RWANDA na Uganda hazikutaka Tanzania itume majeshi yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwenye jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika (AU), Raia Mwema limeambiwa.
Vyanzo vya kuaminika vya gazeti hili kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, vimeeleza kwamba nchi hizo zilituma hadi wawakilishi hapa nchini kwa ajili ya kuiomba serikali isipeleke majeshi huko.
“Rwanda na Uganda hazikutaka tupeleke majeshi DRC. Walituma wawakilishi wao hapa kutuomba tusipeleke majeshi kule lakini sisi tukashikilia msimamo wetu kwamba ni lazima twende. AU imetuomba hivyo na tutatuma majeshi kwa maslahi ya bara letu la Afrika.
“Hawakuwa na sababu nzito ya kutuzuia tusiende. Ni wazi kuna mambo ambayo wao wanayafanya kule Congo na hawataki dunia iyafahamu. Sisi, japo hatukuwa huko (DRC) tunayajua kwa vile tuna mkono mrefu wa intelijensia,” kilisema chanzo hicho cha habari hizi kwa masharti ya kutotajwa jina kwa sababu ya unyeti wa suala lenyewe.
Raia Mwema linafahamu kwamba serikali imefanya mazungumzo na ubalozi wa Rwanda hapa nchini lengo likiwa kujaribu kuweka msimamo wake kwenye suala la amani nchi za Maziwa Makuu.
“Tumewaambia Rwanda kwamba kusemasema kwao hakusaidii kitu. Ni afadhali tu wangekaa kimya. Sisi tulizungumza kwenye vikao rasmi na wao kama wana hoja wazilete mezani.
“Wanatumia vyombo vya habari. Wanatumia baadhi ya wanaojiita waathirika wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Wanaongea na wanajeshi. Wanazungumza huko na huko. Hiyo haitasaidia.
“Ndiyo maana umesikia juzi Waafrika wanaoishi Brusels (mji mkuu wa Ubelgiji) waliandamana kupinga kauli ya Kagame (Rais Paul Kagame wa Rwanda) dhidi ya Rais Jakaya Kikwete. Wananchi wanajua na Jumuiya ya Kimataifa inafahamu kwamba alichosema Kikwete ndilo suluhisho la kudumu la matatizo ya Rwanda,” kilisema chanzo cha gazeti hili kutoka Ikulu ya Tanzania.
Juhudi za Raia Mwema kuzungumza na ubalozi wa Rwanda kuhusu suala hili hazikufanikiwa baada ya mwandishi kutakiwa kuacha maswali ambayo hayakujibiwa hadi tunakwenda mitamboni.
Zimekuwapo taarifa mbalimbali katika vyombo vya habari vya nje ya Tanzania kwamba Rwanda na Uganda hazitaki Tanzania ishiriki katika Jeshi hilo la Umoja wa Mataifa la Kulinda Amani DR Congo, linalojumuisha pia majeshi ya Afrika Kusini na Malawi, kwa madai kwamba uwepo wake utachochea zaidi machafuko kuliko kuleta amani.
Kundi la waasi la M23 ambalo ndilo linaloleta shida mashariki mwa DRC katika mji wa Goma, tayari limetoa taarifa ya kutaka majeshi hayo ya kulinda amani yasiende huko. Kuna taarifa kwamba waasi wa M23 wanaungwa mkono na serikali ya Rwanda.
Mwezi uliopita, baadhi ya asasi za kiraia (NGO’s) zinazofanya kazi mashariki mwa DRC ziliandika barua Umoja wa Mataifa (UN) zikiomba majeshi hayo ya kulinda amani yasiende kwa vile “yataharibu zaidi hali badala ya kurekebisha.”
Taarifa hizi zinaibuka katika wakati ambapo serikali na vyombo vya habari vya Rwanda vimekuwa vikiendesha propaganda ya kuilamu Tanzania na Rais Jakaya Kikwete kwa kushauri nchi hiyo izungumze na waasi wa kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR).
Wiki iliyopita Rais Kagame alisema Rwanda haiko tayari kuzungumza na waasi hao wa FDLR na kwamba wote wanaoshauri mazungumzo na kundi hilo hawafahamu historia ya Rwanda.
Suala hilo la Tanzania kupeleka vikosi DRC ndilo ambalo linadaiwa kwa kiasi kikubwa kwenye vita hii ya maneno baina ya nchi hizi mbili kwenye suala la kuzungumza na waasi.
Rais Kikwete anadaiwa kutoa ushauri wa kutaka Rwanda, Uganda na DRC zizungumze na waasi katika nchi zao kwenye Mkutano wa Viongozi wa Bara la Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia mwezi uliopita.
Raia Mwema limeambiwa na mmoja wa wana diplomasia waandamizi wa Tanzania katika Umoja wa Afrika (AU) kwamba wakati Kikwete alipotoa hoja hiyo ya kuzungumza na waasi, hakuna kiongozi yeyote wa nchi hizo aliyemkatalia.
“Sisi katika diplomasia tunashangaa sana. Tunadhani kuna kitu ambacho wenzetu (Rwanda) hawataki kukisema hadharani. Kama ushauri wa Kikwete ulikuwa mbaya, kwanini hawakusema kitu pale mkutanoni?
“Na Rais (Kikwete) hakuzungumza kwa siri au kwa lengo la kuwasengenya kwa watu. Alizungumza mbele ya macho yao na katika kikao halali kabisa. Hakuzungumza maneno hayo na wafanyakazi wa Tanzania au wanajeshi wetu.
“Kama kungekuwa na nia njema, Rwanda wangetoa maoni yao palepale mkutanoni. Lakini kukaa kimya katika sehemu ambayo watu wanatakiwa kuzungumza ya moyoni kwao na kutoa majibu wakiwa ‘jikoni kwao’ ni ishara mbaya,”” alisema mwanadiplomasia huyo.
Baadhi ya wanadiplomasia wa Tanzania wanaamini kwamba nchi yao itaibuka mshindi katika vita hii ya maneno kwa sababu historia inaonyesha imetumika katika utatuzi wa migogoro mingi.
“Tanzania ikizungumza inasikilizwa katika jumuiya ya kimataifa. Tumesuluhisha mgogoro wa Burundi na kwingineko. Tukizungumza tunafanya hivyo from the point of experience (kutokana na uzoefu). Wenzetu hawajawahi kusuluhisha mgogoro wowote na hivyo hivyo hawana uzoefu wa mambo haya,” kilisema chanzo hicho.
Vuta Nikuvute ya Tanzania na Rwanda
Mambo matatu yaliyotokea katika katika kipindi cha miezi minane iliyopita, yamebadilisha taswira ya mahusiano ya Tanzania na Rwanda.
Mosi, ni hatua ya Tanzania kukubali kupeleka majeshi ya kulinda amani DRC katika maeneo ambayo baadhi ya ripoti za UN yamewahi kuituhumu Rwanda kwamba inahusika kuhujumu maliasili za taifa hilo tajiri.
Duru za kijeshi na intelijensia zimeliambia gazeti hili kwamba kabla ya Tanzania kukubali kupeleka majeshi DRC ilifanya utafiti wa hali halisi kwenye maeneo yenye matatizo na kuzungumza na baadhi ya wahusika wakuu wa vikundi vya waasi; baadhi yao wakiwa wasiopatana na serikali ya Rwanda.
Mmoja wa waliopewa mwaliko wa kuzungumza na majeshi ya Tanzania katika suala hilo ni Jenerali Stanislas Nzeyimana ambaye pia hutumia jina la Bigaruka Izabayo, mmoja wa makamanda wa juu wa jeshi la FDLR ambaye serikali ya Rwanda ilimkamata mara tu baada ya kutoka Tanzania.
“Rwanda haikufurahi kwamba Tanzania ilizungumza na mtu inayemtafuta kwa udi na uvumba. Lakini JWTZ (Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania) isingeweza kupeleka jeshi DRC pasipo kuwa na taarifa on the ground (kwenye eneo la tukio). Sisi tunakwenda pale kama neutral force (jeshi lisilo na upande) na hatuwezi kuchaguliwa mtu wa kuzungumza naye,” kilisema chanzo cha gazeti hili kutoka JWTZ.
Pili, kuna maoni kwamba Rais Kikwete ameanza kupata umaarufu kimataifa kumzidi Kagame ambaye miaka michache iliyopita alikuwa akitajwa kama mfano bora wa kuigwa miongoni mwa kizazi kipya cha viongozi wa bara la Afrika.
Kuna taarifa pia kuwa huku misaada ya mataifa tajiri kama Marekani ikiongezeka, ziara za viongozi wa mataifa makubwa duniani nazo zimekuwa zikiongezeka nchini Tanzania kwenye miaka ya karibuni na wakati huohuo mambo ya aina hiyo yakiwa hayaelekezwi sana Rwanda.
Tatu, kuna madai kwamba Rwanda haikufurahishwa na hatua ya UN na AU kumbadili aliyekuwa Mkuu wa Vikosi vya Kulinda Amani vya UN na AU Darfur, Jenerali Patrick Nyamvumba, na nafasi yake kupewa Mtanzania, Luteni Jenerali Paul Ignace Mella.
Tanzania na Rwanda DRC
Tayari kundi la M23 limetoa vitisho kwamba JWTZ lijiandae kwa maafa kutokana na kupeleka majeshi yake nchini DRC kwenye eneo ambalo wao ndiyo waasi wenye nguvu.
Hata hivyo, JWTZ kupitia msemaji wake, Kanali Kapambala Mgawe, limewataka waasi hao kuacha vitisho maana haviwatishi askari wa Kitanzania.
Katika siku za karibuni, waasi hao wametoa taarifa za vitendo visivyo vya kiungwana vinavyofanywa na askari wa kulinda amani na vimehusishwa na vikosi vya kulinda amani.
Akizungumza na Raia Mwema, Mgawe alisema wanajeshi wa Tanzania hawawezi kushiriki katika vitendo vyovyote visivyo vya kibinadamu kwa vile wamefunzwa vema na wakaiva kwenye mafunzo hayo.
“Tumekwenda DRC na flying colours (sifa nzuri) kutoka kwenye mataifa mengine. Tumekwenda Liberia kulinda amani. Tumekwenda Lebanon. Tuko Darfur na kote huko utakachosikia ni sifa nzuri tu. Taarifa hizo za ubakaji ni propaganda tu.
Chanzo :- Raia Mwema
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/rwanda-haiitaki-tanzania-dr-kongo#sthash.1gwDgqqg.dpuf
No comments:
Post a Comment