Social Icons

Wednesday, 20 November 2013

CCM YAMTAKA JK AWATIMUE KAWAMBWA,CHIZA NA MALIMA

MawaziriMAWAZIRI watatu wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete wapo katika wakati
mgumu baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Nape Nnauye, kutangaza rasmi kuwa atahakikisha wanachukuliwa hatua za
kuwajibishwa kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Wakati Nape akitaka mawaziri hao watimuliwe, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulhaman Kinana, amesema kuwa mawaziri hao watawekwa kiti moto katika kikao kijacho cha Kamati
Kuu (CC), kwa lengo la kueleza ni hatua gani wanachukua katika
kushughulikia matatizo ya Watanzania.

Mawaziri hao ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi
Christopher Chiza,  Naibu wake, Adamu Malima  na Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa ambaye ametajwa kuwa sehemu ya
matatizo katika kila wizara anayopewa kuiongoza.

Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Wilaya
ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Nape alisema hakuna sababu ya kukaa kimya
wakati mawaziri hao wameshindwa kazi, hivyo ni vema wakawajibishwa
ili kukiokoa chama chao.

Kuhusu Chiza na Malima, Nape alisema mawaziri hao wameshindwa
kutekeleza wajibu wao kwani tangu walipochaguliwa kuongoza wizara hiyo
hakuna hata siku moja ambayo wamefika Ruvuma kushughulikia matatizo ya
wakulima wakiwamo wa korosho, tumbaku, mahindi  na mpunga, ambapo
katika mikoa mbalimbali nchini imekuwa ikilalamikia sekta ya kilimo
lakini wenyewe wamekaa kimya bila kuchukua hatua zozote.

“Katibu Mkuu leo ni bora nikazungumza haya ya mawaziri ambao wamepewa
dhamana ya kuwatumikia Watanzania. Nimeuliza hapa Ruvuma Waziri wa
Kilimo na naibu wake walishawahi kufika mara ngapi kushughulikia
matatizo ya wakulima. Jibu lake, hakuna hata siku moja wamefika.

“Hii inaleta tabu, wakati wakulima wanahangaika na pembejeo za kilimo,
ukosefu wa soko na malipo ya fedha wanazodai serikalini mawaziri
wenye dhamana wapo mjini wanafunga tai na suti. Hawafikiri kuhusu matatizo ya wakulima,” alisema.

Aliongeza kuwa yupo tayari kupoteza nafasi yake lakini hawezi
kuvumilia hali hiyo ikaendelea na kutumia nafasi hiyo kumuoma Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ahakikishe wanachukuliwa hatua na
ikiwezekana waitwe CC wahojiwe.

Alisema karibu Tanzania yote wakulima wamekuwa na matatizo mengi na
wamekuwa wakilalamikia wizara hiyo na yeye ni shahidi wa hayo
yanayoendelea kutokea na ili kukinusuru chama hicho mawaziri
walioshindwa kazi wawajibishwe.

Alisema kuwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika imepewa dhamana ya
kuwatumikia Watanzania asilimia 80, ambayo ni wakulima lakini waliopewa
jukumu hilo hawataki kufanya kazi zao.

“Wananchi naomba mnilinde, lakini niseme ukweli. Niseme nisiseme…mawaziri
ambao tumewapeleka jikoni wameshindwa kupika chakula, tunasubiri
sebuleni lakini chakula hakiji. Wanatukwamisha, ni bora wakaondoka kama
wameshindwa kazi.

“Katibu Mkuu mimi nikija, sipo tayari kuona CCM inakuwa chama cha
upinzani bungeni kwa sababu tu ya hawa wenzetu wachache ambao wanafanya
makusudi na uzembe katika kutekeleza wajibu wao,” alisema Nape.

Wakati kwa Dk. Kawambwa mbali ya kushindwa kuongoza Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi naye anatakiwa kuchukuliwa hatua kutokana na mkataba
aliouingia na makandarasi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Namtumbo
hadi Tunduru mkoani Ruvuma.

Nape alisema anamshukuru  Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kwa
kumfukuza mkandarasi huyo aliyemtaja kwa jina la Progressive ambaye
ameshindwa kazi ya kujenga barabara hiyo.

Hata hivyo, kumfukuza mkandarasi huyo pekee haitoshi, hivyo
aliyehusika kumpa mkataba anapaswa kuchukuliwa hatua kwani uchunguzi
unaonesha kuwa alishashindwa kazi na wakati anapewa mkataba huo Waziri
husika alikuwa Dk. Kawambwa.

“Dk. Kawambwa amekuwa akitukwamisha CCM katika kutimiza wajibu wake. Hii
barabara ya Namtumbo hadi Tunduru kushindwa kukamilika imeleta aibu
kubwa na kututia fedheha. Hivyo lazima waliotoa mkataba wawajibishwe.

“Dk. Kawambwa huyu huyu ameshindwa kushughulikia matatizo ya walimu
nchini na atambue kuwa tulimpa muda wa miezi sita na sisi tunahesabu,
ukimalizika hatutaacha kuchukua hatua.

“Chama kitatumia wabunge wake kumuwajibisha. Hatuwezi kukaa kimya. Iwapo
ninaonekana kama kero kwa kupigania masilahi ya nchi na watu wake, nipo
tayari kuondoka na kwenda kujihusisha na kilimo. Maana mimi ndiye mpiga
debe wa chama, nitakwenda kueleza nini kwa umma kutokana na ahadi zetu
kukwama kwa sababu tu ya uzembe wa wachache ndani ya
serikali?” alihoji.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM, Kinana, alisema kuwa
katika kikao kijacho cha Kamati Kuu (CC), kitakachofanyika Desemba
mwaka huu chama kitamuandikia barua Rais Jakaya Kikwete ili mawaziri
wake waje wajieleze mbele ya kikao kwa nini wasifukuzwe kwa
kushindwa kazi.

Chanzo;- Tanzania Daima

No comments:

 
 
Blogger Templates