Social Icons

Thursday, 21 November 2013

MAPENZI YASABABISHA MAUAJI DAR

Polisi wakikagua gari walilokuwa wakisafiria watu wanne kabla ya kushambuliwa kwa risasi na Gabriel MunisiWATU wawili wameuawa jijini Dar es Salaam jana asubuhi baada ya kupigwa risasi kisha muuaji kujiua kutokana na kilichodaiwa kuwa wivu wa mapenzi.

Tukio hilo lilitokea Ilala Bungoni karibu na Klabu ya Wazee, baada ya mtu aliyetambulika kwa jina la Gabriel Munisi ambaye ni mfanyabiashara kutoka jijini Mwanza kuwashambulia kwa risasi watu hao.

Inadaiwa kuwa Munisi aliyetaarifiwa kuwa mchumba wake aliyetambuliwa kwa jina la Christina alikuwa na mtu mwingine kwenye nyumba moja katika eneo hilo, alikodi teksi hadi mahali hapo na baada ya muda akaliona gari aina ya Toyota Surf likitoka kwenye nyumba hiyo, akiwemo mpenzi wake.

Muuaji huyo alitoa bastola na kuanza kulishambulia gari hilo na kumuua kijana aliyefungua geti la nyumba kwa kumpiga risasi kichwani, akampiga mwanamke mwingine ambaye alikuwa amekaa katika siti ya mbele kwenye gari hilo, ambaye pia amefariki, huku dereva akijeruhiwa begani.

Ilidaiwa kuwa Gabriel aliwapiga risasi abiria wawili wasichana waliokuwa wamekaa siti za nyuma ya gari hiyo, na kuwajeruhi mabegani na mguuni na kisha alijipiga risasi na akafa papohapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marieta Minangi aliliambia gazeti hili kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi.

Inadaiwa kuwa mlengwa mkuu kwenye shambulizi hilo ni msichana aliyetajwa kwa jina la Christina, aliyekuwa mchumba wa Munisi, ambaye alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume aliyekuwa akiendesha gari wakati wa tukio hilo.

Kamanda alimtaja mwanamke aliyeuawa katika tukio hilo kuwa ni Alpha Alfred, ambaye ni mfanyakazi wa benki ya Barclays.

Chanzo:- Tanzania Daima

No comments:

 
 
Blogger Templates