Social Icons

Monday, 11 November 2013

BAADA YA M23, KONGO KUPAMBANA NA FDLR

Mwanzoni mwa wiki hii kundi la waasi wa M23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), limetangaza kuweka silaha chini na kurejea kwenye meza ya mazungumzo na serikali ya Kinshasa, ambayo yamekuwa yakifanyika Kampala nchini Uganda kwa lengo la kumaliza mzozo wa Mashariki mwa nchi hiyo.

Kauli ya M23 imetolewa wakati huu ambapo wapiganaji wake wamerudishwa nyuma na vikosi vya Serikali kwa ushirikiano na Kikosi Maalumu cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO), na kukimbilia kwenye milima inayopakana na nchi za Rwanda na Uganda.

Kikosi cha MONUSCO chenye wanajeshi 3,000 kinawajumuisha wanajeshi kutoka Malawi, Afrika Kusini na Tanzania na kina jukumu la kukabiliana na waasi mashariki mwa DRC. Kinajiunga na walinda amani 17,000 ambao tayari wako sehemu mbalimbali nchini humo.

Tayari hali ya mapigano imeshuhudiwa kusimama kwenye baadhi ya maeneo huku wanajeshi wa Serikali wakiendelea kurusha makombora kwenye milima ya Chanzu, Mbuzi na Runyonyo kuwasambaratisha wapiganaji hao.

M23 iliingia katika mazungumzo ya kutafuta amani ya DRC na serikali yanayofanyika mjini Kampala, Uganda, lakini mazungumzo hayo yalisambaratika mwezi uliopita na kusababisha jeshi la Congo kufanya mashambulizi dhidi ya waasi hao.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Sadc na ambaye pia ni Rais wa Malawi, Joyce Banda, ameitaka Serikali ya DRC kurejea katika meza ya mazungumzo na waasi, kwa kile alichokiita kwa ajili ya amani ya DRC, kwani hatua za kijeshi pekee haziwezi kuutatua mzozo huo.

Rais Paul Kagame wa Rwanda hakuhudhuria mkutano huo lakini Rais Yoweri Museveni wa Uganda alikuweko na alisema kuzuka upya kwa mapigano nchini DRC hakukutarajiwa. Umoja wa Mataifa umekuwa ukiishutumu Rwanda na Uganda kwa kuwasaidia waasi nchini DRC madai ambayo nchi hizo imeyakanusha.

Nyuma ya vichwa vya habari vya kusimama kwa vita nchini humo, hali halisi bado si shwari na hakuna anayejua hatima ya nchi hiyo baada ya majeshi ya Tanzania, Afrika Kusini na Malawi yatakapoamua kuondoka.

Kitendo cha kikundi cha waasi cha M23 kuweka silaha chini katika nchi ya DRC, hali bado huenda isiwe shwari katika miaka kadhaa ijayo kwani bado kuna vita nyingine ya kupambana na wanamgambo wa Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR).

Msimamo huo umeungwa mkono na viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) katika mkutano wao uliofanyika wiki hii Pretoria nchini Afrika Kusini, kwa ajili ya kufanya tathmini ya mafanikio ya mpango wa amani katika eneo hilo. Serikali ya DRC imesema kwamba baada ya majeshi yake kufanikiwa kuwadhibiti wapiganaji wa M23 na kuchukua maeneo yote waliyokuwa wakiyashikilia, oparesheni hiyo inaendelea kwa kuwashughulikia wanamgambo wa FDLR waliopo nchini humo.

Msemaji wa Serikali ya DRC, Lambert Mende alisema hayo na kusisitiza kuwa hakuna nafasi tena nchini humo kwa jeshi ambalo si rasmi, ambapo baada ya kuwadhibiti M23 wanaanza kulidhibiti kundi linalofuatia kwa ukubwa la wanamgambo wenye asili ya nchi ya Rwanda, FDLR kisha kuondoa masalia ya makundi madogo kama wanamgambo wa Mai Mai wanaaongozwa na mtu aitwaye Muhima Shetani.

Mende alisema kuwa kundi la wapiganaji wa M23 linaloundwa na watu wa jamii ya Kitutsi ambalo limeshindwa, limekuwa katika orodha ya juu kabla ya kusalimu amri rasmi wiki hii.

Chanzo:- Mwananchi

No comments:

 
 
Blogger Templates