- Wajumbe hao waliowahi kuwa kwenye Halmashauri Kuu ya NCCR Mageuzi, walitambulishwa jana na Mwenyekiti wa muda wa chama hicho, Wales Mayunga....
- Wanadai kuchoshwa na kile walichokielezea kuwa ni chama kuendesha kama taasisi ya mtu ...
Dar es Salaam. Waliokuwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi, Hashim Rungwe na Hassan Mmbwana wamekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) huku wakieleza kuchoshwa kuona NCCR-Mageuzi ikiongozwa kama taasisi ya mtu binafsi.
Pia wamesema NCCR-Mageuzi imegeuzwa kuwa Tawi la CCM kwa madai kwamba kila jambo analotaka kufanya au kusema anapewa masharti ya kutoisema CCM hata ikifanya mabaya.
Wajumbe hao waliowahi kuwa kwenye Halmashauri Kuu ya NCCR Mageuzi, walitambulishwa jana na Mwenyekiti wa muda wa chama hicho, Wales Mayunga. Rungwe aliwahi kugombea urais mwaka 2010 kupitia NCCR Mageuzi na Mmbwana alikuwa Kamishina wa NCCR Mageuzi wa Mkoa wa Tanga.
Akizungumza wakati wa kukabidhiwa kadi ya chama hicho, Rungwe alisema kilichomuondoa NCCR-Mageuzi ni kuchoshwa na hatua ya chama hicho kugeuzwa kuwa tTaasisi ya watu binafsi.
“Nimechoshwa na tabia za viongozi wa juu wa NCCR-Mageuzi, jambo lolote utakalotaka kufanya lazima upewe onyo kwamba usije ukaizungumzia CCM kuhusu jambo lolote ,” alisema Rungwe.
Alisema wakati anagombea urais mwaka 2010 kwenye mikutano yake ya kampeni alikuwa akielezwa wazi kwamba marufuku kuisema CCM kwa chochote jambo ambalo siyo demokrasia ya vyama vingi.
Rungwe alibainisha wazi kuwa uamuzi wa kujiunga na Chaumma umekuja baada ya kusoma Katiba ya chama hicho na kuridhika nayo, kwani inaeleza wazi mambo mbalimbali ya ungozi ndani ya chama ikiwa pamoja na kuwa na kikomo cha uongozi.
“Chama cha NCCR-Mageuzi katiba yake haionyeshi kwamba uongozi ndani ya chama unakikomo, jambo ambalo linafanya watu kugeuza chama kama taasisi yao binafsi ya kujinufaisha,” alisema.
Rungwe alisema katiba ya Chaumma imetaja mambo muhimu ikiwa ni pamoja na kuwa na kikomo cha uongozi.
Alisema mambo aliyoyafanya NCCR-ageuzi ni makubwa ikiwa ni pamoja na kutoa wabunge wanne kutoka Mkoa wa Kigoma.
Chanzo :- Mwananchi
No comments:
Post a Comment