Muswada wa Umwagiliaji wapita kwa mbinde
WAZIRI wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Chistopher Chiza, jana alisulubiwa na wabunge na kulazimishwa kuufanyia marekebisho Muswada wa Sheria ya Uanzishwaji wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wa mwaka 2013. Mbali na Waziri na Naibu wake Adam Malima, wabunge pia walimbana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema ambaye muda wote alionekana kuwa na kibarua cha maswali kutoka kwa wabunge hao.
Viongozi hao wa Serikali walikumbwa na kibano hicho jana bungeni baada ya Bunge kukaa kama kamati ya Bunge kupitia kifungu kwa kifungu muswada huo.
Kutokana na hali hiyo Jaji Werema alikiri mbele ya Bunge kuwa sasa nafasi ya Bunge inaonekana baada ya wabunge wengi bila kujali itikadi zao, kujadili suala hilo.
Hofu kubwa kwa wabunge wengi ilikuwa ni kutaka muswada huo kuwa na kifungu kinachompa mamlaka Mtanzania mwenye ardhi kupewa kipaumbele kwa kumiliki hisa kwenye miradi ya umwagiliaji kuliko jambo hilo kubaki kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi.
Wabunge hao walionyesha wasiwasi wao kwa kusema muswada umeandaliwa kwa lengo kuwanufaisha wawekezaji wageni na kuwaondoa wananchi kwenye ardhi yao.
Baadhi ya wabunge walioongoza mashambulio hayo kwa kuukataa muswada huo hadi urekebishwe, ni mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jafo (CCM) na Halima Mdee-Kawe (Chadema),
Walisema vipengele vingi kwenye muswada huo vilitoa fursa kwa serikali, viongozi na watendaji kuchukua ardhi ya wananchi bila ridhaa ya mikutano ya kijiji.
Kipengele kilichokuwa kikilalamikiwa ni kile kinachoipa mamlaka ya tume ya umwagiliaji kutenga maeneo ya umwagiliaji na kuwalipa fidia wenye ardhi husika ili ikabidhiwe kwa mwekezaji.
Chanzo :- Mtanzania
No comments:
Post a Comment