WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amesema sheria ya tozo ya asilimia tano kwa wasafirishaji wanaozidisha mizigo na kusababisha uharibifu wa barabara hataibadilisha hadi itakapobadilishwa na Bunge.
Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na uongozi wa Kanda Maalumu ya Kipolisi Dar es Salaam, Dk. Magufuli alisema wasafirishaji hao wanapaswa kutii sheria za nchi na si kuzipinga kwa masilahi yao binafsi.
Alisema kama kulikuwa na msafirishaji mizigo ambaye alikuwa hajui sheria hiyo, basi ni wakati wa kujua kuwa ipo tozo ya asilimia tano kwa anayezidisha mzigo, si mpya, bali ilikuwapo tangu mwaka 1973.
“Nataka niwaambie kuwa sheria hazibadilishwi kwa barua, sheria zinabadilishwa na Bunge, sasa kama wanataka waliombe Bunge libadilishe, hata likisema uzito uwe tani 300, ikipitishwa tutaisimamia,” alisema.
Magufuli alisema tozo hiyo iliwahi kuondolewa wakati ule wa Wizara ya Miundombinu kutokana na malalamiko ya wasafirishaji kukwamishwa shughuli zao, ubovu wa miundombinu na matatizo ya vipimo vya mizani moja hadi nyingine.
Alisema baada ya kuanzishwa Wizara ya Ujenzi ambayo imefanikiwa kujenga barabara kwa gharama kubwa, kwa bahati mbaya imebaini kuwa kuna baadhi ya wasafirishaji wamekuwa wakishindwa kutii sheria inayowakataza kuzidisha mzigo zaidi ya tani 56 ambazo ndio uwezo wa barabara nchini.
Alitaja mifano ya viwango vya usafirishaji wa mizigo katika barabara za nchi za Uingereza kuwa ni tani 40 hadi 44, Marekani 36, Uholanzi 54, Ufaransa 40, Ujerumani 40, Bulgaria 40, Australia 40 na Urusi tani 38.
Dk. Magufuli alisema ukiangalia uzito wa nchi hizo bado wa Tanzania ni mkubwa, ambao haustahili kupigiwa kelele, hata hivyo kama kuna msafirishaji ambaye hajaridhishwa na sheria hiyo ni vema akaenda mahakamani kupinga.
“Sasa niwaombe wale wote wasiotaka kutii sheria za nchi, wajue kuwa sheria hiyo itawaandama na kama yupo anayetaka kugoma agome lakini ahakikishe anagoma nyumbani kwake, si kuweka lori lake njiani atakamatwa,” alisema.
Dk. Magufuli aliwataka wasafirishaji nchini kutambua kuwa uzito wa tani 56 katika barabara ni mkubwa kuliko ule unaotumiwa na wafadhili katika nchi zao.
Naye Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, alisema wao kama walinda usalama wa raia na mali zao, hawatakubali kutokea tukio kama lile la juzi lililofanywa na baadhi ya wasafirishaji kuvuruga amani.
Alisema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha kila atakayekusudia kuanzisha vurugu kama zile za juzi anachukuliwa hatua.
Chanzo:- Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment