Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean- Claude Juncker amefichua mapendekezo kadhaa ya kufufua hali ya uaminifu unaoporomoka wa Umoja huo baada ya kura ya Uingereza ya kujitoa katika umoja huo ya Brexit.
Mapendekezo hayo ni pamoja na makao makuu mapya ya ulinzi na pia utengenezaji wa nafasi za kazi pamoja na kuimarisha ukaguzi wa mipaka.
Juncker amewtoa wito wa kuanzisha makao makuu ya jeshi la Umoja wa ulaya ili kuratibu juhudi kuelekea kuunda jeshi la pamoja ambapo baadhi ya mali zake zinamilikiwa na Umoja wa Ulaya. Lakini alisisitiza kwamba mipango hiyo haitachafua mahusiano na Jumuiya ya NATO, ambayo ina wanachama wengi ndani ya Umoja huo.
Uingereza , ambayo ilipiga kura kujitoa kutoka Umoja huo Juni 23 , hapo kabla ilipinga vikali hatua zozote kuelekea kuwa na jeshi la pamoja la Umoja wa Ulaya.
Juncker pia alishauri kumfanya mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja huo Federica Mogherini kuwa waziri kamili wa mambo ya kigeni wa kundi hilo la mataifa na kumpa kiti katika meza ya majadiliano katika mzozo wa Syria.
Amesisitiza kwamba Umoja wa ulaya unapaswa kufanya vya kutosha katika nyanja ya ulinzi, kwa kuanza kuunda makao makuu ya jeshi na kufanyakazi kuelekea kuwa na jeshi la pamoja la mataifa hayo, akisisitiza kuwa ushawishi wa kiuchumi na kitamaduni wa mataifa ya Ulaya hautoshi kulinda nafasi yake katika ulimwengu huu wa sasa.
Umoja wa kijeshi
Juncker ambaye ni mkuu wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya , alisema katika hotuba hiyo kuu kwamba muungano wa mataifa hayo , unapaswa kuwa imara kijeshi.
"Nina imani kwamba tunapaswa kulinda jinsi tunavyoishi. Nina hisia kwamba wengi wamesahau vipi watu wa Ulaya wanavyoishi. Nina hisia kwamba wengi wamesahau kuwa kama mtu wa Ulaya na kuwa sehemu ya Umoja wa Ulaya wa Umoja huu wa mataifa ya Ulaya."
"Kwa pamoja ni lazima tuwe na hakika kwamba tunalinda masilahi yetu," Juncker aliwaambia wabunge wa bunge la Ulaya mjini Strasbourg, nchini Ufaransa.
Rais Obama ataka Ulaya imara zaidi
Mapema mwaka huu rais wa Marekani Barack Obama aliyataka mataifa ya Ulaya kufanya vya kutosha ili kuhimili vishindo vya kitisho cha usalama kama vile kutoka kwa kundi la Dola la Kiislamu.
"Tunahitaji Ulaya imara ili kuweza kumudu mzigo wake, ikifanyakazi nasi kwa niaba ya usalama wetu wote," alisema Obama mjini Hannover , nchini Ujerumani , mwezi Aprili.
Kutokana na hali ya kimabavu inayooneshwa na Urusi , matumizi ya nguvu ya Waislamu wenye itikadi kali , na mashambulizi ya mtandaoni pamoja na changamoto nyingine za kisasa, maafisa wa NATO na Umoja wa Ulaya, wanasema wanashirikiana kwa sasa kwa karibu kuliko ilivyokuwa huko nyuma.
Lakini katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alionya mapema mwezi huu kwamba , "jambo ambalo tunapaswa kuliepuka ni kuwa na kitu kimoja mara mbili."
Iwapo mapendekezo ya Juncker yataidhinishwa , itakuwa ni hatua kubwa katika ushirikiano wa kijeshi katika Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / dpae
Mhariri: Yusuf Saumu
Chanzo. Dw.de
No comments:
Post a Comment