Social Icons

Saturday, 7 May 2016

HISTORIA YA MJI WA TUKUYU


 HISTORIA YA MJI WA TUKUYU

Historia ya mji wa Tukuyu inaanzia enzi za utawala wa Ujerumani nchini Tanganyika, mji mkuu wa utawala wa Ujerumani nchini Tanganyika ulikuwa ni Bagamoyo katika mkoa wa Pwani.


UTAWALA

Ujerumani ili kujilinda na hatari ya kuvamiwa na Uingereza ambayo ilikuwa ikitawala Nyasaland, 'Malawi ya sasa' utawala wa Ujerumani uliamua kujiimalisha kando kando ya ziwa Nyasa katika eneo lililoitwa Langburg " Mwaya ya sasa"
Lungburg maana yake ni Boma lefu.

Makao makuu ya wilaya ya Rungwe, mji wa Tukuyu

Mji wa Langburg ulikuwa ni eneo lote la Matema na Ipinda, boma la mji wa Mwaya au Langburg kwa sasa halipo tena kwani limeshazama ndani ya ziwa Nyasa.

Baada ya Wajerumani kuamua kuuhama mji wa Mwaya au Langburg, ndipo walikuja kujenga Boma katika eneo la Tukuyu na ndio ukawa mwanzo wa mji wa Tukuyu ambao Wajerumani waliuita Neu Langburg, wakiwa na maana ya Langburg mpya.

Boma liliojengwa na Mjerumani katika mji wa Tukuyu

Baada ya Wajerumani kujenga boma katika mji wa Tukuyu au Neu Langburg, pia walijenga kambi ya kijeshi katika kijiji cha Masoko kando kando ya ziwa Kisiba.

Ziwa Masoko mahali ilipokuwepo kambi ya kijeshi ya Mjerumani

Mwanzo wa eneo la Bagamoyo, Tukuyu Mjini

Wakati Wajerumani wanakuja Tukuyu walikuja na askari pamoja na wapagazi kutoka Bagamoyo Pwani, ambao walikuwa ni masalia ya vizazi vya utumwa, makabila yaliyokuja na Wajerumani yalikuwa ni Wayao, Wamanyema, Wanyamwezi, Wamakonde, Wangoni, Wangindo n.k

Wengi ya wapagazi hao walikuwa ni Waislam kutokana na asili ya walikotoka yaani Bagamoyo ya Pwani ya bahari ya Hindi, Hivyo Wajerumani waliamua kuwapa watu waliokuja nao eneo la kuishi mwanzo mwa mji wa Tukuyu, nao wakaamua kuliita eneo hilo Bagamoyo, ili kuenzi walikotoka.

 Mojawapo ya nyumba zilizojengwa na waanzilishi wa Bagamoyo ya Tukuyu

Wapagazi wote waliokuja hawakuja na wake zao na walipata tabu sana kupata wake wa kuoa kutoka kabila la Wanyakyusa, kwani walitofautiana sana katika mila na desturi zao.

Baadae wapagazi hao walipata wasaidizi kutoka katika kabila la Wakinga kutoka Lupila, mkinga wa kwanza kuja kuishi Bagamoyo alikuwa ni Sadiki Mkakile, na alikubali kusilimu na kuwa Muislam.

Sadiki Mkakile ndiye anasadikiwa kuwa aliyerudi tena Ukinga na kuwachukua wakinga wengine na kuja nao Tukuyu Bagamoyo kwa sharti la kusilimu na kuwa Waislam, aliwaleta huku akijifanya ni ndugu zake. 

Hii ndiyo Bagamoyo ya Tukuyu ya sasa.

Mzee Mohamed Mpangule Kyando ndio Mkinga pekee ambaye alikuja Bagamoyo akiwa ni muislamu tayari, kwa kuwa yeye hakuja akitokea ukinga bali alitokea Tanga na kuja Bagamoyo moja kwa moja,
Inasemekana baada ya wapagazi na wakinga walipokaa pamoja na kuelewana vizuri, wapagazi waliwashawishi wakinga kurudi ukinga kwenda kuwatafutia wanawake wa kuoa

Wapagazi hao walipoona umri wao umekuwa mkubwa waliamua kuwarithisha mali zao Wakinga na ndipo sehemu kubwa ya Bagamoyo ya Tukuyu kuwa na Wakinga ambao ni Waislamu.

HISTORIA YA ELIMU KATIKA MJI WA TUKUYU

Wakati wa ukoloni wa Mwingereza na mwanzoni mwa uhuru wa Tanganyika, sera ya elimu ilikuwa ni darasa la kwanza mpaka darasa la nne na baadae mwanafunzi akifaulu anaendelea darasa la tano mpaka la nane.

Kabla ya mwaka 1964 mji wa Tukuyu ulikuwa na shule za darasa la kwanza mpaka la nne zifuatazo.
1. Tukuyu boys, sasa inaitwa Tukuyu day Sekondari
2. Tukuyu girls, sasa inaitwa Bulyaga Shule ya Msingi
3. Tukuyu mixed, sasa inaitwa Tukuyu Polisi Shule ya Msingi
4. TAPA, sasa inaitwa Madaraka Shule ya Msingi.
5. Katumba one
6. Katumba two
7. Aghakhan, sasa inaitwa Bagamoyo Shule ya Msingi
8. Kyimbila

Shule hizi zote zilikuwa zinategemea wanafunzi wao wanaofaulu kuendelea darasa la tano kwenda katika shule zifuatazo.
1. Ndembela boys
2. Mpuguso boys
3. Lutengano girls

Hizo ndizo shule pekee zilizokuwa zinategemewa kuchukua wanafunzi wanaofaulu, si kwa shule za Tukuyu tu, bali kwa Rungwe nzima. Hali hiyo iliwalazimu viongozi wa wilaya kuumiza vichwa na kutafuta jinsi ya kupata shule nyingine ya darasa la tano mpaka nane.

Ndipo mwaka 1964 ilipoamuliwa kuwa Eneo na majengo yaliyokuwa yakitumiwa kuwaandaa watu kwenda kufanya kazi za migodini katika nchi za Afrika kusini, Zambia na Zimbabwe. Lichukuliwe na kugeuzwa shule, na shule hiyo ikaitwa Tukuyu Model, sasa inaitwa Magereza Shule ya Msingi.

Shule ya Msingi Magereza ya Sasa, zamani Tukuyu Model

Mwalimu Mkuu wa wa kwanza wa shule ya Tukuyu Model alikuwa Marehemu Mwalimu George Mwakyembe, baba yake Mhe. Harrison George Mwakyembe Mbunge wa Kyela na rafiki yangu Masumbuko George Mwakyembe.

                                  
 Dkt. Harrison George Mwakyembe, mtoto wa Mwl George Mwakyembe

Pia kwa wakati mmoja huo huo Mwalimu George Mwakyembe alikuwa Mkuu wa Shule zifuatazo Tukuyu boys, Tukuyu Mixed na Tukuyu Model. Miongoni mwa wanafunzi
 wa kwanza wa shule ya Tukuyu Model ilipoanzishwa mwaka 1964 walikuwa Joseph Kasyupa na Habibu Saidi Mohamed. Mwalimu wa darasa wa kwanza shuleni hapo alikuwa Mwalimu Ulindula Mwamakombe.

Pia shule ya sekondari Loleza kihistoria ilianzia mjini Tukuyu katika eneo la Kyimbila  chini ya Mkuu wa shule mama Hungkok ambaye alikuwa ni Mwingereza, Shule hiyo ya Loleza haikuwahi kuwa ya dini bali ilikuwa ya Serikali toka wakati wa mkoloni Mwingereza.

Jengo la Chama Cha Ushirika Rungwe (RUCU)

HISTORIA YA MAJENGO YA KUKUSANYA WATU KWENDA MIGODINI SASA SHULE YA MSINGI MAGEREZA.

Muingereza wakati akitawala Tanganyika pia alikuwa akitawala Afrika Kusini, Zambia, Malawi na Zimbabwe kwa nchi za kusini mwa Afrika, katika nchi za Zambia, Zimbabwe na Afrika Kusini kulikuwa na migodi ya madini mbali mbali, hivyo ilimuhitaji Muingereza kuhitaji watu wa kwenda kufanya kazi migodini.

Baada ya kuumiza kichwa Muingereza aligundua kuwa Wanyakyusa hawakuwa waoga kufanya kazi za migodini na walizipenda kazi hizo, ndipo alipoamua kuanzisha kambi ya kukusanya na kufundisha watu wa kwenda kufanya kazi migodini katika mji wa Tukuyu eneo la Magereza.
Jengo la Halmashauri ya wilaya ya Rungwe, mjini Tukuyu

Kambi hiyo ilianzishwa eneo la jirani na Gereza la Tukuyu, na ilikuwa na majengo yafuatayo.

1. Ofisi za kambi, sasa hivi ni Ofisi ya kazi ya wilaya ya Rungwe.
2. Nyumba za wafanyakazi, kwa sasa wanakaa wafanyakazi wa ofisi ya kazi
3. Mabweni na bwalo la chakula, kwa sasa ni madarasa manne ya Shule ya Msingi Magereza yanayotazamana na Gereza la Tukuyu
4. Nyumba ya Meneja, kwa sasa ni nyumba aliyopewa Amon Nsekela na NBC.

Ndege aina Helkopta ya kwanza kutua Tukuyu ilitua mwaka 1959 na ilitua katika nyumba ya meneja, hali iliyosababisha watu wa mji wa Tukuyu kufurika kuiangalia wakidhani imeanguka.

UMEME

Mji wa Tukuyu ni miongoni mwa miji ya kwanza kuwa na umeme, kwani mji wa Tukuyu ulikuwa na Jenereta la umeme lililokuwa linatoa umeme kwa mji wa Tukuyu tokea mwanzo wa mji wa Tukuyu eneo la Bagamoyo na kuishia Makandana.

Mji wa Tukuyu katika Nyanda za juu kusini kwa maana ya mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa na Songea, ndio ulikuwa wa pili kupata umeme baada ya mji wa Mbeya, mji wa Tukuyu ulipata umeme mwaka 1964. Kituo cha umeme kilikuwa eneo la Batini Bagamoyo, mahali ambapo mpaka sasa ni kituo cha kupokelea umeme toka gridi ya Taifa.

BARABARA

Mji wa Tukuyu ulipata barabara ya kwanza ya lami mwaka 1959, barabara hiyo ya lami ilianzia eneo la njia panda ya kwenda Shule ya Katumba Two na kuishia njia panda ya Polisi ya sasa. Mwaka 1965 mpaka 1968 barabara ya Uyole kwenda Kyela ilijengwa na kampuni kutoka Ujerumani. Wakati wa ujenzi wa barabara ya Uyole kwenda Kyela eneo la Tukuyu toka Katumba mpaka njia panda polisi halikuguswa kwa kuwa tayari lilikuwa na lami ya Mwingereza.

MAJI

Mji wa Tukuyu ulianza kupata maji ya bomba na wakazi wake kuyatumia tokea mwishoni mwa miaka ya 1950, wakati huo Mkoloni Mwingereza aliwajengea wananchi waswahili vituo vya kuchotea maji kama vifuatavyo.
1: Mwanzo wa mji ( Bagamoyo )
2: Eneo la msikitini ( Bagamoyo )
3; Majengo. ( Bagamoyo )
4: Sokoni ( Ndani ya Soko )
5: Kiwira Road.
6: Bulyaga
7: Makandana Hospitali ( Nje ya geti )

Eneo ziliko ofisi za serikali za wilaya na makazi ya viongozi na eneo la uhindini hayakuwa na vituo vya Umma vya kuchotea maji kwani hawa walikuwa wanapata huduma za maji ndani ya majumba yao. Kwani wakati huo mji wa Tukuyu ulikuwa umegawanywa katika maeneo matatu.
1: Uzunguni
2: Uhindini
3: Uswahilini.

HOSPITALI. 

Mji wa Tukuyu ulikuwa na huduma za hospitali kabla ya nchi kupata uhuru, hospitali  ya kwanza ya mji wa Tukuyu ilikuwa katika eneo la Mabonde mahali zilipo ofisi za ujenzi kwa sasa, na Chuo cha kwanza cha Unesi katika mikoa ya nyanda za juu kusini kilikuwa mjini Tukuyu katika Shule ya Msingi Mabonde ya sasa. Hospitali ya Wilaya ya Rungwe ya sasa yaani hospitali ya Makandana ilijengwa mwaka 1962

POLISI

Kituo cha Polisi katika mji wa Tukuyu kilijengwa wakati wa ukoloni, sero ya polisi ilikuwa ni chumba cha upelelezi cha sasa, kutokana na udogo wake ndipo wakazi wa Tukuyu wakapaita "PAFINYE" kwa Kinyakyusa ikiwa na maana Pembamba au padogo kwa kiswahili. Ikumbukwe wakati wa utawala wa Mjerumani hapakuwa na magereza adhabu zote ziliishia kupigwa viboko na kunyongwa tu.

 MAJANGA MAKUBWA YALIYOWAHI KUUKUMBA MJI WA TUKUYU.

Mwaka 1910, mji wa Tukuyu ulikumbwa na tetemeko kubwa la ardhi na kusababisha mji wote kupotea na kurudiwa tena na tetemeko kubwa mwaka 1911, mji wa Tukuyu ulianza kujengwa upya mwaka 1914. Pia ugonjwa wa Ndui uliukumba mji wa Tukuyu mwaka 1911.

 Joseph Kasyupa akitoa historia ya mji wa Tukuyu

UTAWALA WA JADI

Wakati wa utawala wa Mwingereza nchini Tanganyika alifanya jitihada kubwa ya kuunganisha tawala za machifu, na kupata chifu mmoja wa kabila, mfano. Uchagani na kadhalika. 

Kwa Wanyakyusa ilishindikana kuwaunganisha Machifu na kumpata Chifu mmoja wa Wanyakyusa, ndio maana kila Tarafa ilikuwa na mahakama yake, mahakama zote zilikuwa zinaongozwa na Machifu, mahakama ya rufaa ilikuwa Ushirika (Masebe) ndio eneo ambalo machifu walikuwa wanakutana, na kupitia rufaa za hukumu zilizotolewa kwenye tarafa.

Utaratibu uliokuwa unatumika katika mahakama hiyo ya rufaa ni machifu watatu mpaka watano ndio waliokuwa wanapitia rufaa hizo na walifanya kazi hizo kwa mwezi. Mwezi uliofuata waliofuata walifuata machifu wengine.

Habari hii imeandikwa na Bashiru Madodi kutokana na masimulizi ya Joseph Kasyupa.
                                                      (2016)
 

   









No comments:

 
 
Blogger Templates