Social Icons

Friday, 6 September 2013

HAYA NDIYO WALIYOKUBALIANA MUSEVENI, KAGAME NA UHURU KENYATA.....


Wiki iliyopita Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na Rais wa Rwanda, Paul Kagame walikutana Mombasa nchini Kenya na kuzindua mradi mkubwa wa ujenzi wa reli.

Katika uzinduzi huo marais hao wameweka muda wa kuanza kwa miradi mitatu mikubwa. Mosi kuanza kwa mradi wa ujenzi wa reli kutoka Mombasa-Kampala mpaka Kigali, ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Eldoret-Kampala mpaka Kigali na kujenga miundombinu ya umeme wa uhakika.

Pia wamewaagiza mawaziri wa fedha wa nchi hizo kuandaa mapendekezo ya utekelezaji wa miradi hiyo mitatu na taarifa ya mapendekezo hayo wanatakiwa kuitoa kwa marais hao katika mkutano ujao.

Wanazungumza lugha moja

Kwa mujibu wa mratibu wa miradi hiyo, Monique Mukaruliza, ujenzi wa bomba la kusafisha mafuta kutoka Eldoret-Kampala mpaka Kigali, unatarajiwa kukamilika 2017 huku  kabla ya mwisho mwa mwaka huu, viongozi wa  nchi hizo wamekubaliana kuzindua ushuru wa pamoja wa forodha kwa ajili ya kusafirisha bidhaa kwa masharti nafuu kutoka nchi moja hadi nyingine.

Wakati hayo yakiendelea, taarifa zinaeleza kwamba ujenzi wa reli hiyo utagharimu Dola 3.5 bilioni, lakini taarifa nyingine zinasema kwamba mradi huo una thamani ya Dola 13 bilioni na mradi huo utakamilika mwaka 2018 huku ujenzi wa awali wa mradi wa reli kutoka Mombasa mpaka jijini Nairobi unatarajiwa kuanza Novemba, mwaka huu.

Vilevile kuanzia Januari mwakani,  Rais wa Kenya, Kenyatta na Kagame wamekubaliana kwamba wananchi wao waanze kutumia vitambulisho vya uraia kusafiria katika nchi hizo wakati Uganda itatumia kadi ya kupiga kura kusafiri Kenya na Rwanda.

Mbali na hayo taarifa iliyotolewa hivi karibuni imebainisha kwamba katika mkutano wa pili uliofanyika Mombasa wiki iliyopita, marais hao waliwaagiza mawaziri wa fedha wa nchi hizo kuandaa mapandekezo ya utekelezaji wa miradi hiyo ndani ya mwezi mmoja na nusu ujao.

Wataalamu wa masuala ya uchumi, wanabainisha kwamba reli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba mizigo na kwenda kilometa 80 kwa saa wakati itakapoanza kusafirisha mizigo katika ukanda huo.

Bandari ya Mombasa, inategemewa kwa zaidi ya asilimia 50 na Rwanda katika kuagiza mizigo huku ikitegemewa na Uganda, Mashariki mwa Demokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Kaskazini mwa mikoa ya Tanzania na Sudani Kusini.

Burundi na Sudani Kusini

Katika mkutano huo marasi wa nchi hizo tatu walikubali kuijumuisha Burundi na Sudani Kusini katika miradi hiyo baada ya kuhudhuria mkutano huo kama wageni waalikwa.

Chanzo:- Mwananchi



No comments:

 
 
Blogger Templates