SIKU nne tangu Rais Jakaya Kikwete alihutubie Bunge na kuweka bayana msimamo wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Serikali ya Kenya imempongeza huku ikisisitiza kuwa nayo itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alieleza kusikitishwa na hatua ya marais, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni (Uganda) na Paul Kagame wa Rwanda kuanza mazungumzo ya kuitenga Tanzania, lakini akasema kamwe haitaondoka kwenye jumuiya hiyo.
Alisema nchi hizo zimeanza mazungumzo kuhusu ujenzi wa reli na bomba la mafuta, jambo linalovunja misingi ya jumuiya hiyo.
Kufuatia kauli hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, jana alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed.
“Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya yuko nchini, ametumwa na rais wake, Uhuru Kenyatta kuja kutoa pongezi kwa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa bungeni,” alisema Membe.
Kwa mujibu wa Membe, Kenya ilidai kuwa ilifanya hivyo bila kufahamu kwamba nchi hizo zinaibagua Tanzania ambayo ni mwanzilishi wa jumuiya hiyo.
“Tunapongeza hotuba ya Rais Kikwete bungeni na kuahidi kwamba Kenya itaendelea kuwa mwanachama imara wa jumuiya hiyo, atakayelinda misingi imara na taratibu zilizowekwa,” alisema Membe akimkariri Waziri wa Kenya.
Aliongeza kuwa ujumbe huo ulikiri kutokea kwa tatizo hilo, hasa ikizingatiwa kwamba viongozi wa nchi hiyo wamechukua madaraka Aprili 8, mwaka huu.
“Kwa ujumla Kenya inasema ilipotoka kufanya mazungumzo kuhusu mambo ambayo yapo kwenye mkataba bila kuishirikisha Tanzania,” alisema.
Nchi za Uganda na Rwanda bado hazijasema chochote kuhusiana na hotuba hiyo ya Rais Kikwete.
Lipumba aonya
Wakati Kenya ikijirudi, Chama cha Wananchi (CUF) kimeunga mkono msimamo wa Rais Kikwete, lakini kikimtaka vile vile akubali udhaifu uliopo nchini katika usimamizi wa miundombinu mbalimbali ili kuweza kufanya ushindani na kuimarisha uchumi ndani ya jumuiya hiyo.
Alisema kulikuwa na taarifa kuhusu Rwanda na Uganda kutotumia bandari ya Dar es Salaam, na kwamba lisitazamwe kisiasa kutokana na bandari hiyo kuwa na udhaifu mkubwa unaolalamikiwa na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.
“Sio Rwanda na Uganda tu wanalalamika kuhusu bandari hiyo, bali Kongo, Zambia na Malawi pia wanailalamikia kuwa na sifa ya ucheleweshaji wa kupakua shehena za mizigo toka kwenye meli, wizi wa mizigo yakiwemo makontena na vifaa vya magari kama vile taa, redio.
“Uchakachuaji wa mafuta, urasimu na ucheleweshaji wa mizigo kutoka bandarini, ukubwa wa tozo za bandari na barabara na ugumu wa magari ya mizigo kufika na kutoka bandarini, taratibu za utoaji mizigo zisizotabirika na rushwa bandarini,” alisema.
Kwa mujibu wa Lipumba ambaye kitaaluma ni mchumi, asilimia 90 ya biashara yote ya Tanzania na nchi za nje inapita katika bandari ya Dar es Salaam kutokana na nchi sita jirani za Malawi, Zambia, Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda kutokuwa na bandari.
Alisema rais na watendaji wake wanatakiwa kufahamu kuwa bandari ya Dar es Salaam inakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka bandari ya Mombasa inayofanya kazi kwa ufanisi mzuri zaidi na bandari ya Beira, Msumbiji ina ushindani mkubwa kwa mizigo inayokwenda Malawi, Zambia na hata Kongo.
Prof. Lipumba aliongeza kuwa serikali inaelewa wazi kuwa utendaji wa bandari ya Dar es Salaam ni mbaya, usioridhisha, lakini kutokana na ombwe la uongozi imekuwa ikisuasua kufanya mabadiliko ya kuongeza ufanisi.
Alisema uzembe wa utendaji wa bandari unasababisha msongamano ambapo kushusha mizigo kunachukua takribani siku 10 ukilinganisha na ile ya Mombasa inayochukua siku moja .
Pia alisema gharama za tozo Mombasa ni asilimia 22 kwa kila kontena za tozo kwa bandari ya Dar es Salaam ziko juu kwa asilimia 74 ukilinganisha na bandari ya Mombasa.
Pia aligusia utendaji wa Shirika la Reli kuwa umeporomoka ambapo kwa mwaka 2012, shirika lilisafirisha tani 154,000 ukilinganisha na tani 1, 446,000.
“Ikiwa reli ya kati itafanya kazi kwa ufanisi na tija ya hali ya juu, nchi za Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda wanaweza kutumia reli ya kati kusafirisha mizigo yao kwenda na kutoka Dar es Salaam.
“Reli ya Tazara haijatumiwa kwa kadiri ya uwezo wake. Mwaka 2012 ilisafirisha mizigo tani 259,000 ukilinganisha na tani 677,000 kwa mwaka 2002. Kwa kawaida usafiri wa reli ni wa gharama za chini ukilinganisha na usafiri wa barabara, tuna wajibu wa kuimarisha utendaji wa Shirika la Tazara ili kuongeza ushindani wa kibiashara na kukuza uchumi wetu,” alisema.
Chanzo :- Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment