Dar es Salaam. Ni wazi kwamba hali ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo si shwari. Kumekuwa na malumbano ya muda mrefu tena kwenye mitandao ya kijamii ambapo makada na viongozi wa chama hicho wamekuwa wakitupiana lawama.
Malumbano hayo hayakuanza leo wala jana, yamekuwapo kwa muda mrefu. Kwanza mitandao maarufu kama vile Jamii Forums, ilikuwa ikiinufaisha Chadema kwa kuwa mashabiki wake waliutumia kukishambulia chama tawala, CCM kwa upande mmoja na kutiana moyo kwa upande mwingine.
Hali kwa sasa katika mtandao huo na mingineyo imebadilika kuwa sehemu ya kushambuliana wao kwa wao. Watu wamekuwa wakijiita majina bandia na kushambuliana watakavyo. Hata viongozi wa chama hicho wamekuwa wakiutumia mtandao huo kushambuliana.
Ndipo sasa linapokuja suala la Zitto Kabwe ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho kumwandikia Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa akitaka maelezo ya tuhuma zinazorushwa kwenye mitandao zikimtuhumu kwa ufisadi na mkakati wa kuhujumu chama.
Haya yote yanatokea kwa sababu ya mvutano wa madaraka uliomo katika chama hicho. Itakumbukwa kuwa mwaka 2009, Zitto alionyesha nia ya kukitaka kiti cha uenyekiti wa chama hicho, hata hivyo wazee wa chama hicho walimsihi ajitoe ili Mbowe aendelee na ngwe yake ya pili.
Hata hivyo, Zitto hakuishia hapo bado amekuwa na harakati nyingi ziwe halali au haramu, jambo linaloonkana kuwa tishio katika uongozi wa sasa. Kuna mawili, ama uongozi wa chama unajaribu kummaliza kupitia mitandao ya intaneti kwa kumtupia kashfa hizi na zile au anavuna alichokipanda, yaani kutaka umaarufu kupatia chama chake.
Ni wazi kwamba Zitto tofauti na viongozi wenzake amekuwa akitafuta umaarufu kuliko chama. Wenzake wakienda kulia, yeye yuko kushoto, wakienda na Movement for Change (M4C), yeye yuko na kamati hii, mara yuko safari ya hii na ile, ilimradi tu na yeye amefanya kitu tofauti na wenzake.
Hali hii inamfanya kuonekana msaliti na pengine ndiyo sababu kashfa kama hizo zinamwandama.
Lakini kitu kimoja ambacho naona viongozi wa Chadema hasa Mwenyekiti, Mbowe na Katibu Mkuu Dk Slaa, wanakosea ni kutokuwa wazi kuhusu masuala yanayomwandama Zitto. Je, vitimbi hivi anavyofanyiwa vina baraka za chama au havina?
Kama havina baraka za chama kwa nini chama kisijiepusha navyo kwa kuvikana? Kama kweli Zitto ni msaliti kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kama walivyowahi kushughulikiwa kina David Kafulila.
Inawezekana kweli Zitto ni msaliti, lakini kwa ukimya huu anapata nafasi ya kutafuta huruma kutoka kwa wanachama na wapenzi wa chama. Ukimya huu wa Dk Slaa na Mbowe unamaanisha nini?
Chanzo:- Mwananchi
No comments:
Post a Comment