Dar es Salaam. Sakata la Katibu Mkuu wa Yanga limechukua sura mpya baada ya juzi jioni kuibuka vurugu kubwa Makao Makuu ya klabu hiyo, Mtaa wa Twiga na Jangwani wakati kikao cha Kamati ya Utendaji ya Yanga kikiendelea.
Vurugu hizo zilizuka baada ya kuibuka makundi mawili ya vijana, moja likiunga mkono uamuzi wa viongozi kuajiri katibu kutoka Kenya, na lingine likipinga mpango huo.
Kutokana na hali hiyo, zilizuka ngumi miongoni mwa makundi hayo, huku wengine wakirushiana mawe ambapo askari wa kutuliza ghasia (FFU) walilazimika kuitwa kuja kuleta amani.
Akizungumza jana, Makamu Mwenyekiti wa Yanga Clement Sanga alisema, Patrick Naggi bado hajapewa mkataba, ila ni miongoni mwa wale walioomba ajira na bado mchakato unaendelea.
“Mwalusako bado ni katibu wa Yanga, taratibu za kumpata katibu mwingine mchakato unaendelea na yeye ni sehemu ya mchakato huo. Kuna nafasi pia ya Mkurugenzi wa Fedha na Ufundi,” alisema Sanga.
Kauli ya Sanga imekuja siku chache baada ya Baraza la Wazee wa Yanga kuitisha Mkutano na Waandishi wa Habari kupinga kuajiriwa kwa Naggi, kwa kuwa siyo mwanachama.
“Katiba ya Yanga haitambui Baraza la Wazee, inajieleza wazi, ila tunawaheshimu waliotoa ni maoni tu kama anavyotoa mtu mwingine. Utaratibu waliotumia sio sahihi, kama walikuwa na hoja wangefuata taratibu,” alisema.
“Dhamana ya kuajiri ni ya Kamati ya Utendaji na siyo mtu mwingine yoyote. Kama kamati ikipitisha Naggi, basi atakuwa Katibu Mkuu, kwa vile kuna wengine wamewahi kuajiriwa na hawakuwa wanachama wa Yanga,” alisema zaidi.
Chanzo:- Mwananchi.
No comments:
Post a Comment