MSAFIRISHAJI MBABAISHAJI ASABABISHA SHEHENA YA MALAWI ILIYOKUWA IMEZUILIWA KITUO CHA MIZANI CHA KIBAHA MKOANI PWANI KULIPIA SHILINGI MILIONI 350....
Udanganyifu uliofanywa na msafirishaji aliyepewa zabuni ya kusafirisha transformer zinazotakiwa kupelekwa nchini Malawi kupitia bandari ya Dar es Salaam umesababisha shehena hiyo kutakiwa kulipiwa takriban Shilingi milioni 350. Malipo hayo ni tozo, pamoja na gharama za ziada baada ya kubainika kuwepo kwa udanganyifu katika nyaraka za kuruhusu usafirishwaji wa mizigo hiyo.
Malori matatu yaliyobeba mizigo inayosafirishwa kuelekea nchini Malawi yamekwama katika kituo cha mizani ya kupimia magari cha Kibaha mkoani Pwani kuanzia mwezi Aprili mwaka huu. Kukwama kwa mizigo hiyo kumeelezewa kusababishwa na taarifa zisizo sahihi ambazo msafirishaji wa mizigo hiyo aliwasilisha wakati akiomba kibali cha kusafirisha shehena hiyo kwa barabara.
Hali hiyo imesababisha nchi ya Malawi kutuma ujumbe maalum ulioongozwa na Waziri wa Usafirishaji wa chi hiyo Mhe. Sidik Mia, uliwasili juzi jijini Dar es Salaam na kukutana na Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa lengo la kupata suluhu ya mizigo hiyo. Ujumbe huo kutoka Malawi ulijumuisha pia Waziri wa Nishati Mhe. Ibrahim Matola, Katibu Mkuu wa Wizara ya Usafirishaji Bw. Moffat Chitimbe na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishaji Dr. Winford Masanjala.
Pamoja na kushukuru kuwepo kwa ushirikiano mzuri katika sekta ya ujenzi, ujumbe huo hata hivyo ulielezea kusikitishwa na udanganyifu unaoelezewa kufanywa na msafirishaji aliyetajwa kuwa ni Kampuni ya MO & GS kutoka Uganda, ambaye amesababisha ucheleweshaji pamoja na tozo ambazo zitalazimika kulipwa ili mizigo hiyo iweze kuendelea na safari. Kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani Na. 30 ya mwaka 1973 kiasi cha Shs. 350 milioni kitalazimika kulipwa ili kukamilisha taratibu zote za kuruhusu mizigo hiyo kuendelea na safari.
Kati ya malipo hayo kiasi cha Shs. 140,730,150/= ambazo tayari zimelipwa ni gharama ya uharibifu wa barabara kuanzia Dar es Salaam hadi Kibaha. Magari hayo hata hivyo baadaye yaligundulika kuwa na uzito uliozidi kiwango kilichoombwa na hivyo kutakiwa kulipa faini kwa kosa hilo, kiasi cha Shilingi 9,900,00/= (US $ 6,000) kimelipwa kwa magari matatu. Aidha, kutokana na magari hayo kuegeshwa katika kituo hicho cha mizani Kibaha, yatalazimika kulipia kiasi cha Shilingi 2,376,000/= (US $ 1,440 kwa siku) kwa magari yote matatu kwa siku 24. Ili kuweza kuendelea na safari magari hayo yatahitaji kupata kibali maalum ambacho hutolewa baada ya kulipia gharama ya uharibifu kwenye barabara kwa uzito unaozidi tani 56. Hivyo kwa magari hayo matatu ili yaweze kusafiri hadi mpakani mwa nchi yetu na Malawi, yatalazimika kulipiwa kiasi cha Shilingi 183,169,800/= (US $ 111,012).
Mnamo mwezi Aprili mwaka huu wa 2013 magari makubwa matatu yalikamatwa katika Kituo cha Mizani cha Kibaha yakiwa yamezidi uzito kwa kiwango kikubwa. Gari lenye usajili namba UAS958 na tela namba UAS0119V lilipimwa na kukutwa likiwa na tani 91.55, gari jingine ni lenye usajili namba UAP702Z likivuta tela namba UAL788X lilipopimwa lilikutwa na uzito wa tani 93.65 na gari la tatu likiwa na usajili namba UAR 352X na tela namba UAS023V lilikuwa na tani 82.8. Viwango hivi ni zaidi ya uzito unaoruhusiwa ambao hauzidi tani 56.
Mbali na uzito huo, bado upana wa mizigo hiyo ni mkubwa kuliko viwango vilivyoainishwa katika Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973. Kwa mazingira hayo pamoja na gharama zilizoainishwa hapo juu, bado msafirishaji atahitajika kukodi magari mawili pamoja na askari wa kusindikiza mizigo hiyo hadi mpakani mwa nchi yetu na Malawi.
No comments:
Post a Comment