Viongozi wa Ujerumani, Ufaransa na Italia wanakutana Jumatatu (22.08.2016) kujadili mustakbali wa Umoja wa Ulaya kufuatia kujitowa kwa Uingereza na mzozo wa wahamiaji uliolikumba bara hilo.
Mkutano huo unafanyika ndani ya meli ya Italia yenye kubeba ndege za kivita katika bahari ya Mediterenia karibu na kisiwa cha Ventotene nchini Italia ambapo ndiko mahala muasisi wa Umoja wa Ulaya Altiero Spinelli aliandika ilani ya kuunganishwa kwa Ulaya akiwa kifungoni uhamishoni wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Kutafanyika mkutano na waandishi wa habari baada ya viongozi hao Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi kukutana.
Suala la mzozo wa wakimbizi barani Ulaya limerudi tena kwenye agenda kufuatia msururu wa mashambulio ya kigaidi ambapo baadhi ya wanasiasa wameyahusisha na kuwasili kwa wimbi kubwa la wahamiaji barani Ulaya kutoka Mashariki ya Kati na Afrika.
Athari za kujitowa Uingereza
Uamuzi wa Uingereza kujitowa katika Umoja wa Ulaya katika kura ya maoni iliofanyika mwezi wa Juni umewafadhaisha washirika wake katika umoja huo hatua ambayo baadhi ya wanasiasa wa nchi wanachama wa umoja huo wanatowa wito kwa nchi zao kuiiga.
Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi amesema leo hii wakati akijiandaa kukutana na viongozi hao wenzake wa Ujerumani na Ufaransa kwamba Umoja wa Ulaya unahitaji kufanyiwa marekebisho.
Renzi amekaririwa akisema "inakuwa rahisi kuilaumu Ulaya kwa kila jambo....na vigumu kujenga Ulaya tafauti ambayo itazingatia zaidi maadili kuliko kujali zaidi masuala ya gharama."
Renzi ameandika hayo katika mtandao wa Facebook na kuelezea ndio sababu ya kuitisha mkutano huo na wenzake wa Ujerumani na Ufaransa. Amesema hicho ndicho wanachojaribu kufanya kwa kutumia nguvu zao zote walizonazo.
Hatua za vitendo zinahitajika
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akiwa na Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi walipokutana Berlin Juni 2016.
Wakosoaji wa umoja huo wametaka kutumika vitendo zaidi badala ya maneno linapokuja suala la kujitowa kwa Uingereza ambapo inahofiwa kwamba baadhi ya nchi zinaweza kuitisha kura ya maoni kama ile ya Uingereza hususan Uholanzi ambayo inapinga mabadiliko kwa umoja huo ili kuwa na muungano wa karibu zaidi.
Nchi kama vile Jamhuri ya Czech ,Hungary , Poland na Slovakia zimeapa kuandaa mipango yao wenyewe ili kutolimbikiza madaraka makubwa zaidi kwa Umoja wa Ulaya.
Hali ya kiuchmi ya Ulaya, mashambulio ya wanajihadi matatizo ya wahamiaji na wakimbizi, mzozo wa Syria, uhusiano na Urusi na Uturuki yote hayo yamo kwenye agenda ya mkutano huo wa leo.
Mataifa hayo matatu yenye nguvu kubwa barani Ulaya yanatarajia kuwa na msimamo wa pamoja kabla ya kufanyika kwa mkutano usio rasmi wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Bratsilava nchini Slovakia ambao utajaribu kupiga hatua mbele kufuatia kujitowa kwa Uingereza katika umoja huo ambapo Renzi amekiri kumelifanya kundi lao hilo kukabiliwa na changamoto ngumu.
Mkutano kati ya viongozi hao watatu utakuwa ni wa pili kufanyika ukifuatiwa na ule wa kwanza uliofanyika muda mfupi baada ya kujitowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya ambao viongozi hao walitowa wito wa kuwepo kwa msukumo mpya katika umoja huo.
Chanzo. Dw.de
No comments:
Post a Comment