WAZIRI Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye ameanza rasmi harakati zake za kusaka kuungwa mkono miongoni mwa wanaCCM, katika mbio zake za kugombea urais mwaka 2015 katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Habari za uhakika zilizopatikana kutoka jijini Mwanza zinasema hivi karibuni, Sumaye alipiga hodi Kanda ya Ziwa na kuendesha vikao vya ‘siri’ kwa lengo la kutafuta kuungwa mkono. Kanda ya Ziwa, kwa muda mrefu sasa, ikiaminika kuwa moja ya ngome muhimu katika kuamua mshindi ndani ya vikao vya mchujo CCM.
Kwa mujibu wa habari hizo, katika vikao vyake, Sumaye alikutana na makundi mablimbali kwa nyakati tofauti. Kundi la kwanza likitajwa kuwa la wafanyabiashara, ambao kikao chao hicho kilifanyika katika moja ya hoteli maarufu kwa burudani jijini Mwanza, eneo la Kirumba.
Kikao cha pili kinaelezwa kuwakutanisha baadhi ya viongozi wa dini katika moja ya hoteli iliyoko katikati ya Jiji la Mwanza, wakati kikao cha tatu kikifanyika katika ufukwe mmoja wa kisasa ulioko maeneo ya Igombe, nje kidogo ya Jiji la Mwanza, kikiwahusisha wanasiasa, wengi wao kutoka CCM.
Juhudi za kumtafuta Sumaye, ili pamoja na mambo mengine aweze kuzungumzia taarifa hizi, hazikuzaa matunda baada ya kuambiwa na mmoja wa wana familia yake kwamba alikuwa safarini nchini Dubai.
Mmoja wa viongozi wa CCM Mkoa wa Mwanza, anayeaminika kuwa bingwa wa mikakati ya ushindi, na ambaye anafahamika hapa Mwanza kuwa kambi tofauti na Sumaye, amethibitisha kuhudhuria kikao hicho kilichowakutanisha wanasiasa, ingawa haijafahamika kama kuhudhuria kwake huko ni ishara ya kubadili mwelekeo wa kambi.
“Huyu (Sumaye) alikuwa anafikiriwa kuwa atagombea, lakini alikuwa hajaanza mapambano rasmi. Sasa ujio wake hapa Mwanza umezishitua kidogo kambi nyingine, na hasa ikizingatiwa umuhimu wa kura za Kanda ya Ziwa. Kuingia kwake kumeleta taharuki kidogo,” kilieleza moja ya chanzo chetu cha habari hizi ambacho kilihudhuria moja ya vikao vya mwanasiasa huyo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja anayetajwa kuwa kambi ya Waziri wa kwanza wa Awamu ya Nne, Edward Lowassa, amelithibitishia gazeti hili kufanyika kwa vikao hivyo vya Sumaye, akisema baada ya kukamilisha vikao hivyo, kiongozi huyo alisafiri hadi Butiama kuzuru kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Wakati Sumaye akianza harakati zake hizo katika kanda hiyo, kumekuwepo taarifa kwamba kambi ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa katika kuusaka urais wa 2015, imebadili mbinu za kutafuta uungwaji mkono katika kanda hiyo.
Kambi hiyo ya Lowassa kwa sasa inadaiwa kumtumia William Ngeleja, kutafuta kuungwa mkono katika kanda hiyo ya ziwa ili kukwepa mashambulizi kutoka kwa makundi mengine ya wasaka urais, huku ikielezwa ni kupunguza hatari ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu na chama chake endapo atabainika kujihusisha na rafu hizo kabla ya wakati.
“Huu ni mkakati tu wa kuimarisha kambi ya Lowassa. Kinachofanyika hivi sasa ni kuwaonyesha watu kuwa kuna mtu wa Kanda ya Ziwa anasaka urais ili avunje nguvu za wagombea wengine, lakini wakati ukifika Ngeleja atarejea kwenye kambi yao na kuwataka wote wanaomuunga mkono wahamie kambi ya Lowassa,” chanzo chetu cha awali kutoka ndani ya CCM Wilaya ya Ilemela, kinafafanua kuhusu mbinu hizo zinazodaiwa kuwa ni za kambi ya Lowassa kumtumia Ngeleja.
Hata hivyo, mmoja wa watu walio karibu na Lowassa ambaye hakuta jina lake kuandikwa gazetini, amekanusha taarifa hizi za kambi hiyo kubadili mbinu kwa kumtumia Ngeleja, akisema mwanasiasa huyo kijana na ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema, ameingia kwenye mbio hizo za urais 2015 na kampeni anazoziendesha hazifanyi kwa niaba ya Lowassa, bali kwa ajili yake mwenyewe.
“Ngeleja haendeshi kampeni katika Kanda ya Ziwa kwa niaba yetu, bali kwa niaba yake. Nimeongea naye mimi mwenyewe hivi karibuni mjini Dodoma, amenihakikishia atachukua fomu ya kuomba chama kimteue mwaka 2015, kama kuna watu wanadhani anamfanyia kampeni mzee (Lowassa), basi hao hawajui,” kilisema chanzo chetu hicho cha habari kilicho karibu na Lowassa.
Kauli hiyo ya mtu huyo wa karibu na Lowassa ambaye, imeungwa mkono na kiongozi mmoja wa CCM Mmkoa wa Mwanza ambaye anasema; “Ukweli ni kwamba (Ngeleja) amejiengua kutoka kambi aliyokuwa (ya Lowassa) na ameamua kwa dhati kugombea baada ya kushauriwa na wazee kwamba Kanda ya Ziwa imechoka kuwa msindikizaji na safari hii wanataka mgombea wao.”
Kambi hiyo ya Ngeleja inadaiwa kuungwa mkono na mmoja wa wazee waliokuwa wanaongoza timu ya kampeni ya Rais Jakaya Kikwete Kanda ya Ziwa wakati anawania urais mwaka 2005. Aidha, Ngeleja anaelezwa kuungwa mkono na makatibu na wenyeviti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) katika baadhi ya wilaya za mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Geita.
Kanda ya Ziwa inayoundwa na mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Kagera, Simiyu na Geita, imekuwa ikitazamwa na wachambuzi wengi kwenye medani za siasa kama yenye ushawishi mkubwa kutokana na ukweli kwamba theluthi moja ya idadi ya Watanzania wanatoka kanda hiyo.
Akizungumzia harakati hizo za Ngeleja, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mgeja anasema: “Kuendekeza ukanda au hata kutazamana kwa nani ni wa nani, kutalipeleka taifa hili kubaya na kuleta mmeguko usio na sababu. Mimi naamini mgombea atatokana na Chama na Watanzania wote, haya mambo ya kanda mimi siyaafiki, yataligawa taifa ni ya kuepukana nayo.”
Akizungumzia madai kwamba yeye yuko kambi ya Lowassa, Mgeja anasema: “Nitakuwa mnafiki nikimkana. Lakini huu ni upendo wangu binafsi, nampemda kama Mtanzania yeyote na tusihukumiane kwa kuangalia kuwa huyu ni wa mtu fulani na huyu wa mwingine, tuwe makini.”
Wakati Sumaye, Lowassa na Ngeleja wakielezwa kuendesha harakati hizo za kutafutwa kuungwa mkono katika mbio zao hizo za urais mwaka 2015, Katibu wa NEC (Itikadi na Uenezi) wa CCM, Nape Nnauye amezungumza na gazeti hili akisema wote ambao wameanza harakati hizo za kusaka urais kabla ya muda, moja kwa moja wanakosa sifa za kuteuliwa kwa mujibu wa kanuni za chama hicho.
“Kwanza naamini, wote hao wanaotajwa kuanza harakati za kusaka urais wa 2015, wanazifahamu kanuni za chama chetu kuhusu suala hilo. Kwa hiyo, kama kuna walioanza vikao vya kusaka urais, moja kwa moja wanajikosesha sifa ya kuteuliwa kuwa wagombea wa chama chetu,” anasema Nape.
No comments:
Post a Comment