Social Icons

Sunday, 10 November 2013

JK AAHIRISHA KWA MUDA KIFO CHA EAC


HOTUBA ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Alhamisi wiki hii bungeni mjini Dodoma, mbele ya mihimili yote mitatu ya dola, kwamba Tanzania haitajitoa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ni wazi kwamba inaweza kuahirisha kwa muda kifo cha Jumuiya hiyo.

Kabla ya kauli hiyo ya Rais, ambayo ilionekana kulenga kuleta utengamano, kauli zilizopata kutolewa kabla na mawaziri wawili, Samwel Sitta, anayesimamia Wizara ya Ushirikiano wa Afrika na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, zilitoa taswira kwamba Tanzania ilikuwa inafikiria kujitoa EAC, kutokana na kile kinachoonekana wazi kwa viongozi wa kisiasa wa nchi za Kenya, Rwanda na Uganda, kuitenga katika baadhi ya vikao vyake ya maamuzi.

Tofauti kabisa na mawaziri wake, Rais Kikwete amelieleza taifa kuwa Tanzania haitaki inyooshewe kidole kuwa chanzo wala kichocheo cha kifo cha Jumuiya hiyo, ingawa upo ukweli usiokuwa wa kutiliwa shaka kuwa bado uhai wa Jumuiya hiyo uko shakani, kutokana na itikadi kinzani za nchi wanachama ambazo zinaelezwa moja kwa moja kuwa ndizo zilizosababisha kuvunjika kwa jumuiya ya awali, mwaka 1977.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete alitoa msimamo wa Tanzania kutojitoa EAC na kueleza sababu zinazozisukuma baadhi ya nchi wanachama kuichukia kuwa ni msimamo wa viongozi wake kuhusu ardhi, ajira, uhamiaji na uharakishwaji wa shirikisho.

Ni itikadi hizo kinzani ndizo zinazotajwa na wafuatiliaji wa masuala ya Uhusiano wa Kimataifa, kuwa licha ya Tanzania kutamka bayana kuwa inatimiza ipasavyo wajibu wake na kushiriki kikamilifu katika ujenzi na utengamano wa EAC, lakini endapo wakuu wa Nchi za Kenya, Uganda na Rwanda wataendelea na mwenendo wa sasa, tishio la kuvunjika kwake liko dhahiri.

Mpaka sasa marais wa nchi hizo tatu wamekutana na kufanya vikao vitatu kwenye nchi zao kwa ajili ya kujadili ujenzi wa reli unaotarajiwa kukamilika mwaka 2017. Reli hiyo itapita katika nchi hizo tu, huku Tanzania na Burundi zikiachwa kando.

Mbali na ujenzi wa reli hiyo, marais hao pia wamejadili na kukubaliana kujenga kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta nchini Uganda na upanuzi wa Bandari ya Mombasa, nchini Kenya.

Aidha wamekubaliana kusaini mkataba utakaoruhusu wananchi wao kusafiri ndani ya nchi hizo bila kizingiti kwa kutumia kitambulisho cha taifa husika, sambamba na kufikia makubaliano ya ushuru wa pamoja wa forodha. 

Makubaliano haya yote yalisainiwa bila uwepo wa nchi za Tanzania na Burundi, ambazo pia ni wanachama wa EAC.

Baadhi ya wachambuzi na wataalamu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa wanaeleza kuwa kinachotokea sasa EAC ndicho kilichosababisha kuvunjika kwa jumuiya ya kwanza iliyokuwa ikiundwa na mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda mwaka 1977. Wakati huo, Kenya chini ya Rais wake, Jomo Kenyatta ilishutumiwa kuwa moja ya sababu za kuvunjika kwa jumuiya hiyo.

Akizungumza na gazeti la Standard la nchini Kenya hivi karibuni, Profesa Phillip Nying’uro, amesema mgogoro wa sasa wa EAC ni wa kiuchumi zaidi kuliko wa kisiasa.

Profesa huyo alikaririwa akieleza kuwa Tanzania inaishutumu Kenya kwa kuingilia makubaliano yake na nchi za Rwanda na Uganda.

Kwamba awali Uganda na Tanzania zilikubaliana kuimarisha Bandari ya Dar es Salaam, mpango ambao iwapo ungefanikiwa, ungekuwa pigo la kiuchumi kwa Kenya.

Hata hivyo, zipo taarifa zinazodai kuwa Rais Kenyatta amemzidi kete Rais Kikwete, baada kufanikiwa kuwashawishi marais Museveni na Kagame ili nchi zao ziache kuitumia Bandari ya Dar es Salaam na badala yake zipitishie mizigo yake katika Bandari ya Mombasa.

Hali kadhalika, Rwanda na Tanzania ziliwahi kusaini makubaliano ya ujenzi wa reli ya kati kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi Kigali na kwa Uganda reli hiyo ingetokea Tanga ikipitia Mara kuelekea Kampala. 

Inaelezwa kuwa upembuzi yakinifu wa miradi hiyo ulikwisha kufanyika, lakini hadi sasa haijulikani utekelezaji wake umefikia wapi.

Baadhi ya magazeti ya Kenya yameandika kuwa mkakati wa Kenyatta kuhakikisha anahodhi fursa ya kichumi kama ambavyo ilipata kutokea katika Jumuiya ya kwanza iliyovunjika 1977, ndio ambao unatishia kifo cha EAC.

Jumuiya ya kwanza ya Afrika Mashariki iliundwa mwaka 1967 na kudumu kwa miaka kumi, kabla ya kuvunjika mwaka 1977.

Chanzo cha kuvunjika kwa jumuiya hiyo ni hatua ya Rais Jomo Kenyetta kutaka kuhodhi uchumi wa nchi wanachama, jambo ambalo lilimkwaza Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye katika moja ya kauli zake za kupinga nia hiyo, alisema Kenya ni jamii ya mtu anayekula mtu, akilenga ufisadi uliokuwa umetamalaki nchini humo na unyakuzi wa ardhi.

Ni kwa mwenendo huo huo, Rais wa sasa wa Kenya, Uhuru Kenyatta, naye anaonekana kutaka kuhodhi uchumi wa eneo la Afrika Mashariki, jambo ambalo limethibitishwa na Rais Kikwete katika hotuba yake ya wiki iliyopita bungeni Dodoma, kuwa Tanzania inatengwa kwa sababu ya msimamo wa viongozi wake kuhusu ardhi, uhamiaji, ajira na uharakishwaji wa shirikisho.

Chanzo:- Mtanzania

No comments:

 
 
Blogger Templates