Waandishi Bwana.Kazi yao kulalamika tu. Utadhani wao ni masupastaa kama waimbaji. Hebu wafikiche macho na kuona dunia jinsi ilivyo. Dunia hii si ya wazalishaji, ni ya watumiaji wa wazalishaji. Wenye uwezo wa kuuza maneno ni wanasiasa, si waandishi.
Chukua huyu mwandishi anayeitwa Richard Mabala. Fyatu kabisa. Hebu ona barua aliyoandika. Kama hapendi, si bora aandike makala kama mimi Makengeza. Angalau napata kavijitusenti (si kama vijisenti vya yule mwingine!) kila wiki. Potelea mbali kama kesho yake naona makala inafunga maandazi tu (au hata kufunga mabaya zaidi!). Lakini yeye aaah! Eti anataka kuandika kitu kinachodumu. Humu Bongo? Usinichekeshe.
Hebu niwapatie barua yake mkasome na kucheka pia. Lakini hakikisheni kwamba mnashika mbavu zenu zisije zikafyatuka kama Mabala mwenyewe.
Mpendwa Makengeza, kuna faida gani kuwa msanii hapa Bongo? Watu wanajidai eti wanawasikitikia wanamuziki wanavyonyonywa huku wakinunua nakala feki za muziki wao na kuwanyima kipato chao halali. Nakuambia hawa wanamuziki ni kaka zangu na dada zangu, katika kunyonywa na wajasiriawizi. Lakini nawaonea gere kitu kimoja. Angalau wanajitokeza kwenye maonyesho na fiesta na wapi sijui. Angalau wakiimba wimbo mbele ya kadamnasi watajua kama watazamaji wamependa au kuponda. Wanapata mrejesho wa kazi yao. Lakini asili ya uandishi ni upweke. Kuandika ni kama kutupa mshale gizani, hujui utaanguka wapi, hujui kama utamfikia mtu au la. Katika nchi nyingine, hata nchi jirani, angalau watu wengine wanabeba simu ya tochi au mshumaa kupunguza lile giza hivyo mshale wako unaonekana. Watu wanahakiki vitabu kwenye magazeti. Kuna vipindi vya redio na vya runinga kujadili vitabu vipya. Vitabu vipya vinaonyeshwa mahali pa wazi kwenye maduka ya vitabu na hata maktabani. Kuna vyama vya wapenda vitabu na kinachaguliwa kitabu kila mwezi kwa ajili ya watu kununua na kusoma. Lakini hapa ni giza totoro.Ndiyo maana nilimshangaa mwandishi mwenzangu ambaye nilimwona akihojiwa kwenye runinga. Sikuona mwanzo wake lakini nahisi yeye si mwandishi wa vitabu vya kubuni bali vitabu vile vya maswali na majibu kwa ajili ya watahiniwa. Si wazo baya, iwapo kweli amejikita kuleta maudhui iliyotosheleza kweli, yenye umakini na usahihi inayopanua kuliko kufinya elimu lakini nahisi vitabu vyake viko ndani ya kundi la vitabu vyenye makosa mengi na majibu finyu. Sijui. Lakini nilicheka alivyokuwa anajitetea, eti hakuna shida, maana kama amechemsha, ni juu ya watu kuamua, eti kwenye soko huru, soko lenye usawa daima vitabu bora vitajitokeza.
Ndivyo ilivyo kweli? Hivi ni kweli vitabu vyote shuleni vimechaguliwa kwa sababu kweli, kwelikweli, kwelikwelikweli ni bora kuliko vingine. Hebu nikupe mfano. Upande wa uandishi wa kubuni, kuna zawadi imetolewa mara kadhaa kwa riwaya bora ya mwaka. Vingapi vilivyoshinda vimeingia kwenye muhtasari wa shule? Na kama haviingii pale, nani atajua kwamba mtu ameandika kitabu? Giza tupu!
Naomba nitoe mfano wangu. Miaka ishirini na tano iliyopita niliandika vitabu viwili ambavyo kwa bahati nzuri viliingia kwenye mpango wa kuboresha Kiingereza shuleni. Viliandikwa kama vijitabu vya ziada kwa ajili ya kuwafanya vijana wafurahi kusoma Kiingereza hivyo kupata hamu ya kusoma zaidi lakini nikakuta kwamba baadaye vimewekwa kama vitabu cha kiada pia.
Unaona Makengeza? Umeshaanza kuwaza jinsi nilivyoula. Kweli toleo ya kwanza vilinunuliwa vyote na kusambazwa ilivyotakiwa kwa hiyo hata mimi nilipewa mrabaha wangu wa asilimia kumi na kununua gari langu la kwanza. Safiiii! Na vilisomwa kwa hiyo nilipata mrejesho watu walionaje. Lakini baada ya hapo, wale wajasiriawizi, wenye ubunifu wa kuiba kazi za wengine waliingilia kati. Sasa, popote ninapotembea nakuta vitabu feki vinauzwa. Mchapishaji akijaribu kuchukua hatua, wajasiriawizi wanapigwa faini ndogo sana na wajasiriahaki kule mahamani kiasi kwamba wanaenda kutengeneza maelfu zaidi ya vitabu huku mwandishi hapati kitu. Natamani kwenda kununua hivi vitabu feki na kuvichoma mbele ya maduka yanayouza. Lakini najua nitasingiziwa ‘civil disobedience’ na kushtakiwa kwa uhaini.
Lakini angalau nimesomeka. Watu wakikutana na mimi mara ya kwanza wanacheka. Si kwa sababu ya kitambi changu cha mkongoroko, bali kwa sababu wanakumbuka ufyatu wa Mabala mkulima ndani ya kitabu. Kwa hiyo, bila shaka napaswa kujivunia kwamba angalau nimeandika kitabu ambacho kimewavutia wezi wafaidi kwa niaba yangu. Sifa kubwa hii ndani ya Bongo.
Haya, nimeendelea kuandika vitabu, hasa kwa mkataba na mashirika mbalimbali. Jina langu linafahamika kidogo. Lakini kutokana na waheshimiwa wa elimu kuamua kusambaratisha tasnia ya uchapishaji na uuzaji wa vitabu, njia ya kawaida ya kuandika imezibwa. Hadi leo, kuna vitabu vyangu vidogo vya watoto havijatoka hata baada ya miaka minane. Vingine vimekubaliwa kwenye shule za Kenya lakini Bongo … ndoto ya mchana. Vingine vilipata tuzo ya mwandishi bora wa vitabu vya watoto wa Baraza la Kiswahili la Taifa lakini shuleni … thubutuuuuu!
Ndiyo maana namshangaa huyu mwandishi mwenzangu anayesema kwamba katika soko huria hakuna kulia. Tena ningependa kukutana naye na kumwuliza anatumia mbinu gani hadi vitabu vyake vifahamike vile. Nadhani kujitangaza ni kipaji pia.
Haya sasa, mwaka jana niliamua kujitosa kwenye mashindano ya kuandika riwaya kwa ajili ya vijana katika lugha ya Kiingereza. Nikajikunja na waandishi wenzangu wanajua kujikunja maana yake ni nini. Mgongo unapinda hadi watu wanafikiri kisogo ndiyo uso. Miezi mitatu na zaidi kuandika kila siku! Na bahati nzuri nilishinda tuzo. Tuzo kubwa kidogo linaloshinda mrabaha wa miaka kumi. Na tuzo haliwezi kuibwa na wajasiriawizi.
Basi, kwa ujinga wangu, nilifikiri kwamba angalau kitabu kitakuja kufahamika. Kinaweza kupondwa pia, sawa kabisa, lakini angalau kifahamike. Angalau watu wakisome na kutoa sababu kwa nini wanapenda au kuponda. Lakini baada ya sherehe ya tuzo, ambayo iliandikwa na magazeti machache na kuhojiwa kirefu na gazeti moja, kimyaaaa! Nikajiuliza hivi watu watajuaje kwamba kuna kitabu kimetoka iwapo hakuna angalau uhakiki mahali?
No comments:
Post a Comment