Uingereza imetakiwa kuchukua hatua za haraka kuandaa mkakati wa kuzuia makosa ya kibaguzi kwa baadhi ya makundi ya watu wachache ambayo yanaiweka nchi hiyo katika hatari ya kuwa na jamii yenye mgawanyiko.
Tume ya usawa na Haki za Binadamu EHRC, asasi ya umma Uingereza imeitaka serikali ya nchi hiyo kuja na mikakati madhubuti na ya muda mrefu kushughulikia ukosefu wa usawa na ubaguzi dhidi ya jamii za watu walio wachache
Ripoti zinasema tangu Uingereza ipige kura ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya vitendo vya kibaguzi na makosa ya chuki vimeongezeka ambapo katika utafiti uliofanywa na kamisheni hiyo kwa miaka takribani mitano sasa hali ya maisha kwa vijana wanaotoka jamii ya watu weusi imekuwa ikizidi kuwa mbaya hasa katika upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii kama elimu na afya
Mwenyekiti wa tume hiyo David Issa ameitaka serikali ya Uingereza kuanzisha mikakati mipya ya kupunguza ubaguzi wa rangi katika mfumo wa kukabiliana na uhalifu katika idara ya mahakama, elimu na katika ajira
Katika ripoti hiyo iliyotolewa leo Isaac anasema chuki dhidi ya wageni na watu wa jamii ya walio wachache imeongezeka na jambo la kutia wasiwasi linahitaji kushughulikiwa mara moja
Watu weusi wako katika hatari ya kuuwawa mara moja zaidi ikilinganishwa na watu weupe nchini humo hasa England na Wales na mara tatu zaidi wanaweza kushitakiwa na kufungwa kitendo kinachoashiria kutokuwepo kwa usawa
" Ukiwa mtu mweusi au mtu kutoka jamii yoyote ndogo Uingereza inaweza kukufanya ujisikie kama unaishi katika ulimwengu tofauti kabisa" amesema David Isaac mwenyekiti wa tume hiyo
Isaac amesema alitiwa moyo na kauli ya Waziri mkuu wa nchi hiyo Thereza May, alieonesha nia ya kukabiliana na ubaguzi, lakini hata hivyo ameionya serikali na kuitaka itekeleze kauli hiyo ya waziri mkuu kwa vitendo.
Ubaguzi katika ajira na mishahara
Moja kati ya maeneo yanayolalamikiwa kutokuwa na usawa ni pamoja na sehemu za kazi ambapo watu wenye asili ya Afrika na asia wamekuwa wakilipwa ujira mdogo ikilinganishwa na watu weupe
Watu weupe wana uwezekano mkubwa wa kupata ajira katika nafasi nzuri ikilinganishwa na watu weusi lakini pia hata malipo wanayolipwa watu weusi si sawa na watu weupe licha ya kuwa na kiwago kinacholingana kielimu
Watu weusi hulipwa wastani wa 23.1 asilimia chini ya kiwango wanacholipwa wenzao ukweli unaopingana na madai kuwa, mtu anayefanya jitihada kutafuta elimu ya juu nchini Uingereza hupata mafanikio bila ya kujali asili wala rangi yake.
Waziri mkuu wa Uingereza Thereza May ameahidi kushughulikia tofauti hizo kama sehemu ya mpango wa serikali yake kujaribu kusawazisha mambo baada ya migawanyiko iliyosababishwa na kura ya maoni ya kujiondoa umoja wa ulaya
Mwandishi: Celina Mwakabwale/Reuters/AP
Mhariri:Iddi Ssessanga
Chanzo. Dw.de
No comments:
Post a Comment