Social Icons

Saturday, 7 September 2013

WABUNGE WA UPINZANI TZ WASUSIA BUNGE TENA......




*Muswada wa marekebisho ya Katiba wapitishwa...

WABUNGE wa Kambi ya Upinzani, kwa mara nyingine jana walitoka ndani ya ukumbi wa Bunge, ikiwa ni mwendelezo wa malalamiko yao dhidi ya uongozi wa Bunge na mipango ya Serikali. Hatua hiyo inalenga kuendeleza msimamo wao wa kutounga mkono Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, ambao wanadai umejaa makosa mengi.

Hata hivyo licha ya wabunge wa upinzani kutokuwapo bungeni, mjadala huo uliendelea na baadaye muswada huo ulipitishwa huku Serikali ikifanya marekebisho machache.

Sakata hilo lilianza siku ya Jumatano, ambapo wabunge wa kambi hiyo walitoka ndani ya ukumbi wa Bunge, wakidai kuwa muswada huo ulikuwa umeyaweka pembeni maoni ya Wazanzibari.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walisimama kuomba mwongozo wakitaka kuahirishwa kujadiliwa kwa muswada huo, hadi hapo Zanzibar itakaposhirikishwa, lakini mwongozo huo ulipuuzwa.

Hata hivyo, sekeseke hilo liliendelea juzi baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuagiza kutolewa ndani Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye alisimama kutaka ufafanuzi juu ya suala hilo, hatua iliyozua vurugu na ngumi kuibuka.

Kwa siku ya jana wabunge hao walitoka baada ya kipindi cha maswali na majibu, huku wakipinga msimamo wa Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama, ambaye aligoma kupokea hoja za wabunge hao.

Wabunge watatu wa upinzani walibaki katika mjadala huo, ambao ni Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Clara Mwatuka (CUF) na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP).

Mara baada ya kipindi hicho, baadhi ya wabunge hao walitaka mwongozo, lakini Mhagama aliwazima na kuamuru taarifa za Serikali ziendelee kujadiliwa, hatua iliyowachefua wabunge wa kambi hiyo na hivyo kuamua kutoka ndani ya ukumbi.

Wabunge waliosimama kuomba mwongozo wa Spika ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).

Wengine waliosimama ni Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mohamed Mnyaa (CUF) na Mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji (CUF). Kwa upande wa CCM waliosimama ni Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangwalah na Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM).

Baada ya kusimama kwa wabunge hao, Mhagama aliamuru majina ya wabunge hao yaandikwe na baada ya kusikilizwa kwa hoja za Serikali ndipo atawapa fursa ya kutoa taarifa zao kwa mujibu wa kanuni za Bunge.

Hali hiyo ambayo ilionekana kutowapendeza wabunge wa kambi hiyo hasa wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, waliamua kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge huku mjadala kuhusu muswada huo ukiendelea.

Chikawe arusha vijembe

Akihitimisha mjadala huo kwa kujibu hoja zilizotolewa na wabunge, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, alirusha vijembe kwa wabunge wa upinzani na kusema kwamba hawana nia njema na mchakato huo wa Katiba.

Alisema pamoja na Rais Jakaya Kikwete, kutangaza mabadiliko ya uundwaji wa Katiba Mpya, wapinzani wamekuwa wanafiki kwa kuwa na kauli ambazo zinakinzana na mahitaji ya Watanzania walio wengi.

“Ninachotaka kusema hapa kuna unafiki kwa wapinzani, kwani wakati mchakato huu unatangazwa, kila mtu alikuwa akifurahia na hata kusifu ujasiri wa Rais Kikwete ila leo amegeuka mbaya.

“Hili hapana na hatuko tayari kuona mchakato huu unataka kuvurugwa na baadhi ya watu, eti tu kwa maslahi yao kisiasa na katika kulithibitisha hili Februari 9, mwaka 2012, Tundu Lissu alimsifu rais kupitia Bunge hili.

“… leo hii amebadilika na hata kuja na hoja ambazo hazina mashiko kwa Watanzania kwa kudai kuwa eti Zanzibar haijashirikishwa katika mchakato,” alisema Waziri Chikawe.

Alisema katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya wadau mbalimbali, taasisi 675 zilitoa maoni yao ya upatikanaji wa rasimu ya Katiba Mpya vikiwemo vyama vya upinzani.

Kutokana na mjadala huo kuwa mzito, wabunge wa CCM walifanya marekebisho huku Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile (CCM) pamoja na Suleman Jafo, ambao walitaka Bunge Maalumu la Katiba lisifungwe kwa kuwa zaidi ya hoja 70 hazijamalizika kwenye Bunge hilo.

Balozi Seif avunja ukimya

Katika hali isiyotarajiwa, Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, jana alilazimika kusimama bungeni ili kutoa ufafanuzi kuhusu kutoshirikishwa kwa Zanzibar katika mchakato huo.

Hatua hiyo ya kuinuka kwa kiongozi huyo wa Serikali ya Zanzibar, ilitokana na mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM), aliyetaka kiti kimpe fursa kiongozi huyo ili aweze kutoa ufafanuzi kuhusu madai yaliyotolewa na Kambi ya upinzani kuhusu sakata hilo.

Kutokana na taarifa hiyo, Mhagama alisema kuwa pamoja na kutoa kanuni za Bunge hazimtambui Balozi Seif kama Makamu wa Pili kwa uwepo wake ndani ya Bunge.

“Ninaomba ieleweke kuwa uwepo wa Balozi Seif humu ndani si kutokana na nafasi yake ya umakamu wa pili wa rais, ila yeye ni Mbunge wa Kitope na kutokana na hali hiyo, basi ninakupa dakika mbili kuhusu hilo kama unapenda,” alisema Mhagama.

Balozi Seif alipopewa nafasi hiyo, kwanza alisimama na kusema kuwa hana la kusema kisha baada ya muda akatoa ufafanuzi na kusema kuwa Zanzibar ilishirikishwa katika mchakato huo.

Balozi Seif alisema yeye mwenyewe ndiye alitia saini barua kwenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu mchakato huo wa Sheria ya Katiba.

“Baada ya Rais wa Zanzibar, mie ndiye mtendaji na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na katika hili ninapenda kuwaambia kuwa msisikilize maneno yanayokuja kwa njia za panya humu ndani,” alisema Balozi Seif.

Chanzo:- Mtanzania

No comments:

 
 
Blogger Templates