Dar es Salaam. Nyota wa Yanga, Kelvin Yondan na Athuman Iddi ‘Chuji’ wameungana na wachezaji wenzao jana asubuhi kuanza mazoezi magumu huku Salum Telela na Abdallah Mguhi wakianza kufanya mepesi.
Daktari wa Yanga, Nassoro Matuzya aliliambia gazeti hili jana baada ya kumalizika kwa mazoezi Uwanja wa shule ya Sekondari, Loyola Mabibo jijini Dar es Salaam.
“Yondan na Chuji wako fiti kwa asilimia 100, ndio maana leo (jana) wamejiunga na wenzao kuanza kufanya mazoezi magumu.
Telela yeye ameanza mazoezi mepesi rasmi leo (jana) wakati Mguhi ana siku ya tatu sasa.” alisema Matuzya.
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts alisema amefurahishwa na kurejea kwa wachezaji hao na kusema ni dalili nzuri kwake kabla ya kukabiliana na Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Bara wikiendi ijayo.
“Nimefuraha kurejea kwao, nafikiri ni dalili nzuri za ushindi kwenye mchezo wetu dhidi ya Mbeya City. Nafikiri mchezo utakuwa mgumu na ushindani mkubwa.”
Alifafanua kuwa anaenda kucheza na timu ambayo haifahamu kwa maana hiyo itakuwa vigumu kwake kujua atumie aina gani ya mchezo kukabiliana na timu hiyo ngeni kwenye ligi.
Chanzo:- Mwananchi.
No comments:
Post a Comment