Arusha.Serikali za Rwanda, Uganda, Kenya na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, zimefunguliwa kesi katika Mahakama ya Afrika ya Mashariki, zikidaiwa kukiuka mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.
Hatua hiyo inatokana na Serikali hizo kufanya vikao vitatu mfululizo na kuzitenga nchi za Tanzania na Burundi.
Walalamikaji katika kesi hiyo, ni Ally Msangi, David Makata na , John Adam, ambao ni Watanzania, wanaotetewa na wakili Mwandamizi, Jimm Obedi wa jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, walalamikaji wamewaomba majaji katika mahakama hiyo, kutoa tamko la kusitisha utekelezaji wa maazimio yote ya vikao vya wakuu wa nchi hizo tatu.
Pia wameomba majaji watoe tamko la kukomesha kurejewa kwa vikao kama hivyo kinyume cha mkataba wa jumuiya hiyo.
Kesi hiyo ya aina yake, ilifunguliwa jana katika Mahakama ya Afrika ya Mashariki na kupokewa na Ofisa Masijala i katika mahakama hiyo, Boniface Ogoti.
Kufunguliwa kwa kesi hiyo, kunakuja siku kadhaa baada ya Rais Jakaya Kikwete kuzilalamikia nchi hizo, kuhusu kuitenga Tanzania kwa kufanya mikutano mbalimbali ya maendeleo ya nchi zao. Nchi nyingine iliyotengwa ni Burundi.
Kikao cha kwanza cha pamoja kilifanyika Aprili mjini Arusha kabla viongozi hao kukutana Juni 25 na 26 jijini Entebbe nchini Uganda, walidai kuwa na nia moja ya kurahisha mawasiliano katika nchi hizo.
Mkutano mwilingine ulifanyika mjini Kigali Rwanda Oktoba 28 ukiwajumuisha Rais Yoweri Museven wa Uganda, Uhuru Kenyatta (Kenya), Salva Kiir (Sudan Kusini) na Paul Kagame.
Wakili wa walalamikaji Obedi, alisema katika kesi ya msingi, wanawashtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Rwanda, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Uganda,Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Kenya na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo.
Chanzo:- Mwananchi
No comments:
Post a Comment