Social Icons

Friday, 6 September 2013

MBOWE AZIDI KULIBANA JESHI LA POLISI.....



KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kwa mara nyingine ameitaka Serikali kuunda tume huru ya kimahakama, kufanya uchunguzi wa mauaji yote ya raia yaliyofanywa na askari wa Jeshi la Polisi. Akiuliza swali bungeni jana, Mbowe alitaka kujua sababu za Serikali kupata kigugumizi kuunda tume hiyo huku vifo vya raia vinavyofanywa na polisi kuendelea kushamiri.

“Mnataka hadi siku watoto wenu, ndugu zenu au viongozi wa Serikali wauawe ndipo mtaona umuhimu wa kuchukua hatua?” Alihoji Mbowe.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Silima alikiri kutokea kwa matukio hayo, huku akielekeza lawama kwa wananchi.

“Ni kweli matukio mengi ya mauaji ya raia yanatokea katika vurugu zinazosababishwa na raia wenyewe. Matukio yanapotokea tunayachunguza na tunawafukuza kazi askari wanaohusika na kuwafikisha mahakamani,” alisema.

Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), Silima alisema aliyekuwa mwanafunzi wa Sekondari ya Iyunga, Michael Sikupya alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi 53 waliokamatwa na polisi Novemba 26 mwaka 2000, kutokana na kufanya vurugu.

Alisema alipokuwa polisi katika mahojiano hali yake ilibadilika na kuanza kuumwa na kukimbizwa hospitali na kulazwa, ambapo Desemba 3 mwaka 2000 alifariki.

“Uchunguzi wa awali ulifanyika na jopo la madaktari, hakuna mtu aliyechukuliwa hatua kisheria, upelelezi uliendelea na shauri lilifunguliwa mahakamani.

“Aprili 4 mwaka 2011, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, ilitoa maamuzi ya shauri hilo kwa kuundwa tume maalumu ya uchunguzi ikishirikisha vyombo vitano vya upelelezi na tayari imekamilisha upelelezi wake.

“Kwa sasa taarifa ya uchunguzi huo inaandaliwa na mara itakapokamilika itatolewa, hatua stahiki kwa mujibu wa mapendekezo ya tume hiyo zitachukuliwa kwa wale wote watakaobainika kuhusika na mauaji hayo.

Katika swali lake, Mbilinyi alitaka kujua hatua zilizochukuliwa kutokana na mauaji hayo na kuitaka Serikali kuilipa fidia familia ya marehemu huyo.

Chanzo :- Mtanzania

No comments:

 
 
Blogger Templates