MWAKA jana nilikuwa nahitajika kuwasilisha andiko la utafiti ili niweze kuhitimu nilichokuwa nakisoma. Nilichagua kufanya utafiti kuhusu uwezekano wa kuanzisha sarafu moja kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kimsingi sarafu moja ni moja ya mambo ambayo yapo katika protokali iliyoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na inatakiwa kutekelezwa kama moja ya hatua za kufikia shirikisho la Afrika Mashariki.
Wanachama wanaweza kusema sarafu moja ianze kufanya kazi sasa hivi, nilichokuwa nakiangalia katika utafiti huo ni ikiwa nchi za jumuiya hii zimetimiza vigezo muhimu ili sarafu hiyo ikianzishwa manufaa ya sarafu moja yaweze kuonekana.
Hitimisho la utafiti wangu huo ulikuwa ni kwamba nchi wanachama hawajatimiza vigezo muhimu vya kiuchumi na kisiasa ili sarafu moja ikianzishwa iwe na manufaa kwa wanachama na pia uchumi uende bila mikwaruzo.
Vinginevyo tunaweza kuona yanayotokea huko Uturuki yakitokea kwa baadhi ya nchi wanachama. Nilitakiwa kutetea andiko langu hilo mbele ya jopo. Profesa mmoja kutoka Zimbabwe alitofautiana sana na mimi katika hitimisho langu.
Kwa maoni yake alidhani kwamba nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zingeweza kuingia katika sarafu ya pamoja hata siku hiyo nilipokuwa mbele ya jopo.
Hata hivyo aliniambia maadam nilikuwa nimewasilisha takwimu na vielelezo vya kutetea hitimisho langu kwamba nchi za jumuiya hiyo hazipo tayari kwa sarafu ya pamoja, ataridhia andiko hilo kama andiko la kitaaluma tu na si uhalisia.
Leo hii natamani nikutane na yule profesa aliyekuwa akiongoza jopo lile nimuulize kama msimamo wake ni ule ule. Kwa kitambo sasa tumekuwa katika uhusiano usio mzuri na Rwanda, moja ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Wengi wanaona hali hii ya ‘kununiana’ baina ya nchi zetu hizi mbili kuwa ni jambo la kitoto. Wapo wanaoliona ni jambo dogo na wapo wanaoliona ni jambo kubwa kiasi kwamba mitaani nilishasikia watu wakianza kujadili nguvu ya jeshi letu na lile la Rwanda, kwa maana kwamba wapo watu ambao wanaona uwezekano wa vita baina ya nchi hizi mbili.
Binafsi sioni kama kuna sababu ya vita wala dalili yoyote ya vita kwa maana vita vya kutumia silaha na kushambuliana. Si tu hatuombi vita isitokee lakini sioni cha kunifanya nifikirie vita inaweza kuzuka. Kwangu hali hii ambayo naweza kuiita ni tete inanionesha tu kwamba kufikia Shirikisho la Afrika Mashariki si jambo rahisi na hata uwezekano wa kubomoka kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki upo.
Kwa kuzingatia juhudi kubwa zilizofanywa za kujaribu kuiunda upya jumuiya hii na gharama nyingi za fedha na muda hatuwezi kusema mzozo baina ya nchi hizi mbili ni jambo dogo au la kupuuza tu. Ni jambo kubwa na serikali ilipaswa kukubaliana na Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba kuna ulazima wa kunusuru hali ya hewa isichafuke kwani dalili za jumuiya hii kushindwa kusonga mbele ipo wazi sasa.
Moja ya vigezo nilivyovifanyia kazi katika andiko langu ni pamoja na tofauti za kimasilahi kwa nchi husika. Leo hii wanajeshi wa Tanzania wako Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwadhibiti waasi wa M23. Lakini wachambuzi hili suala wanaliona kama mgongano wa kimasilahi si kati ya Tanzania na waasi wa M23 bali ukinzani wa masilahi baina ya taifa letu na Rwanda.
Na hili linatokana na ukweli au propaganda zinazoelezwa na hasa Marekani na washirika wake kwamba Rwanda ina mkono wake katika uasi unaoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Huu mzozo haujaelezwa bayana na serikali zote mbili. Na hapa ndipo tunapokuwa na matatizo kama yule profesa wangu ambaye hataki kuona ukweli bali kuamini moyoni huku amefumba macho.
Tunahitaji kusuluhishwa na Rwanda. Haitusaidii kusema kwamba hatujagombana nao. Sote tunajua ukweli kwamba kuna mzozo na sasa sina hakika kama ni mwendelezo wa mzozo huo au ni jambo linalojitegemea kuona baadhi ya nchi wanachama wakifanya vikao vya peke yao ili kujadili maendeleo yao ya kiuchumi.
Katika mazingira haya ndipo ninapotaka kumhoji yule profesa wa Zimbabwe, hivi sarafu moja itawezekana? Si tu sarafu moja, Jumuiya itaweza kusonga mbele wakati tunafahamu kwamba juma lililopita wakuu wa Rwanda, Uganda na Kenya walikutana huko Kenya na wakajadili masuala ya uchukuzi ambayo yatatugharimu kwa maana ya kupunguza mizigo itakayopitia bandari zetu?
Wakati hao wanakutana, wakuu wa Tanzania na Burundi hawakushiriki. Walikataa kushiriki au hawakukaribishwa? Hili nalo tunaliona dogo hata kama tunazungumzia hoja ya Rwanda na Uganda kutokutumia bandari zetu? Tuache kutoa majibu mepesi kwa maswali magumu.
Nimeona pia katika mtandao taarifa nyingine mbili ambazo kama ni kweli basi inabidi sisi kama taifa tutafakari kuhusu mustakabali wetu katika jumuiya ya Afrika Mashariki na kuangalia kwa kina tunainusuru vipi kwa ajili ya masilahi yetu kama taifa kiuchumi lakini pia kisiasa.
Taarifa ya kwanza niliyoiona takriban majuma mawili yaliyopita ilikuwa ni ile kwamba nchi za Rwanda, Uganda na Kenya wanapanga kwamba raia wao wasafiri baina ya nchi hizo bila pasi ya kusafiria na badala yake watatumia tu vitambulisho. Kama Jumuiya ya Afrika Mashariki ina nchi tano wanachama, iwezekane vipi nchi tatu zifanye mipango hiyo huku nyingine mbili zikitengwa? Inawezekana tunaunda Jumuiya ndani ya Jumuiya?
Na taarifa ya pili niliyoiona siku ya Ijumaa kwenye mitandao ya kijamii ni kwamba nchi hizo tatu zinazoonekana kuwa na ukaribu wa pekee zinafanya mpango wa kutumia viza moja kwa watalii kwa nchi zote tatu ili kurahisisha na kuongeza utalii. Kama hii nayo ni kweli lazima tujue kwamba sasa ni wakati wa kuita beleshi kwa jina lake na si kuita kijiko kikubwa.
Sote tunafahamu kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Lakini kama katika umoja huo kuna wamoja wanaowatenga wengine, hatuna budi kuwa macho zaidi. Tuhakikishe hatuko kwenye ndoa ya mkeka. Tufikirie na kuchukua hatua ya kurekebisha makosa kabla ya kwenda hatua yoyote mbele kwenye Jumuiya hii.
Wapo watu wanaotoa hoja kwamba Tanzania tuna rasilimali nyingi kuliko nchi yoyote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki hivyo iwe iwavyo watu hao wanatuhitaji kuliko tunavyowahitaji.
Sikubaliani na hoja hii kwa misingi kwamba kuwa na rasilimali kwa yenyewe si sababu ya mtu kukuhitaji.
Hoja ni namna gani tunazitumia hizo rasilimali. Mipingo inapatikana kwa wingi katika mikoa ya kusini mwa Tanzania, yaani Mtwara na Lindi, lakini China ndiyo nchi inayoongoza kwa kuuza samani zilizotengenezwa na magogo kutoka kusini mwa Tanzania katika soko la Amerika!
Dhahabu inayochimbwa Tanzania ni nyingi lakini uliza Tanzania tumepata shilingi ngapi kutokana na dhahabu hiyo. Tanzanite inachimbwa Tanzania pekee lakini kuna wakati Kenya iliripotiwa kuuza tanzanite nyingi kuliko Tanzania. Vitunguu vinalimwa kwa wingi Tanzania lakini kuna taarifa za vitunguu hivyo kuvushwa Kenya kisha kusafirishwa nchi za nje kama vile vimetoka Kenya.
Mlima Kilimanjaro upo Tanzania lakini kuna binadamu duniani wameaminishwa upo Kenya na wapo watalii wengi wanaupanda mlima huo wakianzia safari yao Kenya na kumalizia Kenya kabla ya kurudi makwao.
Uganda nao wanauza kahawa nyingi kwenye soko la dunia lakini sehemu kubwa ya kahawa hiyo ya Uganda ni kahawa iliyozalishwa Kagera kisha ikauzwa kwa magendo Uganda.
Mifano ni mingi ila nimalizie tena na hii changamoto mpya ambapo wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki wameanza kusigana wakitaka vikao visifanyikie Arusha pekee ambako ndiko makao makuu ya jumuiya yetu, bali vizunguke pia katika nchi nyingine.
Unapotafakari haya bado unaweza kusema mzozo hata kama unaonekana wa kitoto kati ya Rwanda na Tanzania ni jambo dogo? Tusipoziba ufa tutajenga ukuta.
Chanzo :- Tanzania daima
No comments:
Post a Comment