Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe leo imefanya kikao cha pamoja na Maafisa Watendaji wa Kata zote za Halmashauri hiyo. Lengo la kikao lilikuwa ni hoja tatu, moja: Majukumu ya Watendaji wa Kata, Pili: Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big resurt now). Tatu: Mikakati ya Kuongeza mapato ya Halmashauri.
Akifungua kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Mhe. Alfred Mwakasangula aliwataka maafisa watendaji kuwa huru katika kutoa maoni yao bila woga na watalindwa na mwenyekiti kwa kila watakacho kisema ndani ya kikao hicho.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Mhe. Alfred Mwakasangula akifungua kikao
cha pamoja kati ya Kamati ya Fedha , Utawala na Mipango na Watendaji wa Kata.
Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Ndugu Cheyo, akitoa maelekezo ya wajibu na majukumu ya watendaji wa Kata ikiwa ni pamoja na kusimamia sheria za Halmashauri katika kata zao.
Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Ndugu Daniel Mwakitalu akitoa maelezo kwa wajumbe wa kikao kuhusu mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Resurt Now)
Maafisa Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kutoka kushoto. Ndugu, Lauden Nnala wa Kata ya Ikuti, Ndugu, Japhet Mbwillah na Ndugu, Zephania Charles Mwakatumbula wakipitia nyaraka za hoja zilizojadiliwa katika kikao cha pamoja na Kamati ya Fedha Utawala na Mipango.
Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe wakiwa ndani ya kikao.
Wajumbe wa kikao wakiwa ndani ya kikao cha pamoja kati ya Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango na Watendaji wa Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe.
Wakichangia katika hoja ya uongezaji wa mapato ya halmashauri baadhi ya watendaji wa kata hawakukubaliana na viwango walivyopangiwa wazabuni kulipa kwa mwezi, kwani ni viwango ambavyo vilikuwa vinatozwa kabla ya halmashauri haijapandisha viwango vya ushuru.
Wakitoa mfano walisema, Mzabuni wa kukusanya ushuru wa ndizi amepangiwa kulipa halmashauri Shilingi Milioni 24 kwa mwezi, fedha ambayo ilikuwa inapatikana kabla ya kupanda kwa ushuru wa ndizi kutoka Shilingi 100/- kwa mkungu mmoja na kuwa Shilingi 200/- kwa mkungu kwa sasa. Hivyo walitaka mzabuni alipe angalau Shilingi milioni 40 kwa mwezi.
Pia walitoa mfano, Makusanyo ya ushuru wa viazi aliopewa mzabuni wa Shilingi Milioni 42 kwa mwezi, ni fedha ambayo ilikuwa inapatikana kabla ya kupanda kwa ushuru wa viazi kutoka Shilingi 500/- kwa gunia na kuwa Shilingi 1000/- ya sasa, hivyo mzabuni alitakiwa angalau alipe kwa Halmashauri Shilingi Milioni 70 kwa mwezi.
Pia watendaji wa kata waliomba kuwa na mawasiliano na vikao vya mara kwa mara na uongozi wa halmashauri ya Wilaya, ili kuondoa sintofahamu zinazojitokeza kati yao na uongozi wa Halmashauri,
Kwani Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa unategemea sana mahusiano mazuri kati yao na watendaji wa halmashauri pamoja na Madiwani.
Na Basahama blog.
No comments:
Post a Comment