Social Icons

Sunday, 1 September 2013

"VITA" YA VYOMBO VYA HABARI ISIYOKUWEPO......

  • CHADEMA yatumika kuhalalisha propaganda dhidi ya Kikwete


KATIKA siku za karibuni, kumekuwapo na hali ya sintofahamu baina ya Rwanda na Tanzania. Mwandishi Wetu, Ezekiel Kamwaga, alikuwa katika nchi hiyo ya Rwanda wiki nzima iliyopita na hii ni sehemu ya kile alichokishuhudia katika taifa hilo jirani la watu takribani milioni 12 na linalozidiwa kwa ukubwa na Tanzania, kwa zaidi ya mara 30.

WIKI iliyopita nilikuwa nchini Rwanda. Nilikuwa nikiishi katika mji mkuu wa taifa hilo, Kigali, lakini kwa sababu ya udogo wa nchi hiyo na uzuri wa barabara zake, nilifanikiwa kutembea zaidi ya kilomita za mraba 10,000 kwa muda wa siku tano- nikifika kwenye mipaka ya nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda pamoja na miji mingine.

Jambo moja kubwa nililolibaini kuhusu Rwanda ni kwamba ni taifa linalojengwa na watu wanaozungumza lugha zaidi ya moja. Mmoja wa wenyeji wangu, alikuwa ni kijana aliyezaliwa na kukulia katika kambi ya wakimbizi wilayani Karagwe mkoani Kagera. Anazungumza Kiswahili na Kinyambo vizuri tu.

Nilipotembelea gereza la Nyanza, Kusini mwa Rwanda, Mkuu wa gereza hilo alikuwa ni kijana mwingine muungwana aliyekulia nchini DRC. Anazungumza Kiswahili chenye lafudhi kama ya vijana na wanamuziki wa kikongo tunaoishi nao jijini Dar es Salaam.

Mmoja wa wahudumu katika hoteli niliyofikia ni kijana aliyezaliwa na kukulia nchini Uganda. Anapozungumza Kiingereza, unasikia kabisa lafudhi ya Kiganda kwenye matamshi yake. Ukienda kwenye hoteli kubwa na sehemu za mkusanyiko, utakutana na vijana wa Kinyarwanda waliokulia sehemu mbalimbali duniani.

Jambo moja la kuvutia ni kwamba wengi wao wanaipenda Tanzania. Wanapenda mchele kutoka Tanzania. Wanapenda wazungumza Kiswahili kutoka Tanzania. Kuna siku, kijana mmoja aliomba kujiunga katika meza niliyokuwa na Watanzania wenzangu ili apate tu fursa ya kusikiliza Watanzania wakizungumza Kiswahili chao!

Kwenye kijiji kimoja huko Shangasha, nilimwona mama mmoja akiwa amevalia fulana yenye picha ya Rais Jakaya Kikwete huku akiendelea na shughuli zake. Pengine alipewa tu fulana hiyo lakini kama angekuwa na chuki yoyote dhidi ya kiongozi huyo, basi asingeivaa.

Mambo hayo yanayofanyika kwa wananchi wa kawaida ni tofauti na unapoanza kufuatilia magazeti na vyombo vingine vya habari vya taifa hilo. Hapo unapata picha tofauti kabisa.

Picha inayojengwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari vya Rwanda (na baadhi vya nchini) inatoa taswira kuwa vita i mbioni kutokea wakati wowote kuanzia sasa.

Kwa vile nilipata bahati ya kuwa Rwanda kipindi hiki, itakuwa vema iwapo nitatoa mifano ya ripoti za upotoshaji kwenye vyombo vya habari kulinganisha na hali halisi iliyopo.

Chukulia mfano wa gazeti la The Kigali Sun la Jumatatu, Agosti 13 mwaka huu. Kwenye ukurasa wake wa mbele, gazeti hilo linalotoka kila wiki, lilikuwa na habari kuu iliyokuwa na kichwa cha habari “ Kikwete aliweka eneo la Maziwa Makuu Kwenye Taharuki (Tanzania’s Kikwete Puts Region on Tension).

Habari hiyo ilimfananisha Rais Kikwete na mmoja wa wachochezi wakuu wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, Leone Mugesera ambaye mwaka 1992, alichochea Wahutu kuwaua wenzao Watutsi aliowaita “mende tu” na kuwataka wawaue na kuitupa miili yao katika mto Nyabarongo.

Mto huo ni tawi la Mto Nile na utupwaji huo wa miili hiyo katika mto huo ulikuwa na lengo la kuhakikisha maiti wanarejea katika nchi ya Ethiopia ambako Mugesera alidai ndiyo nchi asilia ya Watutsi.

Kwa nini Kikwete alilinganishwa na Mugesera? Kwa sababu aliagiza wahamiaji haramu waondolewe nchini wakati alipokuwa wilayani Karagwe katika Mkoa wa Kagera hivi karibuni.

Niliposoma makala ile, nilijiuliza maswali mengi. Mojawapo ni iwapo Kikwete anastahili kulinganishwa na wauaji wa kimbari kwa sababu ya kutoa matamshi yake mkoani Kagera. Marekani na nchi nyingi za Ulaya hivi sasa zinazidi kuweka sera kali kuhusu wahamiaji haramu lakini hawafananishwi na wauaji.

Iweje kauli ya Kikwete ifananishwe na akina Mugesera? Takwimu zilizopo zinaonyesha kwamba Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa iliyoathirika sana na suala hilo la wahamiaji haramu na kwa kawaida, ilitarajiwa rais azungumze suala hilo mkoani humo. Kulikuwa na mantiki ya kufanya hivyo.

Hata hivyo, The Kigali Sun waliona inafaa kumpa Kikwete majina yote mabaya. Ndani zaidi, habari hiyo ilidai vyombo vya habari vya Tanzania vinamuunga mkono Kikwete katika ajenda hiyo na hivyo; likimnukuu Profesa Paul Rutayisire akidai “vyombo vya habari vya Tanzania vinaripoti mambo ambayo ni sawa na kugawa mapanga kwa wananchi.”

Gazeti hilo pia lilidai kwamba kutokana na kauli za uchokozi za Tanzania na Kikwete dhidi ya Malawi, tayari Serikali ya Malawi imeliweka Jeshi lake katika kile kinachoitwa “Hali ya Hatari.”

Likinukuu chanzo makini kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), gazeti hilo lilidai kwamba kutokana na hali ya hatari iliyopo sasa, kikosi cha vifaru cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF), tayari limesogeza vifaru vyake Kaskazini mwa taifa hilo kujiandaa na tishio lolote.

“Watanzania wanafahamika kwamba ni watu wanaopenda sana taifa lao. Na wanapokuwa katika tishio la aina yoyote ile wanakuwa wamoja. Kuna mtu mmoja aliye madarakani ana lengo la kuharibu hiba (legacy) yote iliyoachwa na Mwalimu Nyerere,” gazeti hilo lilinukuu chanzo chake cha kuaminika kutoka ndani ya CHADEMA. Hata hivyo, mtu yeyote makini atakayesoma gazeti hilo atabaini kwamba kwa kiasi kikubwa habari hiyo ilikuwa ya kutungwa tu. Mosi, hakuna kiongozi yeyote wa CHADEMA aliyenukuliwa kwenye habari hiyo jambo ambalo linatia wasiwasi.

Pia, si rahisi kwa ofisa wa kawaida wa CHADEMA kuwa na taarifa kuhusu Kikosi cha Vifaru cha UPDF kuanza kusogea kuelekea Kaskazini mwa taifa hilo kabla hata vyombo vya habari vya Uganda vyenyewe havijaripoti kuhusu hilo.

Uongo mwingine unaeleza namna vyombo vya habari vya Tanzania vinavyoendesha kampeni kali dhidi ya watu wenye asili ya Rwanda ambapo gazeti hilo limedai kumnukuu mmoja wa wanadiplomasia aliyepo nchini. Kimsingi, hakuna chombo chochote cha habari hapa nchini ambacho kinafahamika kwa chuki zake za wazi dhidi ya Rwanda.

Juni mwaka huu, gazeti hilo hilo la Kigali Sun lilimchora katuni Rais Kikwete akidai kwamba anaomba muda wa miaka miwili baada ya kumaliza kipindi chake ili amalizie ajenda yake binafsi.

Gazeti hilo la Jumatatu, Juni 17 mwaka huu, lilihoji ni ajenda ipi ambayo Kikwete anataka kuimalizia. Miongoni mwa mambo ambayo gazeti hilo lilihisi anataka kuyafanya ni; mosi kuua Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kuchimba madini pamoja na waasi wa kundi la FDLR na kuishambulia Rwanda.

Chanzo cha habari hiyo pia hakikujulikana. Lakini, je, huo ndiyo ukweli kuhusu Kikwete na Rwanda? Kinachofahamika nchini ni kwamba Kikwete hajawahi kuzungumza hadharani au kwenye vikao vya ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu nia ya kutaka kuongeza muda wake wa kukaa madarakani. Isipokuwa yaliwahi kutokea madai kwamba kuna watu wanataka kupendekeza hivyo ili Kikwete abaki madarakani hadi Katiba mpya ianze.

Akiwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Tanzania mwaka 1997, Kikwete alikuwa sehemu ya ujumbe wa Tanzania uliofanikisha kuundwa upya kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Haiingii akilini kwamba mwanasiasa huyo huyo anaweza leo kuchochea kuvunjwa kwa jumuiya hiyo hiyo.

Suala la kuishambulia Rwanda pia haliingii akilini kwa sababu Kikwete anafahamika kama mmoja wa wasuluhishi wa migogoro. Kwa mwanasiasa ambaye amehusika katika upatanishi wa migogoro katika nchi za Burundi, Madagascar, Comorro, Zimbabwe na DRC, haileti mantiki kuona kwamba sasa anataka vita.

Hivi karibuni tu, Kikwete alitoa msimamo kwamba nchi hizi mbili ni marafiki wa muda mrefu na Tanzania itafanya kila jitihada kuhakikisha kwamba uhusiano huo mwema unaendelea kwa faida ya Tanzania.

Kwa upande mwingine, gazeti linalotolewa mara mbili kwa mwezi kwa lugha ya Kinyarwanda la Rushyashya, la Agosti 9 hadi 23 mwaka huu, lilikuwa na kichwa cha habari, Rais wa Tanzania atangaza mgogoro na Rwanda (Perezida wa Tanzania yatangaje igisa nk’intambara k’u Rwanda).

Gazeti hilo lilikuwa limetandaza picha za kijeshi tupu katika ukurasa wake wa mbele. Kwenye habari hiyo, kulikuwa na picha kubwa za wakuu wa majeshi ya nchi hizo, Jenerali Davis Mwamunyange wa Tanzania na Jenerali Patrick Nyamvumba wa Rwanda.

Kulikuwapo pia na picha mbili za askari katika ukurasa huo huo wa kwanza. Kwanza ni ya Waziri wa Ulinzi wa Rwanda, Jenerali James Kabarebe na askari wa kundi la waasi wa FDLR linaloundwa na waliokuwa askari wa Jeshi la Rwanda wakati wa utawala wa Rais Juvenal Habyarimana na wafuasi wao wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Ripoti za namna hii haziishii Rwanda peke yake. Mwezi uliopita, gazeti moja la hapa nchini (kwa sababu za wazi kabisa sitalitaja jina), liliripoti pia kwamba majeshi ya Tanzania yanayolinda amani nchini DRC yalitoa kichapo kikali kwa waasi wa kundi la M23.

Habari hiyo inadai mapigano hayo yalifanyika kwa takribani saa mbili mfululizo. Kutokana na uhusiano unayotajwa kuwako baina ya M23 na Serikali ya Rwanda, habari hiyo ilikuwa na lengo la kuonyesha namna majeshi ya Tanzania yalivyo tayari kwa vita dhidi ya Rwanda.

Nilipokuwa Rwanda nilikwenda hadi mpakani mwa Rwanda na DRC. Uchunguzi nilioufanya kwa kuzungumza na vyanzo mbalimbali, ulionyesha kwamba hakujawahi kuwapo mapigano “yoyote ” baina ya majeshi ya Tanzania na kikundi cha M23 tangu majeshi yetu yalipokwenda huko.

Ni wazi lengo la gazeti hilo lilikuwa ni ile tu kuchochea dhana ya vita kukaribia baina ya Rwanda na Tanzania wakati kitu chenyewe hakipo.

Katika baadhi ya mitandao ya kijamii hapa nchini, kumekuwapo pia na watu wanaohusisha mauaji ya askari wa Tanzania kule Darfur, Sudan na majeshi ya Rwanda. Kwamba waasi walisaidiwa na majeshi ya Rwanda kufanya walichofanya.

Hadi sasa, hakuna chanzo chochote kilichowahi kuthibitisha tuhuma hizi nzito. Kinachoonekana katika ripoti za namna hii ni kile kile, kujenga dhana ya kunukia kwa vita ambayo haipo kwa wananchi.

Lengo la kampeni ni Kikwete?

Ukisoma kwa makini, kwa ujumla wake, mlengwa mkuu wa propaganda za vyombo vya habari vya Rwanda ni Rais Kikwete.

Katika magazeti mengi niliyosoma, na nimesoma mengi kwa kipindi kifupi, hakuna vyombo vinavyowatuhumu wananchi wa Tanzania au serikali yao kwa kutaka kuvuruga amani. Mlengwa mkuu ni Kikwete.

Kwa mfano, kwenye Kigali Sun, dhana ya Kikwete kutaka kudai kipindi cha tatu cha madaraka yake inapewa nguvu kuliko kawaida. Ni kama vile tayari rais huyo wa Tanzania ametangaza azma yake hiyo hadharani.

Katika toleo lake hilo la wiki iliyopita, gazeti hili limedai kwamba limezungumza na chanzo cha kuaminika ndani ya CCM na kimewaeleza kwamba Kikwete anapiga kampeni za kuomba kipindi cha tatu cha utawala wake baada ya kumaliza vipindi viwili vya kikatiba.

Rushyashya linakwenda mbele zaidi kwa kueleza kuwa Kikwete anataka kuondoa utaratibu ambao umedumu katika desturi za siasa za Tanzania kwa kubatilisha hiba iliyoachwa na marais Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi ambao walitawala kwa miaka 10 kila mmoja.

“Chanzo cha kuaminika” cha gazeti hilo ndani ya CHADEMA kilidai kwamba mgogoro wa sasa unatengenezwa na Kikwete kwa vile anataka Watanzania waone kwamba ni yeye pekee anayeweza kuongoza nchi katika kipindi cha misukosuko kama sasa.

Watanzania wamegeuzwa na Kikwete kuwa wahanga wa uroho wa madaraka. Kusini mwa Tanzania, kuna mgogoro na Malawi. Magharibi kuna mgogoro na Rwanda na tunasikia Uganda nao wanasogeza majeshi yao mpakani. Lakini, unataraji nini unapokuwa na mtu aliye Ikulu na anataka kutawala kinyume cha Katiba? Watanzania wanatiwa uoga na Kikwete ili wampe nafasi aendelee kutawala,” kinaeleza chanzo hicho cha The Kigali Sun kutoka ndani ya CHADEMA.

Kuhusu mlinganisho wa Kikwete na Mugesera, gazeti hilo lilimnukuu mtaalamu wa masuala ya Mawasiliano ya Umma, Raymond Gatare, akidai kwamba matamshi yao yanafanana kwa vile wote “ wanachochea vurugu, ubaguzi na utenganifu baina ya jamii, jambo linaloweza kusababisha mauaji ya kimbari wakati wowote.”

Pia, inajengwa taswira ya Kikwete kuwa mtu katili na asiye na huruma. Kwenye vyombo hivyo, Mtanzania mmoja mwenye asili ya Rwanda, Eugene Byagatonda, alinukuliwa akisema; “Wakati jua linapozama, unakwenda kulala wakati ukiwa na hofu. Hofu ambayo imetokana na rais wako mwenyewe. Rais ambaye kura yako ilimweka madarakani.

“Anawezaje (Kikwete)- bila aibu wala huruma, kutangaza kwamba sisi Wanyarwanda ni wezi na kupe tusiokuwa na hadhi ya kuishi Tanzania? Kwa Kikwete, Wanyarwanda wote waliopo Tanzania ni wahamiaji haramu. Matokeo yake, sasa watoto wetu walio shule kila siku wanaulizwa na wenzao wataondoka lini,” amenukuliwa mwananchi huyo anayedaiwa kuishi Bukoba, Kagera.

Hadi sasa, kuna maelfu ya Wanyarwanda wanaoishi nchini kama wanafunzi, wafanyakazi na kada nyingine za maisha lakini hawafukuzwi. Kauli ya Byagatonda inamaanisha Wanyarwanda wote hawatakiwi nchini Tanzania, ambao kimsingi ni uongo.

Katika siku yangu ya mwisho nchini Rwanda, nilihudhuria mkutano wa waandishi wa habari wa Waziri wa Mambo ya Nje ya Rwanda, Louise Mushikiwabo, ambaye alizungumzia kuhusu masuala ya Wanyarwanda kufukuzwa Tanzania.

Alitumia nafasi hiyo kuwahakikishia Watanzania waishio Rwanda kwamba wanakaribishwa na wanatakiwa kuishi bila ya hofu yoyote. Nilitaraji Serikali ya Tanzania nayo ingetoa kauli kama hiyo kwa Wanyarwanda waishio nchini kihalali. Sote tunajua kwamba raia wa Rwanda hawafukuzwi Tanzania. Wanaofukuzwa wanatakiwa kuwa wahamiaji haramu (ambayo ni halali kisheria duniani kote). Pengine, labda kuna watu wanafurahia mazungumzo haya ya kunukia kwa vita.

Wananchi wa Tanzania na Rwanda wala hawana habari na vita. Lakini, kama vyombo vya habari vitaamua kutengeneza ajenda ya vita na ikazama vichwani mwa watu, watakaoumia ni wananchi wa kawaida ambao kimsingi hawataki kabisa.

Pengine huu ni wakati wa vyombo vya habari na serikali kuanza sasa kuelekeza uandishi wa kuchochea wananchi kufanya biashara na kushirikiana badala ya propaganda ya vita.

Chanzo:- Raia Mwema

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/%E2%80%98vita%E2%80%99-ya-vyombo-vya-habari-isiyokuwepo#sthash.IRBmzgOK.dpuf

No comments:

 
 
Blogger Templates