Social Icons

Monday, 2 May 2016

Miaka mitano baada ya kuuawa Osama bin Laden

Leo tarehe mbili mwezi Mei imetimia miaka mitano kamili tangu wanajeshi wa kikosi maalum cha jeshi la Marekani walipomuuwa Kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda Osama bin Laden nchini Pakistan 2011

Osama Bin Laden Porträt

Lakini wachambuzi wanasema ingawa kuuwawa kwa bin Laden kumelidhoofisha kundi hilo, lakini bado lingalipo na linaendelea kuwa kitisho likiwa limefanya mashambulizi kadhaa ya kigaidi Afrika, Ulaya na Yemen.

Kufuatia mauaji ya mjini Paris katika ofisi ya jarida la Charlie Hebdo pamoja na mlolongo wa mashambulizi katika kanda ya Afrika magharibi, bado Al Qaeda limeonyesha linaweza kushambulia wakati wowote. Halikadhalika nchini Syria na Yemen, wapiganaji wake wameitumia hali ya vurugu iliozuka katika nchi hizo na kuyatwaa maeneo kadhaa, hata wakati mwengine kutoa sura ya kwamba ni nguvu mbadala kwa maovu yanayofanywa na utawala wa Dola la Kiislamu.

Wakati kikosi maalum cha jeshi la Marekani kilipomuua bin Laden Mei mbili 2011, Al-Qaeda ilioundwa mwishoni mwa miaka ya 1980, ilikuwa tayari imepata pigo kubwa, huku viongozi na wapiganaji wake wengi wakiwa wameuawa au kukamatwa kufuatia kampeni ya Marekani ya , “Vita dhidi ya Ugaidi.” Mivutano ilizuka miongoni mwa viongozi wa ngazi ya juu wa Al Qaeda na Ayman Al-Zawahiri akashika uongozi wa Al-Qaeda Juni 26, 2011.Tawi moja wapo lililokuwa likijulikana kama Al-Qaeda katika Iraq lilijitenga na kuunda Dola la Kiislamu kwa Iraq na eneo la Sham, ikimaanisha hadi Syria (ISIL ).

Ehemaliges Versteck von Osama bin Laden in Abbotabad Pakistan

Bin Laden aliuliwa katika makaazi yake ya Abbotabad

Baada ya kuyatwaa maeneo makubwa nchini Iraq na Syria 2014, kundi hilo likatangaza kuundwa utawala wa Kiislamu katika maeneo iliokuwa likiyadhibiti na kuyaita Dola la Kiislamu.Tangu wakati huo IS imemuathiri mno mshirika wake wa zamani kwa kuwavutia maelfu ya wapiganaji Jihadi kujiunga nalo na kudai kuhusika na mashambulizi yaliowauwa mamia ya watu Brussels, Paris, Tunisia, Uturuki, Lebanon, Yemen, Saudi Arabia na kwenye ndege ya abiria ya Urusi ilioripuliwa ikiwa katika anga ya Misri.

William Mccants kutoka taasisi ya Brookings mjini Washington, anasema ni kweli Al-Qaeda imevunjwa nguvu na IS , lakini imejiimarisha. Imeonyesha nguvu Syria na Yemen na tawi lake nchini Syria la Al-Nusra ni moja wapo ya makundi yenye nguvu katika mapigano dhidi ya utawala wa Rais Bashar al-Assad. Tawi lake nchini Yemen (AQAP) ni kitisho katika ghuba ya bara Arabu.

Mashambulizi ya tawi la Al-Qaeda katika eneo la Maghreb barani Afrika (AQIM) nchini Mali, Burkina Faso na Cote d´Ivoire, Novemba mwaka jana ambapo watu kadhaa waliuawa wakiwemo raia wakigeni ni ushahidi mwengine wa kuzagaa kwa kundi Al-Qaeda. Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Mizozo-International Crisi Group- linasema ingawa IS limetokeza kuwa na nguvu, Al-Qaeda imejitanua ikiwa na matawi Afrika Kaskazini, Somalia, Syria na Yemen na baadhi yakiwa na nguvu zaidi kuliko hapo kabla. Itakumbukwa Agosti 7 1998, zaidi ya watu 200 waliuawa katika miripuko ya mabomu katika balozi za Marekani mjini Dar es salaam Tanzania na Nairobi Kenya .

Miaka mitano baada ya kifo cha muasisi wa kundi hilo, Al Qaeda inabakia kuwa kitisho kikubwa na kama afisa mmoja wa zamani Idara ya usalama Alain Rodier alivyoandika katika mtandao mmoja wa habari wa Ufaransa Atlantico mapema mwezi Aprili, “Jihadi hii itadumu miongo kadhaa.”

Chanzo. Dw.de


No comments:

 
 
Blogger Templates