Wiki iliyopita ulifanyika mkutano Mjini Mombasa na kuhudhuriwa na marais, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda, Pierre Nkurunzinza wa Burundi na Salva Kiir wa Sudan Kusini, lakini Rais Kikwete hakuhusishwa.
Tangu Rais Jakaya Kikwete alipotoa ushauri kwa nchi ya Rwanda kukaa na waasi wa FDLR ili wamalize migogoro yao, uhusiano baina ya Tanzania na Rwanda umekuwa shakani.
Mwaka 1994, wanajeshi wa Kihutu na wanamgambo waliua watu 800,000 nchini Rwanda wengi wao wakiwa Watutsi.
Kwa sasa, Rwanda inatawaliwa na Serikali ya Watutsi chini ya Rais Paul Kagame, huku makundi ya kijeshi ya Kihutu yakifuatilia kwa mbali. Moja ya makundi hayo ni FDLR.
Uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda kwa sasa unaonekana kulegalega kutokana na kitendo chake kupeleka majeshi yake kuungana na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa (UN) vilivyoko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika Jimbo la Goma.
Chanzo cha Uhasama
Uhasama huo unatokana na Kundi la M23 linaloundwa na wapiganaji wa Kitutsi likiaminika kusaidiwa na Rwanda na linapambana na majeshi ya Serikali ya DR Congo. Hata hivyo, Rwanda inapinga kuisaidia M23.
Kumekuwa na malumbano kupitia vyombo vya habari vya nchi hizo mbili huku kila upande ukirusha vijembe vya kumponda mwenzake.
Mbali na vijembe, hivi karibuni Rwanda imejitoa na kuanza kuacha kutumia Bandari ya Dar es Salaam kuingizia mizigo yake, badala yake sasa imejielekeza Mombasa nchini Kenya.
Hali hiyo inaonyesha kuiathiri Tanzania hata katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo katika mikutano ya hivi karibuni ya wakuu wa nchi hizo, Rais Kikwete hakushiriki.
Mkutano huo uliofanyika wiki iliyopita mjini Mombasa na kuhudhuriwa na marais, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda, Pierre Nkurunzinza wa Burundi na Salva Kiir wa Sudan Kusini walialikwa na kutuma wajumbe wao, lakini bila kumhusisha Rais Kikwete ni moja ya dalili ya Tanzania kutengwa au kuenguliwa.
Baada ya mkutano huo, marais hao wamezindua eneo jipya la bandari ambalo litasaidia kuimarisha huduma ya kupakia na kupakua mizigo.
Chanzo:- Mwananchi
No comments:
Post a Comment