FEDHA yoyote duniani imepatikana kwa nguvu ya mbadilishano, ndiyo maana watu wanaotaka kuwa na fedha nyingi huwa hawaanzi na fedha bali wanaanza kujiuliza kwamba: “Nigundue nini nitakachobadilishana na watu wanipe fedha?”
Majibu ya swali hili ndiyo biashara inayoweza kuwa ya bidhaa, huduma au uzalishaji.
Hapa ndipo unakutana na wagunduzi wa teknolojia, bidhaa na wabunifu mbalimbali ambao msingi wao ulianza kwa kujiuliza swali hilo ili kuwa na fedha.
Watu wengi wamekuwa wakitajirika kwa kuangalia matatizo ya jamii, nchi na dunia kama vile teknolojia duni, magonjwa, kukosekana kwa huduma za jamii kama vile maji, afya na kutumia fursa hiyo kugundua suluhu ya matatizo wanayobadilishana na jamii inayowapa fedha.
Kinachotakiwa ni kutokuwa na mpaka wa mawazo kufikiri nje ya uzio ili uweze kufanikiwa kimaisha, fikiri tofauti ili ufanye mambo ya kitofauti na kuweza kufanikiwa kwa sababu ukifikiri kikawaida utafanya mambo ya kawaida na kuishi maisha ya kawaida.
Watu wengi waliofanikiwa hawafanyi mambo tofauti na wengine wanayoyafanya bali wanayafanya mambo hayo hayo ila kitofauti, hapa nazungumzia ubunifu na upekee.
“Mtu yeyote ambaye ni tajiri hapa duniani kihalali ni kwa sababu amejibu uhitaji mmojawapo wa watu wengi sana,” anaeleza Mwalimu Christopher Mwakasege, ambaye ni mtaalamu wa mambo ya uchumi katika kitabu chake cha Kanuni za kufuata ukitaka mapato yako yazidi matumizi, katika ukurasa wa 41.
Mfanyabiashara mmoja aliwahi kusema kuwa asilimia kubwa ya watu wanaoishi sasa hivi duniani wanawategemea watu waliokufa kwa maana ya teknolojia, mifumo mbalimbali waliyoianzisha, bidhaa walizogundua tunaendelea kuzitumia na watu wengi wanatumia kiasi kidogo cha uwezo wa akili walichopewa na Mungu.
Mfano hasa, watu walioajiriwa kwenye taasisi kama vile benki, viwandani na maofisini, watu wanatumia teknolojia na mifumo iliyoanzishwa na watu wengine ambao wengine tayari wamekwisha kutangulia mbele ya haki.
“Kama pesa yako haina kazi ni vigumu kuongezeka na ni vigumu kuwa na fedha nyingi, kwa sababu utakuwa unapata fedha na kuzitumia… huna namna ya kuzifanya fedha zako ziweze kuongezeke na kuwa nyingi, hivyo utakuwa unaishi maisha ya chini kiuchumi tofauti na wale wanaozifanyia kazi fedha zao zinazoongezeka, wanakuwa na maisha mazuri kiuchumi,” anasema Mtaalamu wa masuala ya ujasiriamali, Joseph Mayagila, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mafunzo katika Chuo cha Uandishi wa Habari na Utangazaji Arusha (AJTC).
Mayagila anasema wengine ambao ni waoga kufanya biashara wamekuwa wakinunua vitu vinavyoongezeka thamani kila siku kama ardhi ambayo baadaye wakiuza wanapata faida mara dufu, nayo ni njia ya kuhifadhi fedha na kuwekeza, ardhi ni benki nzuri.
Anasema fedha haziwezi kukufanya uwe tajiri bali unachokijua kuhusu fedha ndicho kinachokufanya kuwa tajiri au maskini, hapa anazungumzia nguvu ya mbadilishano iliyoko katika fedha, pia wazo la biashara linaweza kumfanya mtu akafanikiwa kiuchumi na kuwa tajiri.
Fedha haziwezi kukuletea furaha au huzuni, fedha zinakuletea uhuru wa kufanya mambo mbalimbali na uhuru huo ndio unaokuletea furaha au huzuni katika maisha.
Watu wengi wanaamni kuwa fedha ni kila kitu na inampa mtu furaha, jambo ambalo si kweli, japokuwa asilimia kubwa ya mahitaji ya binadamu yanahitaji fedha.
Unashauriwa na nani kuhusu fedha yako?
Mtu anayekushauri kuhusu pesa yako anatakiwa awe ni mtu anayekuzidi mawazo, akili, pesa na umri.
Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya fedha, ni muhimu kuchagua washauri kama unataka kusonga mbele na kupiga hatua kiuchumi ila usiwadharau watu wenye kifua kikubwa kiuchumi, ambao utaweza kujifunza kwao namna ya kukabiliana na changamoto unazokutana nazo.
Nguvu ya kutazama na ubunifu pia ni muhimu kwa mtu kutazama eneo alilopo na fursa za kiuchumi zinazopatikana katika eneo analoishi ili kufanya biashara na kupata fedha.
Pamoja na kuwa mbunifu, ni vema kuhakikisha kitu unachotaka kukianzisha hata kama kimeshaanzishwa na mtu mwingine ila unakifanya kwa ubunifu mkubwa na kukiboresha ili kuwavuta wateja wengi na kufanikiwa kiuchumi.
Mfano mfumo wa upakiaji (vibebeo).
“Yupo mtu mmoja alikwenda kununua asali dukani akaletewa asali mbili, moja kutoka Tanzania na nyingine ya Kenya, ile ya Tanzania ilikuwa nyingi katika chupa ya kilevi na ile ya Kenya ilikuwa kwenye kachupa kadogo kalikorembeshwa na kutiwa nakshi na inauzwa bei ghali, cha kushangaza mtu huyo akanunua ile ya Kenya na ni mtu wa kawaida, si kwamba ana fedha sana, nikagundua kuwa alivutiwa na kibebeo cha ile asali ya Kenya japo ilikuwa ni chache na ghali,” anasema Mayagila, Mkurugenzi wa Mafunzo katika Chuo cha Uandishi wa Habari na Utangazaji Arusha (AJTC).
Anasema wajasiriamali wengi wana tatizo la kuwa na mfumo mbaya wa upakiaji, hawana vibebeo vyenye ubora, vya uhakika na vinavyomvutia mteja kuweza kununua bidhaa zao.
Mkurugenzi wa Mafunzo katika Chuo cha Uandishi wa Habari na Utangazaji Arusha (AJTC), anasema ipo haja kwa serikali, watu binafsi na wadau wa viwanda kufikiria kutengeneza vibebeo ili bidhaa zetu ziweze kufanya vizuri katika soko la ndani na nje ya nchi.
Kutokana na hilo, ipo haja ya wafanyabiashara kuzisajili bidhaa zao katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili waweze kutambulika zaidi.
Mtaalamu mmoja wa masuala ya ujasiriamali anafafanua kuwa tajiri ni imani, ukijijengea imani ya kuwa tajiri unaweza kuwa tajiri, endapo utafanya kazi kwa bidii, kuwa na nidhamu ya fedha, kuweka akiba na kutimiza malengo uliyojiwekea.
Pia anashauri mtu mmoja mmoja kujijengea nidhamu ya kutimiza malengo yake ili aweze kufanikiwa kimaisha na kusema kwamba njia ya mafanikio imejaa changamoto nyingi, hivyo yakupasa uzishinde na si kuziogopa, kwa sababu changamoto ni sehemu ya maisha ambayo wakati mwingine ni kama jaribio au mtihani ambao ukifaulu unaingia katika hatua nyingine ya maisha ya mafanikio.
Chanzo:- Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment