Imani hizo zimesababisha watu watano kuzikwa wakiwa hai, masoko kuungua, watu kuchunwa ngozi na kujeruhiwa kwa nondo.
Siri ya migogoro na matatizo ya vurugu mkoani Mbeya yakiwamo ya kuungua kwa masoko imefichuka, baada ya machifu kupitia Taasisi ya Muungano wa Jamii Tanzania (Mujata) kugundua kuwa ni ushirikina uliokithiri wa wafanyabiashara. Machifu wanasema vitendo hivyo kwa kiasi kikubwa vinachangia kuvuruga kasi ya maendeleo ya mkoa huo.
Kwa mujibu wa Mujata, hata viongozi nao hasa wale wa kisiasa wanachangia kuwepo kwa hali tete mkoani humo, kwa kushindwa kuwapa taarifa wananchi, huku wengine wakijiingiza katika ufisadi kupitia wananchi.
Masoko kuungua mara kwa mara
Mwenyekiti wa Mujata nchini, Chifu Shayo Masoko anasema chanzo cha masoko kuungua mkoani humo, ni kuwepo kwa imani za kishirikina miongoni mwa wafanyabiashara wanaolezwa na waganga kuwa wakichoma moto mali zao na za wenzao watapata utajiri zaidi.
Mwaka 2009 Soko la Tunduma liliko mpakani mwa Tanzania na Zambia liliungua na baadaye mwaka 2010 soko kongwe la Uhindini jijini hapa liliteketea kwa moto katika mazingira ya kutatanisha.
Hata hivyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja anasema Serikali inaamini kwamba masoko ya Mwanjelwa na Uhindini yaliungua kutokana na hitilafu ya umeme, wakati lile la Sido liliungua kwa moto wa mama lishe.
Kwa upande wa Mujata, Chifu Masoko anasema kutokana na kukithiri kwa matukio hayo, viongozi wa taasisi yake walikutana na kupokea taarifa za walinzi wa kijadi, waliotoa taarifa kwamba siri ya kuungua kwa masoko hayo ni ushirikina uliokithiri.
Walisema kuwa baadhi ya wafanyabiashara waliahidiwa kupata mtaji mkubwa kama wangeunguza moto bidhaa zao na za wafanyabiashara wengine.
’Katika uchunguzi wa kimila tulibaini kwamba mpango huo ulitaka kufika kwenye masoko ya Mbalizi na Wilaya ya Momba, jambo ambalo tulilazimika kufanya mikutano ya hadhara kukemea waziwazi tabia hiyo ya ushirikina’’ anasema.
Chanzo:- Mwananchi
No comments:
Post a Comment