Ripoti ya siri ya jopo maalum la Umoja wa mataifa linalofuatilia mgogoro wa Sudan Kusini imewatuhumu viongozi wote wawili nchini humo wanaogombea madaraka kuhusika katika mauaji ya raia
Ripoti ya siri ya jopo la Umoja wa mataifa linalofuatilia mzozo wa Sudan Kusini kwa ajili ya kuliarifu baraza la usalama la Umoja huo wa Mataifa limebainisha kwamba rais Salva Kiir na kiongozi wa wasi Riek Machar bado wanavidhibiti vikosi vya wanajeshi wao na kwahivyo wanaweza moja kwa moja kulaumiwa kwa mauaji ya raia na vitendo vingine ambavyo vinastahili kuhalalisha hatua ya kuwekewa vikwazo.
Nakala ya ripoti hiyo imelifikia shirika la habari la Reuters jana Jumatatu.Baraza la usalama la Umoja wa mataifa lenye wanachama 15 kwa muda mrefu limekuwa likitishia kupitisha vikwazo vya salaha lakini Urusi yenye kura ya Turufu ikiungwa mkono na Angola imekuwa ikipinga hatua hiyo.
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vitaly Churkin alisema hapo jana anawasiwasi kwamba vikwazo vya silaha vinaweza kuwekewa upande mmoja kwasababu itakuwa rahisi kuiwekea serikali.Jopo la Umoja wa Mataifa lakini limependekeza katika ripoti yake hiyo kwamba viongozi wa ngazi ya juu walioko katika nafasi ya kutoa maamuzi ambao wanawajibika kwa vitendo vinavyoshuhudiwa pamoja na sera zinazotishia amani, usalama na uthabiti wa taifa hilo waingizwe katika orodha chafu.
Hata hivyo orodha ya majina yaliyopendekezwa na jopo hilo kuingia katika vikwazo vya usafiri na mali zao kuzuiliwa hayakujumuishwa ndani ya ripoti hiyo,ingawa mwanadiplomasia mmoja anayejuwa kilichomo ndani ya ripoti hiyo ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba miongoni mwa watu wanaotajwa ni pamoja na rais Kiir na mpinzani wake Riek Machar.Kutolewa kwa ripoti hiyo kumekuja wakati ambapo Riek Machar amesikika akitoa mwito wa kuitaka Uganda iingilie kati na kuwa msuluhishi katika mvutano wa kuundwa serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Kiir na Machar wakipeana mkono na kiongozi wa kidini kabla ya kutia saini makubaliano ya amani ya 2014 Addis Ababa
Imetajwa kwamba Machar na Museveni walipangiwa kukutana janaKimsingi muda wa mwisho uliokuwa umewekwa wa pande hizo zinazovutana Sudan Kusini kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa ulikuwa ni Jumamosi iliyopita lakini muda mfupi kabla rais Kiir bila ya kufanya mashauriano na upande wa pilisi akachukua uamuzi wa kuongeza idadi ya mikoa kutoka 10 hadi 28 suala lililoibua mvutano mpya.Rais wa zamani wa Bostwana anayesuluhisha mgogoro huo wa Sudan Kusini ameikosoa hatua ya Kiir akisema haikubaliki.Sasa Riek Machar anamtaka Museveni kutumia nafasi yake kumshinikiza Kiir .
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri : Mohammed Abdul-rahman
Chanzo, Dw.de
No comments:
Post a Comment