Social Icons

Friday 29 April 2016

Nyerere na Nkuruma wasingekubali yaliyotokea Libya



MADA iliyopita katika Soma na Hirji (SNH) ilikuwa na swali lifuatalo; Kabla ya kuvamiwa na nchi za Magharibi, Libya ilikuwa nchi iliyoendelea kiuchumi, kielimu, kiafya na mambo mengine kuliko nchi nyingine zote za Afrika, ijapokuwa ilikosa kuwa na mfumo wa kidemokrasia.
Leo hii, nchi hiyo imesambaratika kabisa, maisha yamekuwa magumu kwa watu wote, usalama katika maisha umepotea, mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanaendelea na watu wengi wanakimbia kwenda Ulaya.

Je, kwanini nchi nyingine za Afrika zilikaa pembeni wakati ushambulizi wa nchi za Ulaya; ushambulizi usioidhinishwa waziwazi na Umoja wa Mataifa (UN) ulikuwa unaendelea? Na kwanini hatusemi kuwa hawa washambuliaji ni wahalifu wa kivita?

Kwanini tunaendelea kukaribisha majeshi kama haya kuua Afrika? Je, Mwalimu Nyerere au Kwame Nkrumah wangesema nini kuhusu uamuzi huo ?
Swali hili lilijibiwa na LEWIS BARNABAS ambaye ndiye amekuwa mshindi wa shindani hilo. Hivi ndivyo alivyojenga hoja zake.

LIBYA ni nchi iliyoko Kaskazini mwa bara la Afrika. Inapakana na nchi za Misri, Sudan, Niger, Chad, Algeria,Tunisia na Bahari ya Mediterranean. Eneo kubwa la Libya ni sehemu ya Jangwa la Sahara lenye akiba kubwa ya mafuta ambayo ndio utajiri wa nchi hiyo.

Huwezi kuzungumzia historia ya Libya bila kumtaja Kanali Muammar Gaddafi aliyeipindua serikali ya mfalme Idris, tarehe mosi, Septemba 1969 na kutangaza Jamhuri ya Kiarabu ya Libya. Gaddafi ni mwanamapinduzi mahiri aliyetumia mfumo wa utawala wa Kijamahiriya, uliomfanya kila Mlibya ajione ni sehemu ya uongozi kwa kushiriki katika kamati za uongozi wa umma zilizoanzia ngazi ya kata hadi taifa.

Kanali Gaddafi alikuwa mwenye kufuata itikadi ya ujamaa na alihakikisha rasilimali za nchi yake zinamilikiwa na kuwanufaisha wananchi.
Alikataa nguvu za ubeberu na unyonyaji wa Marekani na washirika wake wa nchi za Magharibi. Mfumo huu uliwawezesha wananchi wa Libya kupata huduma nzuri za kijamii, kiuchumi, kielimu, kiafya na kufurahia rasilimali za nchi yao.

Pamoja na hayo, wapo waliomchukulia Gaddafi kama dikteta na mtu mkatili kwa kutoruhusu mfumo huru wa kidemokrasia na kuwakandamiza wale wote waliojitokeza hadharani kumpinga na kumshauri.
Gaddafi aliuawa kikatili mwezi Oktoba Oktoba, 2011 na majeshi ya Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO). Tangu kuanguka kwa utawala wa mwanamapinduzi huyo, Libya pamekuwa si mahali salama kwa maisha ya watu wake.

Maisha yamekuwa magumu kwa watu wote, mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanaendelea na usalama wao umepungua, yaani kifo kipo “nje nje”.
Hali hii imepelekea Walibya wengi kukimbilia Ulaya na Asia kusalimisha roho zao. Haya yote katika kuwania madaraka ya taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta baina ya makundi makuu mawili.

Kundi la kwanza ni lile linalojiita “Baraza Kuu la Taifa” ambalo linaunda serikali inayotambuliwa kimataifa lenye makao yake makuu Mashariki ya Libya, baada ya kuukimbia mji mkuu Tripoli ambao ulichukuliwa na muungano wa makundi ya wanamgambo mwezi Agosti 2014.
Kundi la pili ni kundi la kigaidi la “Dola ya Kiislamu (IS)”.

Hili ndiyo kundi tishio zaidi kwa usalama wa watu, limekuwa likisaidiwa na makundi mengine ya kigaidi kutoka barani Asia na nchi jirani kama Tunisia. Kundi hili limekua likitoa mafunzo ya kijeshi na kuwasajili kwa nguvu vijana kwenye kundi lao.

Hili ndilo kundi lililosheheni makamanda waliokuwa watiifu kwa jeshi la Muammar Gaddafi, limechukua udhibiti wa mji wa Sirte na kufanya mashambulizi makali dhidi ya mahasimu wao, yakiwemo mashambulizi ya kujitoa mhanga, ambayo yamekua yakiua watu wengi.

Pia limepiga hatua kubwa kwenye kutwaa baadhi ya vituo vya mafuta nchini Libya. Hali hii ya mapigano baina ya pande hizi mbili ndiyo msingi wa machafuko nchini humo yanayopelekea watu kuikimbia nchi yao.

Lakini cha kusikitisha ni kwamba nchi za Afrika chini ya umoja wao (AU) zilikaa pembeni wakati wa ushambulizi wa Libya. Hii ni kutokana na kwamba nchi za Afrika bado hazijapata uhuru juu ya maslahi ya mataifa yao katika nyanja zote za maisha, zimeishia kuwa na “uhuru wa bendera” basi!

Hii inadhihirisha kwamba mizizi ya ukoloni bado ipo (ukoloni mamboleo). Kinachozidi kutugharimu ni Afrika kuwa na viongozi vibaraka kwa nchi za Magharibi, wanaoendelea kuwa watumwa eti wasije wakakosa misaada kutoka kwao.

Wamekuwa wakikiuka haki za binadamu kama, kuchochea mauaji kwa kutoa silaha kwa baadhi ya makundi, kuchochea ndoa za jinsia moja, kufunga jela na kuua viongozi wa Afrika wanaoonesha upinzani kwao.

Haya yote yanatokea ilhali kuna Umoja wa Mataifa (UN), ambao hauna misingi thabiti ya kulisaidia bala la Afrika kwa kuwa UN imekua ikitumiwa na mataifa makubwa kwa maslahi binafsi.
Vilevile nchi zenye rasilimali zimekuwa na machafuko ambapo nchi za magharibi zimekua zikichochea ghasia kwa kujenga chuki baina ya makundi, na kuweza kuchota rasilimali hizo kirahisi kwa kile wanachoamini kwamba “vita ya panzi, furaha ya kunguru”.

Kwa mujibu wa Katiba ya UN, Ibara ya 2 (7) hakuna nchi ambayo ina haki ya kuishambulia nchi nyingine kutokana na sababu za ndani ya nchi. Nchi moja hairuhusiwi kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine.

Nchi nyingi za Afrika zimeendelea kupokea majeshi kutoka mataifa ya ughaibuni, nchi kama Kongo (zote mbili), Somalia, na Jamhuri ya Afrika ya kati zimekua zikipokea majeshi kutoka ughaibuni. Kiukweli, nchi za Afrika zina majeshi imara yanayoweza kulinda amani, haya ya kigeni yanaletwa kwa maslahi ya nchi zao.

Kwa maoni yangu, mataifa ya magharibi, yenye uchu wa rasilimali, yanatawala na kukandamiza demokrasia za nchi maskini, hususani kutoka bara la Afrika, kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiitikadi.
Waasisi wa bara hili wakiongozwa na Mwalimu Nyerere wa Tanzania na Kwame Nkrumah walipinga kwa nguvu zote unyonyaji na ukoloni. Walitaka Afrika iungane ili iweze kupambana na changamoto za uhuru.

Umoja wao wa Afrika umeshindwa kutatua matatizo ya Waafrika. Utawala mbovu, udikteta, ukame, uonevu na uporaji wa maliasili vinaendelea kushamiri.

Kwa maoni yangu, nazishauri serikali za Afrika zisimamie misingi iliyowekwa na waasisi wake, misingi iliyopinga mazingira yote ya ujinga, umasikini, maradhi na njaa. Hii itawezekana endapo viongozi wetu watazingatia kanuni za utawala bora na kuwa na hofu ya Mungu.

Nina uhakika, kama akina Nyerere na Nkrumah wangekuwa hai na wakiwa madarakani, isingewezekana kwa mabeberu wa Magharibi kufanya kile walichokifanya kwa Gadafi na Libya.

No comments:

 
 
Blogger Templates