Marekani na Urusi zimefikia makubalinao kuhusu mchakato wa kupatikana amani nchini Syria ikiwemo kusitishwa kwa mapigano kote nchini Syria kuanzia Jumatatu wiki ijayo.
Makubaliano hayo pia yanajumuisha kuimarisha shughuli za kutolewa kwa misaada na opereshenzi za pamoja za kijeshi kupambana dhidi ya makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali.
Makubaliano hayo yaliyofikiwa mapema Jumamosi (10.09.2016) kati ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov yanafuatia mazungumzo ya kina yaliyokuwa yakifanyika mjini Geneva, Uswisi.
Lavrov amesema licha ya kuendelea kutoaminiana kati ya pande hizo mbili, wamefanikiwa kuafikiana kuhusu jinsi ya kushirikiana kupambana dhidi ya ugaidi na kuyafufua mazungumzo ya kisiasa ya kupatikana amani nchini Syria kwa njia bora zaidi.
Je mzozo wa Syria utakoma sasa?
Kerry ambaye alichelewesha kwa siku moja safari yake kutoka Geneva na kurejea Marekani ili kuhakikisha wamefikia makubaliano na mwenzake wa Urusi amesema utawala wa Rais wa Marekani Barack Obama unajituma zaidi katika kuutatua mzozo wa Syria kwasababu wanaamini Urusi ina uwezo wa kuushinikiza utawala wa Rais wa Syria Bashar al Assad kusitisha vita na kuja katika meza ya mazungumzo ili kupatikane amani nchini humo.
Kerry ameongeza kusema kuwa msingi wa mazungumzo hayo ya Geneva ilikuwa ni makubaliano kuwa serikali ya Syria haitafanya mashambulizi ya angani kwa kisingizio cha kuwasaka wapiganaji wa kundi la wanamgambo wenye itikadi kali wa al Nusra Front, linalofungamanishwa na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani amesema kusitishwa huko kwa mashambulizi ya angani katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi kutafikisha kikomo matumizi ya mabomu ya mapipa na mashambulizi ya kiholela na ina uwezo wa kubadili mkondo wa mzozo wa Syria.
Marekani na Urusi zimekubaliana iwapo mapigano yatapungua, nchi hizo mbili zitashirikiana kufanya operesheni za kijeshi kwa pamoja dhidi ya Al Nusra na kundi la wanamgambo wenye itikadi kali la Dola la Kiislamu IS.
Chini ya makubaliano hayo pande zote zinazohusika zinapaswa kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano kote nchini Syria, kusitisha mashambulizi yote yakiwemo ya angani, kutojaribu kuyadhibiti maeneo mapya wakati wa kusitishwa kwa mapigano, kuruhusiwa kwa misaada ya kibinadamu kufika katika maeneo yaliyozingirwa ikiwemo katika mji unaodhibitiwa na waasi wa Aleppo.
Umoja wa Mataifa siku ya Ijumma ulisema serikali ya Syria imezuia misafara ya magari ya kutoa misaada ya kibiandamu mwezi huu kuingia katika mji wa Aleppo na mji huo unakumbwa na hatari ya kuishiwa mafuta katika kipindi cha wiki moja ijayo na hivyo kuyafanya mazungumzo kuhusu Syria kushughulikiwa kwa dharura zaidi.
Marekani na Urusi kushirikiana kijeshi
Iwapo hayo yatazingatiwa kuanzia Jumatatu wiki ijayo, Urusi na Marekani zitaanza siku saba za kazi za maandalizi ya kuunda kituo cha pamoja cha kuteleza shughuli zao za kijeshi Syria ikiwemo kubadilishana taarifa kuhusu maeneo yanayodhibitiwa na wanamgambo na kuhusu makundi ya upinzani.
Marekani na Urusi zimekuwa kila moja ikiunga mkono upande tofauti katika vita vya wenyewe kwa wenyewe Syria ambavyo havionyeshi dalili ya kukoma hivi karibuni hata baada ya miaka mitano ya mzozo ambao umesababisha nusu ya idadi ya Wasyria kuyahama makaazi yao, maelfu kuuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
Katika mzozo huo, Urusi inamuunga mkono Rais Bashar al Assad huku Marekani ikiunga mkono upinzani unaotaka kumng'oa madarakani Rais Assad. Pendekezo la Kerry la ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi yake na Urusi limekumbwa na upinzani kutoka kwa maafisa wa Marekani wa ulinzi na wa kijasusi wanaodai Urusi haiwezi kuaminiwa.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp
Chanzo. Dw.de
No comments:
Post a Comment