Awali, DPP alikata rufani akipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachia huru Zombe na wenzake katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva taksi mmoja wa Manzese, Dar es Salaam.
DPP, aliwasilisha maombi hayo mahakamani hapo, baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali rufani yake dhidi ya Zombe na wenzake wanane baada ya kubainika kuwapo na kasoro katika taarifa ya kusudio la kukata rufani.
Mei 8, mwaka huu, Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali rufani hiyo, baada ya kubaini kasoro hizo za kisheria ambapo katika hati ya taarifa ya kusudio la kukata rufani, waliandika wanapinga hukumu iliyotolewa na Jaji Salum Massati wa Mahakama ya Rufani badala ya aliyekuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu wakati huo.
Richard Rweyongeza, Majura Magafu na Dennis Msafiri, mawakili wanaowakilisha upande wa kina Zombe, walipinga maombi hayo kwa madai ya kwamba kasoro iliyojitokeza katika taarifa ya kusudio hilo ilitokana na uzembe na si tatizo la uchapaji.
Jopo hilo la mawakili liliyapinga maombi hayo, baada ya mawakili wa Jamhuri, Edward Kakolaki na Timoth Vitalis kueleza sababu za kuishawishi Mahakama Kuu iwaruhusu kuwasilisha rufani nje ya muda.
Miongoni mwa sababu zao, ni kwamba kulikuwa na makosa yaliyofanyika katika taarifa hiyo likiwemo la kumuandika Jaji Massati kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kutokana na sababu za uchapaji.
Katika rufani wanayotarajia kupeleka Mahakama ya Rufani, kuna masuala ya msingi ya kisheria ambayo wanataka yajibiwe na kutolewa uamuzi katika Mahakama hiyo.
Upande wa mawakili wa wajibu maombi, ulipinga maombi hayo na kuiomba mahakama iyatupilie mbali kwa sababu makosa yaliyofanyika katika taarifa ya kusudio si ya uchapaji bali ya uzembe.
Rweyongeza alidai upande wa Jamhuri hauonyeshi kilichotokea hadi makosa yakatokea na hakukuwa na sababu yoyote isipokuwa uzembe na hakuna maelezo ya aliyefanya kosa hilo.
Chanzo:- Mwananchi
No comments:
Post a Comment