*Msemaji wa Jeshi awatumia salamu M-23
HALI ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inazidi kuwa tete tangu kuvuja kwa taarifa za serikali ya Rwanda kupeleka bataliani mbili zenye wanajeshi 1,700 ili kukabiliana na kile kinachoonekana kuwa kishindo cha vikosi vya Umoja wa Mataifa vyenye jukumu la kulinda amani katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa kiraslimali.
Habari za uhakika kutoka vyanzo vya habari vya kuaminika zinaeleza kwamba, hatua ya Rwanda kupeleka wanajeshi wa ziada katika eneo hilo ambalo limekuwa katika mapigano kwa muda mrefu sasa kati ya waasi na vikosi vya DRC vinavyosaidiwa na vile vya Umoja wa Mataifa (MONUSCO) inakuja baada ya waasi wa kundi la M23 kupata kipigo kikali katika siku za hivi karibuni.
Taarifa ambazo Mtanzania Jumapili imezinasa kutoka katika uwanja wa mapambano na ambazo zimegusa vichwa kadhaa vya habari zinaeleza kuwa, brigedia maalum ya vikosi vya UN yenye dhamana ya kujibu mashambulizi (FIB) katikati ya wiki hii iliendesha operesheni kubwa iliyoharibu kabisa ngome muhimu ya waasi wa M23 hali inayotajwa na wachambuzi wa mambo kuwa ndiyo iliyoishtua serikali ya Rwanda ambayo inatuhumiwa kuwasaidia waasi hao.
Taarifa za kijeshi zinaeleza kuwa, FIB ambayo inaundwa na wanajeshi wapatao 3,000 kutoka Tanzania na Afrika Kusini chini ya Azimio Namba 2098 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limejizatiti kwa zana za kisasa za kivita zikiwamo mizinga na helikopta za kivita.
Taarifa kutoka mashariki ya Kongo zinaeleza kwamba, mashambulizi dhidi ya waasi wa M23 ambao hivi karibuni waliripotiwa kusababisha kifo cha mwanajeshi mmoja wa Tanzania aliye katika jeshi la UN yamesababisha waasi hao kukimbilia katika eneo la milima iliyopo umbali wa kilomita tano kutoka mji mdogo wa Kanyaruchinya Mashariki mwa Goma.
Juhudi za MTANZANIA Jumapili za kumtafuta Rais wa M23, Bertrand Bisiimwa ili aeleze sababu za vikosi vyao kuondoka katika ngome yao ya kivita sambamba na kueleza kuhusu taarifa za kuibuka kwa mapigano mapya ya hivi karibuni, hazikufanikiwa kutokana na simu zake zote za kiganjani kutopatikana.
Hali hiyo ya mambo inakuja wakati kukiwa na taarifa kwamba, tayari Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye ndiye mwenyekiti wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ameshaitisha mkutano wa wakuu wa mataifa hayo ili kujadili kuhusu mwenendo wa mambo ndani ya DRC.
Akizungumza na gazeti hili jana, Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambalo askari wake ni sehemu ya wanajeshi wa UN walioko DRC, Meja Jenerali Komba alisema anaamini kwamba shambulio lolote la waasi katika eneo hilo litajibiwa vikali.
Meja Komba ambaye hakuwa tayari kueleza iwapo alikuwa na taarifa zozote kuhusu bataliani mbili za Rwanda kupelekwa mashariki mwa DRC alikwenda mbele kwa kueleza kwamba vikosi vya MONUSCO vimejizatiti vilivyo kulinda amani na kukabiliana na uasi wowote.
“Suala la wanajeshi wa Rwanda silijui na siwezi kulizungumzia labda uliandike wewe... ila kikosi cha MONUSCO kina wajibu wa kusimamia amani ya Goma. Tutawashambulia kama waasi, hapa siwazungumzii wanajeshi wa Rwanda kama ulivyoniuliza,” alisema Meja Komba.
Hata baada ya gazeti hili kumtaka msemaji huyo kutoa kauli kuhusu habari zilizokuwa zimeandikwa katika magazeti mawili ya serikali jana ambayo yaliripoti kuhusu Rwanda kupeleka askari Kongo, Meja Komba aliendelea kushikilia msimamo wake wa kutokuwa na taarifa kuhusu kadhia hiyo.
Katika kurasa zake za mbele jana, magazeti ya serikali yalikuwa na habari kubwa inayofanana ambayo pamoja na mambo mengine ilieleza kuhusu kuibuka kwa mapigano makali kati ya vikosi vya UN na vile vya M 23 ambayo yalisababisha maangamizi makubwa dhidi ya waasi hao.
Habari hizo ambazo zilidaiwa kutolewa na vyanzo vya kuaminika zilizungumzia kuhusu hatua ya Rwanda kupeleka batalioni mbili ambazo zilikuwa zikionekana kuwa ni jitihada za kujaribu kupunguza au kukabiliana na athari za kuzidiwa nguvu kwa waasi wa M 23.
Wakati hayo yakitokea, Msemaji wa UN aliyeko Kinshasa, nchini Kongo Edmond Mulet, jana alithibitisha kuhusu taarifa za wanajeshi wa Rwanda kuingia katika eneo la Goma, mashariki mwa Kongo kwa lengo la kuwaongezea nguvu waasi walioelemewa.
Mulet ambaye aliilaani hatua hiyo alikwenda mbele zaidi na kueleza wasiwasi wake kuhusu kauli iliyotolewa na serikali ya Rwanda kwamba, Jeshi la Kongo lilikuwa limerusha makombora ndani ya nchi hiyo jirani na kusababisha madhara.
Naibu Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa alimkariri Mulet ambaye alikuwa akilipa taarifa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akisema, makombora ambayo yanaonekana kurushwa Rwanda yakitokea Kongo ni yale yaliyoelekezwa huko na waasi wa M23 na siyo na Jeshi la Kongo.
"Kwa mujibu wa Mulet matukio pekee ya makasha ya makombora yaliyoelekezwa katika ardhi ya Rwanda yalielekezwa huko na vikosi vya M23,” alieleza Balozi Lamek akimkariri Mulet.
Maelezo ya balozi Lamek yalikuwa yakiendana na yale ya Mulet mwenyewe ambaye awali alikaririwa akiyaponda madai ya Kongo kurusha makombora Rwanda kuwa ‘yasiyo na ukweli wowote’.
Taarifa zilizosambaa katika mitandao ya intaneti zinaeleza kwamba, tayari serikali ya Rwanda imetumia madai hayo ya makombora kutua katika ardhi yake kama sababu ya kutuma batalioni mbili na silaha nzito katika eneo la Giseny lililoko mashariki ya Kongo.
Msemaji wa Serikali ya Rwanda, Louise Mushikiwabo ametetea kitendo cha kupelekwa kwa zana hizo za kivita katika eneo la Giseny akisema, hatua hiyo inalenga kuimarisha ulinzi katika mpaka wake na Kongo.
Kutoka Afrika Kusini, jeshi la nchi hiyo tayari limetangaza kuwa lipo tayari kuongeza nguvu kwa wapiganaji wa vikosi vya MONUSCO vilivyoko DRC kwa kuwa linaamini kuwa lipo imara kukabiliana na vitendo vyovyote vya uchokozi.
Akizungumza na wanajeshi wa nchi hiyo katika kambi ya Thaba Tshwane, Luteni Jenerali, Derrick Ngwebi alisema kuwa UN imewaomba kuongeza zana za kivita nchini Kongo.
Alisema tayari katika kujibu ombi hilo la UN, Tanzania imeshapeleka kikosi cha mizinga wakati wao wakijiandaa kutuma helikopta za kivita zitakazosaidia brigedi ya kujihami kwa kujibu mashambulizi ya FIB kuzima uasi wa M23.
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa operesheni hizo za kujihami kwa ajili ya kuwalinda askari wa JWTZ, Meja Komba hakuwa tayari kueleza lolote kuhusu ama kuongeza nguvu ya wanajeshi au vifaa katika eneo hilo la Kongo.
“Masuala ya kupeleka wanajeshi yana taratibu zake na tena zinachukuwa muda mrefu hadi kukamilika... lakini kuna wanajeshi zaidi ya 20,000 wanaolinda amani Mashariki mwa Kongo mbona mnauliza kuhusu Tanzania tu?” alihoji Meja Komba.
Akizungumzia madhara ambayo askari wa Tanzania wameyapata katika uwanja wa mapambano, Meja Komba alisema mbali ya kifo cha mwanajeshi mmoja, kuna wengine watano ambao wamejeruhiwa.
Kwa upande wake, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mkumbwa Ali alisema hafahamu kama una mpango wa kuongeza wanajeshi nchini Kongo.
“Kwa kweli sifahamu na si rahisi, kwa sababu suala hili hutokana na maombi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN). Unajua huko ni vitani na kuna mambo mengi yanaweza kutokea kwa hiyo taarifa nyingine unatakiwa kuwauliza JWTZ,” alisema Mkumbwa.
Chanzo:- Mtanzania
No comments:
Post a Comment