MARA baada ya kutangazwa kwa uteuzi wa Dk. Modestus Francis Kipilimba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Tanzania (TISS) wiki iliyopita, kama ilivyo ada, baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vilianza kujadili uteuzi huo.
Baadhi ya magazeti yaliandika kwamba uteuzi wa DK. Kipilimba ni ‘wa kwanza’ kutokea kwa mtu asiye na historia ya idara hiyo kupewa nafasi kubwa namna hiyo. Kwa maneno mengine, kwamba Dk. Kipilimba si mwenye ufahamu wa masuala na majukumu ya TISS.
Hiyo ni kwa sababu, kwa mujibu wa wasifu uliotolewa na Ikulu, Dk. Kipilimba alielezwa kama mtu aliyefanya kazi katika taasisi kama Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Kabla ya kwenda mbali zaidi, ni muhimu kueleza kwamba kwa mujibu wa taarifa mbalimbali Dk. Kipilimba; msomi wa kiwango cha Shahada ya Uzamivu (PhD) katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ni kachero mbobezi aliyejiunga na TISS tangu mwishoni mwa miaka ya 1970.
Kwanini Kipilimba?
Nimebahatika kusoma vitabu na maandishi mengi kuhusu masuala ya ukachero. Kwa hapa Tanzania, nimewahi kuzungumza na makachero; wa sasa na wastaafu na kusema kweli naweza kuwa najua mawili matatu kuhusu TISS na masuala ya ushushushu.
Ili kuelewa sababu za Rais Dk. John Magufuli kumteua Dk. Kipilimba, ambaye ni mhitimu mwenzake wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ni muhimu kuelewa mabadiliko makubwa yaliyoikumba tasnia ya ukachero katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.
Kwenye miaka ya 1960 mpaka 1980, jukumu kubwa la makachero lilikuwa ni kukusanya taarifa kutoka popote zilipo. Watu mahiri zaidi katika kazi hiyo, walikuwa ni wale waliokuwa na uwezo wa kupenya popote kutafuta na kuzipata taarifa muhimu kuhusu usalama wa taifa.
Ndiyo sababu, duniani, kulikuwa na makachero wa aina ya kina Kim Philby kutoka katika lile kundi maarufu la The Cambridge Five. Wakati huo, Marekani ilikuwa inatafuta Warusi wa kuwaibia siri zao huku Warusi nao wakitafuta Waingereza (kama Philby) na Wamarekani wa kuwasaidia kazi zao.
Hapa Tanzania, kwenye miaka hiyo, kulikuwa na michapo ya watu waliofikia hatua ya kuishi kama watu waliorukwa akili (vichaa) kwa lengo tu la kupata taarifa.
Ndiyo maana, kuna vichaa wengi waliopachikwa jina la ‘watu wa usalama’ kwenye miaka hiyo kwa sababu kulikuwa na minong’ono mingi kuhusu watu wa namna hiyo.
Kwenye miaka ya 1990 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, jukumu lilibadilika kutoka ukusanyaji wa taarifa na kuwa uchambuzi wa taarifa.
Kwa mujibu wa taarifa za kikachero hata hapa kwetu mtazamo umekuwa ni huo huo wa uchambuzi wa taarifa na nyingi ya hizo zikiweza kupatikana kupitia vyombo vya habari.
Hivyo, kwa vile taarifa zilianza kupatikana kupitia vyanzo vingine, jukumu kubwa la mashushushu lilikuwa ni kuwa na watu wenye uwezo wa kufanya uchambuzi wa taarifa hizo.
Hatua hiyo inaeleza tu namna majukumu ya ushushushu yalivyobadilika. Leo hii majukumu hayo yameingia katika hatua nyingine mpya.
Kwa wafuatiliaji wa vyombo vya habari, watakuwa wanafahamu kuhusu namna Marekani inavyohangaishwa na akina Edward Snowden na Julian Assange. Hawa ni watu wanaosumbua kwa ujasusi wa kimtandao.
Hivyo, kwa sasa, kwa vile taarifa nyingi zaidi zinaweza kupatikana kupitia teknolojia ya habari na mawasiliano; ni sifa ya ziada kuwa na kachero namba moja ambaye ni mbobezi kwenye eneo hilo.
Mtu akitaka kupata kupata taarifa za awali kuhusu Ezekiel Kamwaga, anaweza kwenda kwenye akaunti yangu ya facebook na kupata picha ya kwamba mimi ni mtu wa namna gani.
Akitaka kwenda ndani zaidi, atatafuta namba yangu ya simu na kuangalia watu ninaowasiliana nao, muda gani na natuma meseji za namna gani na kwa watu gani. Hizi taarifa zote zipo shukrani kwa maendeleo ya kiteknolojia.
Hili ni eneo ambalo Dk. Kipilimba analifahamu vema. Si kwamba amesomea tu lakini amefundisha pia katika vyuo vikuu vya kimataifa.
Shahada ya kwanza amesoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika masuala ya Kompyuta, Shahada ya Uzamili (Masters Degree) alisoma nchini Uingereza katika Chuo Kikuu cha Salford, Manchester akizama kwenye masuala ya kompyuta tangu Septemba 1992 hadi Novemba 1994.
Shahada ya Uzamivu (PhD) alisoma tena hapohapo Salford kutoka Februari 2002 hadi Septemba 2005. Msomi huyo amefundisha kwenye vyuo vikuu kadhaa nchini humo.
Hivi sasa, kuna mambo makubwa ya kiusalama yanayofanyika kiteknolojia. Ni wazi kwamba uteuzi huu wa Dk. Kipilimba una lengo la kuwa na mtu ambaye anajua kinachoendelea na ataweza kufanya maboresho yatakayosabisha TISS iende kisasa zaidi.
Katika kitabu maarufu cha mwanazuoni wa Kichina, Lao Tzu; The Art of War; inaelezwa kwamba jeshi au taifa lililoendelea zaidi kikachero, lina nafasi nzuri zaidi ya kushinda vita kuliko lile lililo nyuma.
Kipilimba ni nani?
Mara baada ya kutangazwa kwa uteuzi wake, nilifanikiwa kuzungumza na baadhi ya wafanyakazi wa BoT kujaribu kupata picha ya kachero huyu ni mtu wa namna gani.
Kwanza niliambiwa kwamba ni mtu asiyejikweza. Kwamba kama humjui yeye ni nani, usingeweza kujua kwamba ni ofisa wa ngazi za juu kwa sababu hakupenda kujionyesha.
Wakati akiwa BoT, mojawapo ya sifa zake kuu kwenye vikao vya ngazi za juu alivyokuwa akishiriki ni kwamba alikuwa mtetezi wa haki za wafanyakazi. Nilielezwa kuwa ni mtu aliyekuwa hapendi uonevu au kumnyimwa mtu haki yake.
Hili linaelezwa na sifa yake nyingine ya pekee –kwamba yeye pia ni mcha Mungu. Dk. Kipilimba ni Mkristo na ni mchamungu kiasi kwamba huhubiri katika Kanisa analofanya kazi.
Yeye na mkewe, Dk. Bertha Kipilimba ni wachungaji katika Kanisa la Dar City Harvest. Katika mitandao ya kijamii wiki iliyopita, kulikuwa na picha zilizomuonyesha kachero huyu akiwa katika mojawapo ya matukio ya kanisa lake hilo.
Sasa litakuwa ni suala la kusubiri endapo ataendelea kuhubiri katika wakati huu ambapo sasa anafahamika rasmi kwa kazi yake anayoifanya.
Sifa hii ya ulokole inaeleza pia kuhusu tabia nyingine mbili za kipekee za Dk. Kipilimba; Uaminifu na Uadilifu.
“ Huyu bwana hajawahi kufanya biashara ya aina yoyote katika maisha yake. Kimsingi, naweza kukuthibitishia kwamba hajawahi kumiliki hata duka katika maisha yake,” mmoja wa marafiki wa Dk. Kipilimba aliniambia katika mazungumzo naye wiki hii.
Katika dunia hii iliyojaa majaribu na katika jamii ya kimasikini kama ya Tanzania, ni muhimu kuwa na kiongozi katika idara nyeti kama TISS ambaye ana hofu ya Mungu na hajawahi kuendeshwa na tamaa ya mali.
Rashid Othman Vs Modestus Kipilimba
Nimefanikiwa kumfahamu kwa kiasi Rashid Othman (RO)- mtangulizi wa Dk. Kipilimba (MK) katika nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa TISS.
RO ni zao la kizazi cha nyuma cha makachero kabla ya kina Dk. Kipilimba. Othman ni mtu aliyelelewa na kukulia katika idara hiyo na alikuwa akiifahamu kama kiganja chake.
Othman alifundishwa kazi na kizazi cha kwanza cha makachero wazalendo. Kama wewe ni wale wanaoitwa ‘watoto wa mjini’, Othman angeweza kuzungumza nawe kimjinimjini na kama wewe ni wa kijijini, RO angeweza kuzungumza nawe katika namna uliyotaka.
Sifahamu ni lugha ngapi za Tanzania ambazo RO alikuwa akiweza kuzizungumza kwa ufasaha lakini nimewahi kumsikia akizungumza zaidi ya lugha tano za hapa nchini. Ni tabia hizi ambazo pengine zilimfanya apate taarifa popote alipotaka hapa nchini.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, alipata kusema huko nyuma kwamba ukizungumza na mtu kwa lugha anayoilewa, utaiteka akili yake lakini ukizungumza kwa lugha yake utauteka moyo wake.
Bahati nzuri kwa Othman ni kwamba alipata fursa ya kufanya kazi barani Ulaya baadaye katika utendaji wake na aliporejea nchini ilikuwa rahisi kwake kuingiza mambo mapya.
Kwenye awamu ya pili ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, kulikuwa na maboresho makubwa katika eneo la TEHAMA na kiusalama, Othman anasifiwa kwa kuingiza maboresho hayo, hususan, katika masuala ya usalama.
Ukiwa na Othman, mngeweza kuzungumza kuhusu Simba na Yanga, Sikinde na Msondo na Manchester United (Man U) na Liverpool (LFC). Nimezungumza na mmoja wa marafiki wa Kipilimba na ameniambia kuwa hajui kama kachero huyu ni shabiki wa Simba wala Yanga.
Kimsingi, aliniambia haijawahi kutokea katika mazungumzo yao wakazungumzia habari za mchezo wa mpira. Na hawawezi pia kuzungumzia habari za Msondo na Sikinde kwa sababu rafikiye ni mchungaji.
Faida aliyonayo Dk. Kipilimba ni kwamba amepata pazuri pa kuanzia baada ya Othman. Tayari msingi wa kuelekeza idara ya usalama katika zama mpya za sayansi na teknolojia umewekwa naye kazi yake sasa itakuwa ni kuongoza mabadiliko hayo.
Wapo watu ndani na nje ya idara hiyo wanaotamani pafanyike mabadiliko kadhaa, na wanamwona yeye kama anayetamani mabadiliko pia, hivyo bila shaka tutaona hayo mabadiliko siku si nyingi.
Dk. Kipilimba ana faida moja ambayo watangulizi wake hawakuwahi kuwa nayo. Katika takribani miaka yake 30 ya utumishi, ametumia theluthi moja tu kufanya kazi ndani ya idara na theluthi nyingine mbili nje ya idara; ikiwamo ndani na nje ya nchi.
Hii ni faida kwa sababu ana mtazamo mpana wa ndani na nje. Kama angekuwa ni mtu asiyejua kitu kuhusu ndani, kungekuwa na hatari ya kuingiza “usasa” mwingi ambao pengine usingekubalika na kama angekuwa wa ndani sana; kungekuwa na hatari ya kuwa mhafidhina asiyekubali mabadiliko.
Kachero mwandamizi
Kwa mujibu wa taarifa zilizo rasmi, Kipilimba alijiunga na TISS mwishoni mwa miaka ya 1970. Wakati huo, vijana waliojiunga na idara hiyo walikuwa wamechunguzwa kwa muda mrefu na kufanyiwa usaili wa kutosha.
Hakuna taarifa za kutosha sana kumhusu lakini inajulikana kwamba kwenye miaka ya 1980, alikuwa akifanya kazi za kiusalama katika Sekretarieti ya Usalama iliyopo Ikulu ambayo ndiyo hufanya uchambuzi wa taarifa zote kutoka mikoani.
Ni wakati huo ambao Mkuu wa Sekretarieti alikuwa Bernard Membe ambaye baadaye alikuja kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Alijiunga na BoT mwaka 1995 kama ofisa katika idara ya mambo ya teknolojia ya mawasiliano; huku mmoja wa mabosi wake akiwa ni Charles Kitwanga (aliyekuja kuwa Waziri wa kwanza wa Mambo ya Ndani kwenye serikali ya Rais Magufuli).
Kati ya mwaka 2000 au 2001, Kipilimba ‘alipotea kazini’ katika mazingira ya kutatanisha. Mabosi wake BoT walikuwa wamemhamishia Arusha kikazi kutoka Dar es Salaam alikokuwa akifanya kazi awali.
Ni muda huo ‘aliopotea kazini’ ndio alioutumia kwenda kusoma masomo yake ya uzamivu pamoja na kufundisha katika vyuo vikuu nchini Uingereza.
Baadhi ya wafanyakazi wa BoT wameeleza mshangao wao kwa kitendo cha mfanyakazi wa taasisi hiyo kuacha kazi mwenyewe na kisha kurejeshwa. Mara nyingi BoT huwa haiwarejeshi wafanyakazi walioacha kazi wenyewe.
Bila shaka, wafanyakazi hawa hawakuwa na uelewa kuhusu ‘kazi nyingine’ ya Dk. Kipilimba tofauti na ile waliyokuwa wakiifahamu pale BoT. Alirejea BoT kama mshauri wa Gavana, Profesa Benno Ndullu, mwaka 2000 kabla ya kuajiriwa tena mwaka 2011.
Uhusika kwenye Infosys
Kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii na baadhi ya magazeti, kuna taarifa za kumhusisha Dk. Kipilimba na kampuni ya Infosys inayotajwa katika kashfa ya mfanyabiashara Said Lugumi.
Kwenye taarifa hizo, inaelezwa kwamba Dk. Kipilimba ni mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo na uteuzi wake kuwa bosi wa TIS unaweka ukakasi.
Ingawa ni kweli kwamba Dk. Kipilimba amewahi kufanya kazi na watu wanaomiliki Infosys; walikuwa mabosi wake BoT, si kweli kuwa naye ni mmiliki.
Ndani ya BoT inafahamika kwamba mojawapo ya sababu za kuhamishwa kwake kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha kama nilivyoeleza hapa juu, ilikuwa ni kuzorota kwa uhusiano kati yake na Kitwanga.
Vyanzo kadhaa vinasema Kitwanga na Kipilimba hawajawahi kuwa na uhusiano wa kibiashara, na kimsingi bosi huyo mpya wa TISS hajawahi kufanya biashara ya aina yoyote.
Kutajwa kwake Infosys pengine kunatokana na ukweli kwamba baadhi ya wamiliki wa kampuni hiyo ni watu aliowahi kufanya nao kazi kwa karibu.
Kuliko bosi mwingine yeyote wa TISS, Dk. Kipilimba anachukua nafasi hiyo katika nyakati ambazo sasa zinafahamika kama “Zama za Habari na Taarifa”. Ofisi yake na yeye binafsi watamulikwa kuliko katika wakati mwingine wowote.
Changamoto zake pia ni za kipekee; uhalifu wa kimtandao na ugaidi; ambao kimsingi ni vita dhidi ya adui asiyejitambulisha waziwazi.
Katika wakati ambao Tanzania inamulikwa kimataifa kutokana utajiri wake wa rasilimali kama vile gesi, mafuta, madini na makaa ya mawe; Dk. Kipilimba atakuwa na kazi kubwa kuhakikisha kwamba njia ya kiuchumi kuelekea Uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025 inafikiwa pasipo hujuma za kiuchumi.
Dk. Kipilimba ambaye amesoma katika Sekondari za Kigonsera mkoani Ruvuma na Mkwawa mkoani Iringa alifunga ndoa mwaka 1988 na ana mke na watoto watatu.
Chanzo. Raia mwema.
No comments:
Post a Comment