Dk. Benjamin (Ben) Rugangazi, Balozi wa Rwanda nchini Tanzania na Shelisheli amezungumza na gazeti hili la Raia Mwema kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo nchi hizi mbili. Yafuatayo ni mahojiano kamili baina mwandishi wa gazeti hili, Ezekiel Kamwaga na mwanadiplomasia huyo ambaye kitaaluma ni daktari wa mifugo.
Raia Mwema: Mheshimiwa Balozi, matamshi ya viongozi wa juu wa nchi hizi mbili katika siku za karibuni yanaonyesha kwamba hali ya uhusiano baina ya Rwanda na Tanzania si nzuri kwa wakati huu. Je, wewe unalionaje hili?
Dk. Rugangazi: Nashukuru kwa swali lako. Kusema ukweli, hali ya uhusiano baina ya nchi zetu ni nzuri na ndiyo maana leo tunazungumza hapa bila matatizo yoyote.
Hata hivyo, niseme kwamba baadhi ya vyombo vya habari vinalikuza suala hili. Nitoe mfano wa makala moja iliyoandikwa na mwandishi aliyejiita Abdul Majid kwenye gazeti lenu ambayo ilizungumza mambo mengi yasiyo mazuri.
Makala ile kwa kweli haikutenda haki kwa Rwanda, kwa Rais Paul Kagame na kwa uhusiano mwema wa Tanzania na nchi yangu. Mambo mengi yalikuwa ya upotoshaji.
Vyombo vya habari vina wajibu wa kuchochea uhusiano mwema na sisi kama taifa ni wahanga wa uhasama uliochochewa na vyombo vya habari. Hata mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994, yalichochewa sana na vyombo vya habari.
Raia Mwema: Makala unayoizungumzia iligusia suala la madai ya muda mrefu kuwa mauaji ya aliyekuwa Rais wa Rwanda, Juvenal Habyarimana, yalifanywa na kundi la RPF ambalo sasa ndilo linaloongoza serikali ya nchi hiyo. Unazungumziaje kuhusu madai haya?
Dk. Rugangazi: Huo ndiyo upotoshaji ninaouzungumzia. Kuna tume ilifanya uchunguzi na ambayo taarifa yake ilitolewa na ipo hadharani kwamba bomu lililolipua ndege ya marehemu Habyarimana lilitokea katika maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Kigali.
Kwa wakati huo, uwanja huo ulikuwa ukishikiliwa na majeshi ya serikali pamoja na yale ya Ufaransa. RPF haikuwepo kwenye eneo hilo na ndiyo maana ripoti ikasema RPF haihusiki.
Huo ni upotoshaji unaofanywa kwa makusudi kabisa.
Raia Mwema: Chanzo cha tofauti ya sasa baina ya nchi yako na Tanzania kinaelezwa kuwa ni hatua ya Rais Jakaya Kikwete kushauri mzungumze na kundi la waasi la FDLR. Kuna ugumu gani kwenu kuzungumza na kundi hilo?
Dk. Rugangazi: Kwanza niseme mapema kwamba suala la sisi kufanya mazungumzo na waasi wa FDLR halipo kwenye ajenda yetu. FDLR ni kundi la waasi ambalo dhamira yake ni kufanya mauaji mengine ya kimbari dhidi ya wananchi wa Rwanda.
Tofauti iliyopo baina ya serikali na FDLR si ya kisiasa wala si ya ugomvi wa kawaida. Ni tofauti kwamba kuna watu hawataki wenzao waishi hapa duniani na wengine wanataka kuishi na kuendeleza taifa lao.
Tatizo la sisi na FDLR nalilinganisha na tatizo la Wayahudi na Manazi wa Ujerumani. Huwezi leo ukasema Wayahudi wakae na kupatana na manazi maana hawana matatizo ya kuyajadili wakayamaliza.
Wanazi wanataka Wayahudi wafutike kwenye uso wa dunia. Hiyo ndiyo sera waliyokuzwa nayo. FDLR ni wauaji na huo ndiyo mtazamo wetu.
Hata hivyo, tumesema kwamba wale wapiganaji wa FDLR ambao wako tayari kukiri makosa yao na kutubu, tunaweza kuwasamehe na kujenga upya nchi yetu. Tumefanya hivyo tayari na ndiyo maana waasi zaidi ya 51,000 wamerejea Rwanda wakitokea katika kundi la FDLR katika kipindi cha kati ya mwaka 1996 hadi sasa.
Baadhi yao wameingizwa katika Jeshi la Rwanda na hivi ninavyozungumza na wewe, Mkuu wa Magereza nchini Rwanda alikuwa askari wa zamani wa FDLR.
Wale ambao hatuwezi kuzungumza nao ni wale ambao wana mashitaka ya kujibu kutokana na makosa waliyoyafanya kwenye mauaji ya mwaka 1994.
Wale ambao bado wanataka kufanya mauaji ya kimbari na hawataki kukiri makosa yao hatuwezi kuzungumza nao.
Raia Mwema: Kama mmeweza kuchukua watu 51,000 na wengine mkawapa madaraka makubwa, mnashindwaje kuzungumza na hawa wengine?
Dk. Rugangazi: Kuna watu waliua na wameshitakiwa kwa makosa waliyoyafanya na hawa ambao wana mashitaka ya kujibu ni lazima sheria ichukue mkondo wake.
Kuna watu ambao hadi Umoja wa Mataifa (UN) umetangaza kwamba wanatafutwa na kama unavyofahamu, serikali ya Marekani imetoa hadi zawadi kwa mtu atakayefanikisha kukamatwa kwao.
Kama wanadhani wanaonewa, wajitokeze na waende kujibu mashitaka yao kwenye Mahakama ya Kimataifa kama wenzao waliopelekwa ICTR ya Arusha. Kama wakishitakiwa huko na wakakutwa hawana hatia na wakaonyesha kuwa hawana nia wala mwelekeo wa kutaka kuangamiza Wanyarwanda hapo tunaweza kuwa na mawazo mengine.
Lakini katika hali ya sasa, hakuna cha kuzungumza nao.
Genocide is not an ordinary crime. It is not fighting to defeat. It is killing to decimate (Mauaji ya kimbari si uhalifu wa kawaida. Si kupigana kwa lengo la kushinda vita. Ni mauaji yenye lengo la kuhilikisha (kuwafuta kabisa kwenye uso wa dunia) wapinzani wako.
Hii ndiyo sababu tunasema waliohusika na mauaji ya kimbari ni watu ambao kwanza wanatakiwa kukumbana na mkono wa sheria kabla ya mambo mengine.
Raia Mwema: Kuna taarifa kwamba serikali yenu haikufurahishwa na hatua ya Tanzania kupeleka askari wake kwenye kikosi cha kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Kuna ukweli kwenye hili?
Dk. Rugangazi: Si kweli. Rwanda inaunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU) kwenye kuleta amani nchini DRC. Hivyo hatuna tatizo na uwepo wa Tanzania.
Raia Mwema: Nina taarifa kwamba serikali yenu ilituma ujumbe kwa serikali ya Tanzania kuomba isitishe mpango wake wa kupeleka askari Rwanda. Vyanzo vyangu vinaniambia kwamba serikali ya Tanzania ilikataa. Unazungumziaje suala hili?
Dk. Rugangazi: Mimi ndiyo nasikia kutoka kwako hizo taarifa. Kama mimi balozi ndiyo nasikia kwako suala hili kwa mara ya kwanza, maana yake ni kwamba suala lenyewe halipo.
Maana kama ujumbe umetumwa na serikali ya Rwanda kuja Tanzania, mimi nitakuwa mtu wa kwanza kujua. Huo ndiyo ukweli. Serikali ya Rwanda haikutuma watu kuja Tanzania.
Raia Mwema: Kuna madai kwamba hamkutaka Tanzania iende huko kwa sababu mna uhusiano wa karibu na kundi la M23 ambalo ndilo hasa linaloleta matatizo Mashariki mwa Congo. Je, ni kweli kwamba mnalisaidia kundi hilo?
Dk. Rugangazi: Huo ni uzushi mwingine wa NGO’s zilizoko DRC. Taarifa hizi zinaandikwa sana kwenye vyombo vya habari vya Ulaya na Marekani. Jibu langu kwa swali lako ni moja tu; Nenda mwenyewe Mashariki mwa DRC na ukahakikishe. Hatutoi msaada wowote kwa M23.
Kuna mambo yao wenyewe na serikali ya DRC ambayo yanatakiwa yamalizwe lakini Rwanda haitoi msaada wowote. Uhusiano pekee uliopo ni kwamba lugha kubwa inayozungumzwa katika maeneo hayo ni Kinyarwanda.
Raia Mwema: Rais Kagame analaumiwa kwamba siku hizi ni dikteta na hafuati misingi ya utawala bora. Una maoni gani kuhusu hilo.
Dk. Rugangazi: Nani anayemlaumu?
Raia Mwema: Hata Jenerali Kayumba Nyamwasa anadai hivyo.
Dk. Rugangazi: Namfahamu Nyamwasa kwamba ni mtu ambaye alishindwa kutimiza majukumu yake. Ameanza kulalamika mara tu baada ya kuvuliwa nyadhifa zake. Kama angekuwa mkweli, angeyasema anayoyasema wakati akiwa na vyeo vyake vyote jeshini.
Niseme tu kwa ufupi kwamba rekodi ya Rais Kagame iko wazi. Rwanda imetoka katika kipindi kigumu sana lakini imepata maendeleo ya haraka ambayo yanapigiwa mfano.
Hata hivyo sisemi kwamba eti Rwanda inajihisi inaonewa wivu kutokana na maendeleo iliyoyapata kama ambavyo ile makala ya kwenye gazeti lenu ilivyodai.
Rwanda bado ni nchi masikini na Rais Kagame halali usingizi kwa ajili ya hilo. Ukweli wa wazi kabisa ni kwamba Rwanda na Tanzania bado ni nchi masikini na zinahitaji sana kushirikiana ili kujiongezea maendeleo.
Raia Mwema: Sawa Nyamwasa hakutimiza majukumu, lakini madai kama hayo yamewahi kutolewa pia na wanasiasa wengine wakubwa tu wa Rwanda. Watu kama Seth Sendashonga miaka ya nyuma na Theogene Rudasingwa. Wote hawa pia walikuwa na uchungu wa kunyimwa madaraka?
Dk. Rugangazi: Ok. Kwanza niseme kwamba siwezi kukaa hapa na kukupa majibu ya watu wote ambao wamewahi kupingana na Rais Kagame miaka ya karibuni au zamani.
Ninachokifahamu ni kwamba Rais Kagame ni mchapakazi na ana nia ya kuibadili Rwanda na Wanyarwanda ili wawe bora kuliko alivyowakuta. Kwenye hili, yuko tayari kuhatarisha mahusiano yake binafsi na watu kwa ajili ya faida ya taifa lake.
Raia Mwema: Wewe ni balozi na unazungumza na Rais Kagame wakati wowote na pia unazungumza na Rais Kikwete pale unapohitajika. Kuna madai kwamba viongozi hawa wawili hawana mahusiano mazuri. Unazungumziaje hili?
Dk. Rugangazi: Nisingependa kuzungumzia mahusiano binafsi ya viongozi wangu. Nawaheshimu sana na si kazi yangu kuhakikisha viongozi wana mahusiano mazuri au mabaya.
Kilicho cha muhimu kuliko vyote ni wananchi zaidi ya milioni 150 walioko ndani ya nchi hizi mbili. Kama wananchi hawa wakiwa na uhusiano mzuri, sote tutafaidika.
Nadhani hilo ndilo ambalo nimetumwa kulifanya hapa. Kuhakikisha Rwanda na Tanzania zinakuwa na uhusiano mzuri kiuchumi, kisiasa, kijamii na katika nyanja zote za muhimu.
Raia Mwema: Unakumbuka nini kwenye mauaji ya kimbari ya mwaka 1994? Kuna ndugu, jamaa au marafiki uliopoteza kwenye mauaji hayo?
Dk. Rugangazi: Ndiyo. Kimsingi, sidhani kama kuna Mnyarwanda ambaye hakupoteza ndugu, jamaa au marafiki wakati wa mauaji hayo. Ninachokumbuka zaidi ni kuona miili ya watu waliouawa kikatili ikiwa imezagaa barabarani.
Kuna wengine waliouawa walikuwa watoto wanaotambaa. Mtu anachukua panga na kumuua mtoto ambaye anatambaa kumfuata kuomba msaada.
Sasa unajiuliza huyu mtoto mchanga anayetambaa ana makosa gani ya kuuawa kikatili namna hii? Siku moja nilikuja kwenye shughuli za utoaji wa misaada ya kijamii hadi mpakani mwa Tanzania na Rwanda upande wa Kagera.
Kwenye mto Kagera nikaona maiti zinapita. Kuna maiti moja ikawa inapita kwenye mkondo wa maji unaozunguka. Maiti ikawa inazungushwa tu bila ya kwenda popote. Kwa kweli nililia sana siku ile.
Na niseme ukweli, tangu wakati huo, imani yangu kwa Mungu iliingia kwenye wakati mgumu sana. Nilijiuliza, hivi kweli kama yupo anaruhusu vipi watu wake wateseke namna hii? Maiti ile ina makosa gani. Watoto wale wachanga wana makosa gani?
Na unajua walikuwa wanajuaje kama huyu ni Mhutu au Mtutsi? Vitambulisho. Vitambulisho vilivyokuwepo vilikuwa vinaandikwa kama mtu ni wa kabila gani. Hivyo wauaji walikuwa wanasimamisha magari na kukagua vitambulisho. Wale waliokuwa wameandikwa Wahutu walikuwa wakiuawa hapohapo.
Chanzo :- Raia Mwema
No comments:
Post a Comment