Social Icons

Thursday, 25 August 2016

Mbowe atakula sukari yenye mchanga?

KABLA sijaanza mada niliyokusudia kuiandika leo nitasema, japo kidogo, kuhusu Dk. John Magufuli, kutengua uteuzi wa aliyekua Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda na kumteua Mrisho Gambo badala yake.

Magufuli hakueleza sababu ya kumwondoa Ntibenda. Ukimya huo ulisababisha watu kubashiri sababu. Baadhi walisema Ntibenda alikaa kimya huku madiwani wakila fedha za umma.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru, Halmashauri ya Wilaya ya Meru pamoja na Halmashauri ya Jiji la Arusha wanatuhumiwa kulipana posho kama vile hakuna kesho. Na kuna taarifa kwamba wenzao katika halmashauri za Monduli na Longido nao wanakula posho kwa kwenda mbele. Ajabu ni kwamba madiwani hawa ni wale kutoka vyama vya upinzani ambao walitarajiwa wangekuwa mfano wa uadilifu. Ntibenda alishindwa kuwathibiti.

Wilayani Ngorongoro habari za Ntibenda kuondolewa zilipokewa kwa shangwe. Ntibenda, akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa anatuhumiwa kuhusika moja kwa moja na dhuluma dhidi ya wafugaji Ngorongoro. Na hili ni somo kwa Gambo, amsaidie rais kutatua migogoro ya ardhi katika Mkoa wa Arusha.

Sasa narejea katika mada ya leo; double standards (kigeugeu) cha kiongozi wa umma, Freeman Mbowe, Mbunge wa Jimbo la Hai. Mbowe ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa. Vile vile ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Mbowe, kwa nyakati tofauti, alitoa kauli tofauti kwa matatizo yanayofanana. Kauli zake tata ni nyingi. Nitajadili baadhi.

Kwanza, Mbowe alionesha misimamo miwili tofauti kuhusu migogoro ya ardhi katika wilaya za Bagamoyo na Hai. Mei 19, 2016 katika Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Mbowe alitaka kufahamu ni kwa nini serikali imeshindwa kuliendeleza shamba la miwa la Bagamoyo ambalo lingeweza kusaidia kuzalisha sukari.

Mbowe anazungumzia mradi wa kilimo cha miwa, zao lenye kiu kupindukia, katika Wilaya ya Bagamoyo. Agro EcoEnergy kampuni kutoka Swiden ilitamani kulima miwa na kujenga kiwanda cha sukari. Gazeti la Guardian la Uingereza la Oktoba 21,  2015 liliripoti kwamba sukari hiyo na ethano itakayozalishwa na Agro EcoEnergy ni kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi.

Mradi huo, wenye thamani ya dola za Marekani milioni 500 ulikabiliwa na upinzani mkali. Wakazi zaidi ya 1,200 wanaotumia ardhi hiyo yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 22,000 walitaka walipwe fidia. Vile vile hawakufahamu wangehamia wapi hata kama wangelipwa fidia. Upinzani huo ulisababisha mmoja wa wawekezaji wakubwa wa mradi huo, SIDA ya Swiden, kujitoa.

Mbowe, kwa maneno yake, alisema; “Ni kwa namna gani serikali imeshindwa kuliendeleza shamba la Bagamoyo ambalo uanzishwaji wake ulianza tangu mwaka 2006 ambapo tungezalisha tani 120,000.” Haleluya! Majaliwa, kwa bahati nzuri, hana mzaha.

Alimjibu Mbowe kuwa mradi wa kilimo cha miwa Bagamoyo ungeyakausha maji Mto Wami na kuhatarisha maisha ya binadamu pamoja na viumbe vingine ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani.

Kauli ya Majaliwa ni ushindi kwa wakazi wa Bagamoyo. Lakini pia ni ushindi kwa wadau wengine wengi waliopambana kwa miaka kadhaa kupinga mradi huo.

Pamoja na hayo kuna vitu vichache sana vitamu kama sukari. Na kwa kuwa Dk. Magufuli alipiga marufuku uagizaji holela wa sukari, ili kulinda walaji pamoja na viwanda, ghafla tamtam hiyo iliadimika mno. Mbowe akapata fursa adimu ya kulitumia bunge kupiga siasa.

Wakati Mbowe akiitaka serikali kuwahamisha watu katika ardhi yao katika Wilaya ya Bagamoyo, Mbowe huyo huyo anapinga mradi wa serikali wa kuwahamisha watu katika wilaya za Hai na Meru ili kupanua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Mafisadi, wanaojificha nyuma ya pazia la kupanua KIA, wanajaribu kupora ardhi yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 11,000. Uporaji huo utaviathiri vijiji vya Sanya Station, Chemka na Mtakuja katika Wilaya ya Hai kwa upande mmoja na Majengo, Samaria, Malula na Maroroni katika Wilaya ya Meru. Mbowe, kwa nia njema, amekuwa mtetezi mkubwa wa ardhi hiyo.

Mbowe hakosi usingizi wakazi wa Bagamoyo wakipoteza hekta 22,000. Mbowe yule yule anaumia sana wakazi wa Hai na Meru wakipoteza hekta 11,000. Wakazi wa Bagamoyo wanatofauti gani na wakazi wa Hai na Meru? Au tuseme ni kwa sababu Mbunge wa Bagamoyo anatokana na chama tawala wakati wabunge wa Hai na Meru wanatokana na chama cha upinzani? Hivi wanaodai kuwa baadhi ya vyama vya siasa vina dalili za kuendekeza ukanda wanakosea?

Pili, Mbowe aliwahi kusema kuwa Edward Lowassa hafai kuiongoza Tanzania. Mbowe,  aliwatahadharisha Watanzania dhidi ya genge la waganga njaa lililokuwa likimpigania Lowassa. Mbowe alionya, “Hao wanaomtaka Lowassa ni wale wanaojua watanufaika binafsi (Lowassa akiwa rais).” Ghafla Mbowe akabadilika na kuanza kuimba sifa na utukufu kwa Lowassa.

Baada ya kuiweka pembeni agenda safi ya upinzani ya vita dhidi ya ufisadi Mbowe alijaribu kuuaminisha umma, bahati nzuri bila mafanikio, kuwa Lowassa ndiye hasa anafaa. Wakati mwingine unajiuliza hivi Mbowe huwa anajitazama kwenye kioo?

Washirikina hufanya matambiko Septemba. Septemba 8, 1900 kimbunga kibaya kuliko vyote katika historia ya Marekani kilipiga Texas na kuua watu zaidi ya 8,000. Septemba mosi, 1939 majeshi ya Adolf Hitler yalivamia Poland na kuanza Vita ya Pili ya Dunia.

Shambulizi kubwa zaidi duniani lililowaua watu takriban 3,000 Marekani lilitokea Septemba 11, 2001. Jaribio la kumpiga risasi Rais wa Marekani, Gerald Ford, lilifanyika Septemba 5, 1975. Majeshi ya Hitler yaliteketeza Jiji la London Septemba 7, 1940. Wapiganaji wa Black September waliuwaua watu wengi mjini Munich, Ujerumani Septemba  5, 1972.

Mbowe na wenzake nao, makusudi au kwa kutokujua, wamepanga kufanya maandamano nchi nzima kupinga kile wanachokiita udikteta wa Dk. Magufuli tarehe 1 Septemba 2016. Bila shaka watu wengi watajitokeza kumuunga mkono kiongozi wa chama chao.

Sina tatizo na mashabiki wa Mbowe wanaompenda kwa dhati bila kujali upungufu wake maana ni binadamu. Sina tatizo na mashabiki wanaokataa kuhoji jambo lolote linalofanywa na kiongozi. Sina shida pia na wale wanaomshabikia, kana kwamba wameng’olewa ubongo, kwa sababu ya matumaini ya kupendelewa kupata fursa, hasa vyeo, ndani na nje ya chama.

Ugomvi wangu ni kuwatumia vijana wasio na hatia hasa wale wasio na uwezo wa kuhoji mienendo ya viongozi wa umma. Vijana ninao watetea ni wale wasio na uwezo au nafasi ya kukumbuka alichokisema kiongozi jana na kukilinganisha na anachokisema leo.

Hawa ni vijana walio wengi wanyonge, waliojikatia tamaa wasiofahamu pakukimbilia. Ikitokea mechi kama hakuna kiingilio watatembea kwenda kutazama maana hawana kazi. Kukiwa na maandamano, hata kama hawaelewi mantiki yake, wao watajitokeza tu. Hawana cha kufanya.

Luka 17:1-2 inaonya, “…Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa (vijana) wadogo hawa.”

Chanzo. Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates