MSOMAJI wangu Brown Mwangomale wa Mbeya, ambaye amejitambulisha kwangu akisema ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), baada ya kuipitia makala yangu ya wiki iliyopita, iliyokuwa imebeba kichwa cha habari kisemacho; Pona ya CCM 2015 ni kujikabidhi kwa mafisadi, alinipigia simu kunipongeza.
Pongezi zake hizo zilifuatiwa na mazungumzo marefu kiasi kati yetu, yaliyotuchukua karibu dakika 20, akinieleza jinsi anavyoumizwa na mwenendo wa CCM ya sasa na hasa yale yanayofanywa na watendaji wake katika ngazi za wilaya na mikoa.
Kwa kifupi Mwangomale, anasema CCM, katika ngazi zote za wilaya na mikoa nchini hakipo, kimekufa. Anasema karibu wenyeviti wote wa wilaya na mikoa waliochaguliwa mwaka jana katika uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho, badala ya kushughulika na kero za wananchi, na kuwaambia wananchi wa maeneo yao juu ya kazi nzuri iliyofanywa na serikali yao kwa ajili ya maendeleo yao, wao wamejikita zaidi katika kuwashughulikia wanachama wenzao waliokuwa washindani wao katika nafasi zao hizo wakati wa uchaguzi huo.
Anasema makatibu wa CCM katika ngazi za wilaya na mikoa ni waajiriwa wa Chama, wanalipwa mishahara na posho kutokana na kuwa makatibu watendaji, wamewezeshwa magari ili kuwarahisishia kuyafikia maeneo yenye watu kwa lengo la kukutana na wananchi, lakini nao pia hawafanyi kazi za chama na mara nyingi magari yao hayo waliyopewa na Chama, utayakuta yameegeshwa kwenye vilabu vya pombe na starehe nyingine kuanzia asubuhi hadi usiku wa manane.
Anatolea mfano wa mkoa wake wa Mbeya, akisema tangu watendaji wa CCM wachaguliwe katika ngazi mbalimbali za uongozi mwaka jana, haoni wenyeviti wala makatibu wake wakiitisha mikutano ya hadhara kuzungumzia maendeleo na kero za wananchi, bali wamekalia malumbano ya wenyewe kwa wenyewe na dhidi ya viongozi wa vyama vya upinzani.
Ndipo hapo Mwangomale anapoungana nami akisema pona ya CCM hii ya sasa mwaka 2015 ni kujisalimisha tu kwa mafisadi wenye fedha ili watumie fedha zao hizo kununua shahada za kupigia kura ili kupunguza kura za wapinzani wao.
Kimsingi, nilikubaliana naye, naamini hata wana CCM wenye chama chao, wanaoamini katika imani yao ya kwamba nitasema kweli daima fitina kwangu ni mwiko, watakubaliana na Brown Mwangomale, kada wa CCM aliyeko mkoani Mbeya, kwamba katika ngazi za wilaya na mikoa, CCM imekufa, haipo.
Mwangomale amegusia namna watendaji wa CCM katika ngazi za mikoa na wilaya wanavyochangia kwa namna moja au nyingine kukiua chama chao hicho. Lakini kwangu, hata katika ngazi ya taifa, siioni CCM yenye uhai, bali naiona mitifuano miongoni mwa makada wake, mitifuano inayozidi kukielekeza chama hicho kibra.
Tumeyasikia na kuyaona haya hivi karibuni kati ya mafahari wawili wa CCM katika siasa za kanda ya kaskazini mwa Tanzania na Tanzania kwa ujumla wake; Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa. Hakuna shaka yoyote kwamba wawili hawa ni vigogo ndani ya CCM na wanao watu wengi nyuma yao wanaowaunga mkono katika mbio zao za urais.
Kwa mtazamo wangu, Sumaye na Lowassa wanaposimama na kushambuliana wao kwa wao hadharani au wanaposimama hadharani na kuishambulia serikali ya chama chao kwa hili na lile wakidhani wanajijenga kisiasa mbele ya Watanzania, kwa hakika wanakuwa sawa na wenyeviti na makatibu hao wanaolalamikiwa na Brown Mwangomale.
Hawa wanajijenga wao kisiasa kwa gharama ya chama chao na matokeo yake, kesho watakuwa wagombea urais kupitia chama mfu, walichoshiriki wao wenyewe kukiua bila kujijua.
Tumemsikia Lowassa akisimama bungeni hivi karibuni kuendeleza wimbo wake wa mara kwa mara, wa ukosefu wa ajira kwa vijana wa nchi hii ni bomu linalosubiri kulipuka. Lowassa anailamu serikali ya chama chake ndani ya Bunge kwamba inaendesha mambo yake kiuswahili swahili, inaogopa kutekeleza mipango mikubwa na hivyo kujikuta ikiwa na mipango mingi midogo isiyo na tija kwa ajira na uchumi wa nchi.
Tukumbushane, mwasisi wa msemo wa kwamba ukosefu wa ajira kwa vijana katika nchi hii ni bomu linalosubiri kulipuka, ni Mwandishi Habari Nguli wa hapa nchini, Jenerali Ulimwengu. Amelisema sana hili kupitia makala zake tangu enzi za awamu ya pili na ya tatu, Lowassa akiwa serikalini bado, lakini hakuna mahali popote katika kumbukumbu zangu panapoonyesha kwamba mwanasiasa huyo alisimama na kumuunga mkono Jenerali katika rai na wito wake huo.
Lakini pia suala hili la ajira kwa vijana wetu, limefafanuliwa kwa mapana yake katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015 katika sura ya Tano, Ibara ya 77. Na kwa kiasi kikubwa serikali hii ya CCM, chini ya Rais Jakaya Kikwete, imejitahidi kwa kadiri kutekeleza Ilani yake hiyo, ila tatizo liko kwa vijana wetu wenyewe kujituma katika kazi za ujasirimali na katika kipengele cha juhudi na maarifa, eneo ambalo kina Lowassa wangesaidia kuwaelimisha vijana kuacha tabia ya kuchagua kazi.
Kwa kifupi tu niseme Lowassa anaposimama bungeni na kuibomoa serikali ya chama chake kwa upande mmoja na Sumaye akasimama upande wa pili kuwabomoa makada wenzake kwamba ni mafisadi na wala rushwa, huku akijua kwamba serikali yake, akiwa Waziri Mkuu ndiyo iliyohalalisha rushwa kisheria kwa kuiita takrima, wote hawa wanashiriki kukiua na kukibomoa chama chao.
Na ieleweke hapa kwamba mnyukano huu wa Lowassa na Sumaye, ni rasharasha tu. Mnyukano wenyewe bado. Tusubiri kuona mpambano wa mvua ya mawe miongoni mwa makada wa CCM walioko kwenye mbio za urais katika nusu ya pili ya mwakani na nusu ya kwanza ya mwaka 2015. Mimi si mtabiri, lakini kwa jinsi wapambe wa wasaka madaraka hao ndani ya CCM walivyojipanga, nasema tujiandae kwa rambirambi na kusoma tanzia!
Kina Lowassa na Sumaye ni tatizo jingine linaloliangamiza CCM. Inawezekana, ndani ya CCM wapo mawakala na wapambe waliokaa mkao wa kula fedha za wasaka urais hawa na kwa hiyo wasingependa kulisikia hili la kina Lowassa na Sumaye kuwa tatizo kwa kuwa lililomo ndani ya vinywa vyao ni ‘mambo yanakwenda vizuri mzee’ ili waendelee kuyatafuna mafungu ya fedha yaliyotengwa katika maandalizi hayo ya urais.
Hata hivyo, nihitimishe makala haya kwa kusema CCM kama chama cha siasa, naamini kinajua hatari ya kuteua mmoja wapo kati ya makundi hayo yaliyoko kwenye mapambano ya kusaka urais. Moja ya hatari hiyo, ni ile hasira ya ‘bora tukose wote!’
Kwa hiyo, dawa sahihi kwa CCM ni kuyatosa makundi yote mapema, bila hata kuhitaji kujadili fomu zao za maombi ya uteuzi kwenye vikao vyake, kama alivyofanya Mwalimu mwaka 1995 kwa Lowassa na John Malecela na kama alivyofanya Mzee Benjamin Mkapa kwa Malecela huyo huyo mwaka 2005.
No comments:
Post a Comment