe.

Kwa kutambua ukweli huo kwamba wananchi wanatafuta mkombozi mbadala ndiyo sababu uchaguzi uliopita ukawa mgumu sana kwa CCM. Na kama siyo ukweli kwamba uamuzi wa Chadema ulikuwa na hitilafu ya msingi ni wazi kwamba hivi sasa tungelikuwa tunaizungumzia CCM kama kiongozi wa upinzani.

Najua siyo rahisi wakereketwa wa CCM wakaukubali ukweli huu kwamba safari hii ni uamuzi wa wapinzani wao ndiyo uliowaokoa kuhamia viti vya upinzani, lakini tathmini ya kimazingira inaonesha kwamba hali haikuwa shwari hata kidogo na ndiyo sababu Dk Magufuli akalazimika kujinadi yeye kama yeye na kuahidi kwamba ataunda serikali ya Dk John Magufuli na kukwepa kabisa kuwaudhi na kuwakera wapiga kura kwa kusema kwamba ni CCM iliyomtuma. CCM haiwezi kumtuma mtu ye yote kwenda kwa wapiga kura wakamkubali kwa sababu CCM kimepoteza mvuto kwa wapiga kura.
Si kwamba rangi za kijani na manjano zimechuja bali ni chama kimepoteza mwelekeo na kinahitaji kurejeshwa kwenye njia kuu.

Kama nilivyosema katika sehemu ya kwanza ya safu hii wiki iliyopita ni kwamba CCM imejigeuza kuwa ni genge la watu wasiojali chochote na kuamini kwamba wananchi wa kawaida wananunulika tu wakati wa kupiga kura.

Kitendo cha wanamapinduzi wa kweli ndani ya chama hicho kupigwa chini kutokana na nguvu ya pesa ya wavamizi walioingia kwa nguvu ya pesa ndicho ambacho kimeklfikisha chama hicho hapa kilipo. Wananchi wanahitaji kuwa na chama cha kuwatetea na kuwapigania. Badala ya kuwapigania na kuwatetea CCM imekuwa ikiwadidimiza na kuwapiga kutumia kila silaha na fimbo iliyo mbele yake. Wananchi wamegundua kwamba hawana mshirika ndani ya CCM na ndiyo sababu wanakiona kwamba ni adui badala ya rafiki.

Inapotokea kwamba wanamapinduzi wachache waliobakia ndani ya CCM wanajitahidi kukirejesha chama hicho kwenye mstari wananchi wanachoshuhudia ni jitihada za pamoja za wahafidhina na wapinga mapinduzi na mamluki kutoka katika kila kona wakijumuika na kupigana kwa nguvu zao zote na zaidi kutumia fedha kuwapaka kila aina ya uchafu na matusi. Mfano mzuri ni mchakato wa katiba uliokuwa unasimamiwa na Jaji (mstaafu) Joseph Sinde Warioba.

Yeyote yule ambaye anajua umuhimu wa kuwapatia wananchi katiba nzuri itakayowalindia maslahi yao sasa na baadae hawezi kukaa kimya bila ya kueleza umuhimu wa rasimu ya katiba aliyoiandaa Jaji Warioba na wenzake. Inawezekanaje utunge katiba mpya ya Tanzania baada ya Azimio la Arusha usishughulikie masuala ambayo ndiyo yametusababishia madhila yote haya hapa nchini sasa hivi?
Utawezaje kuwa na Katiba mpya ya Tanzania ambayo haitambui ukubwa wa tatizo la uongozi? Au isiyoona kwamba kuna kila sababu ya kulinda rasilimali za umma? Au isiyoona umuhimu wa kupunguza madaraka ya rais ili kuondoa mgongano wa maslahi ambao unatokana na mfumo wa sasa hivi unaompatia rais madaraka makubwa kupindukia?

Nani asiyejua kwamba unapokuwa na kiongozi ambaye anaweza kujilimbikizia mali na kuwa na akaunti nje ya nchi ni kuhalalisha rushwa tu na si vinginevyo?
Hili la rasimu ya katiba mpya ni moja ya mambo ambayo yamekianika mno CCM kiasi kwamba ni vigumu kukubaliana nacho kama chama cha utetezi wa maslahi ya umma. 

Ni wazi kwamba kwa kujichukulia madaraka na kuamua kuondokana na vipengele vinavyolinda umma kutokana na matumizi mabaya ya ofisi yanayoweza kufanywa na viongozi wao ni kujitangazia vita na wapiga kura na haiwezekani chama hicho kikapendwa na hao wapiga kura.

Upo kila ushahidi kwamba kama CCM isipojiangalia na kutambua kwamba wananchi hawapendi mambo yake basi ijiandae kuwa sehemu ya historia. 

Chanzo. Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates