MAONI ya wasomaji wa makala yangu ya wiki iliyopita, iliyokuwa imebeba kichwa cha habari; Tatizo la CCM ni Kikwete mwenyewe, yamenilazimisha kuendeleza mjadala huo katika sehemu hii ya pili, kutokana na mchango wa mawazo wa baadhi ya wasomaji wangu hao juu ya hatima ya Tanzania yetu nje ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Makala yangu ya wiki iliyopita niliiandika, nikikosoa tabia ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, kuogopa kutimiza wajibu wake wa kiuongozi kwa sababu tu ya kukwepa kulaumiwa na hasa pale alipowaambia watendaji wa chama chake kule Dodoma kwamba kwa nafasi yake ya urais, anapata taarifa za vitendo vyao vya rushwa na kiasi halisi cha rushwa wanachotumiwa na wasaka madaraka ndani ya chama chake.
Hata hivyo, pamoja na Mwenyekiti Kikwete kuwatambua mawakala wa rushwa na kiasi cha rushwa kinachotolewa, nilisema ameishia kulalamika tu huku akiwasukumia wengine, kina Philip Mangula na Abdulrahman Kinana wawashughulikie watovu hao wa nidhamu kwa niaba yake, kwa sababu tu anaogopa kulaumiwa.
Nilihitimisha makala yangu hiyo ya wiki iliyopita kwa kumshauri Mwenyekiti Kikwete kwamba ndiye wa kuiponya CCM dhidi ya dhoruba inayokuja 2015, kwa kuachana na tabia yake ya kukwepa kulaumiwa.
Nilisema ni bora Mwenyekiti Kikwete akubali kulaumiwa leo na hao watendaji wake mawakala wa rushwa kuliko lawama atakazozipata pale CCM itakapomfia mikononi mwake, baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Nilihitimisha hivyo kwa kuzingatia msingi mmoja kwamba Makamu wa Mwenyekiti wa CCM (Bara), Mangula, ambaye amekabidhiwa rungu na Mwenyekiti Kikwete kuwashughulikia wanaoshiriki vitendo vya rushwa, mmoja baada ya mwingine, pamoja na majukumu yake mengine, yeye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya CCM, chombo chenye jukumu la kuwashughulikia hao watoaji na wapokeaji rushwa ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, kwa kanuni za CCM, Kamati ya Maadili haina mamlaka yoyote ya kuadhibu. Kazi yake, ni kusimamia maadili ya Chama, kwa kufungua jalada lenye orodha ya tuhuma, kabla ya mtuhumiwa kuitwa mbele ya kamati hiyo kwa mahojiano na utetezi.
Hata kama katika mahojiano utapatikana ushahidi wa kumtia hatiani mtuhumiwa, Kamati ya Maadili haina mamlaka ya kutoa adhabu, zaidi ya kupeleka madhambi ya mhusika kwenye vikao vya juu vya uamuzi, yaani Kamati Kuu na Halmashauri Kuu (NEC).
Katika vikao hivyo, inategemea mtuhumiwa amejipanga vipi. Kama hakujipanga sawa sawa na hivyo kukosa asilimia kubwa ya watetezi, adhabu itamwangukia. Lakini kama amejipanga vizuri na kupata watetezi wengi, atapeta tu!
Kwa hiyo, utendaji kazi wa Kamati ya Maadili ya Mangula, ni tofauti na utendaji kazi ya Mwenyekiti wa CCM kama taasisi. Mwenyekiti wa CCM anayo mamlaka ya moja kwa moja, kwanza; kama kiongozi mkuu wa Chama na msimamizi mkuu wa maadili ya Chama, na pili; kama mkuu wa Serikali.
Mwenyekiti wa CCM, anazo mamlaka mbili kuu anazoweza kuzitumia kukomesha vitendo vya rushwa ndani ya Chama chake na ndani ya serikali yake, bila kuhojiwa na yeyote, bila kukwazwa na kanuni wala sheria yoyote ya chama chake, wala ya nchi.
Mwenyekiti Kikwete anafahamu hili, lakini woga wa kulaumiwa ndilo tatizo lake kuu. Ndiyo maana, wenye imani na CCM juu ya hatima ya uongozi wa nchi hii, hawaishi kumwambia ukweli kwamba kama ataendelea na tabia ya woga wake huo, basi asubiri jahazi la CCM limzamie mikononi mwake!
Msomaji wangu mmoja kati ya wengi waliopongeza na kutoa ushauri kwa makala yangu iliyopita, ambaye bila shaka ni kiongozi au mwanachama wa CCM kutokana na picha ninayoipata kutokana na ujumbe wake huu kwangu, ameandika hivi:
“Umesema kweli kiongozi, hebu mwangalie Nape (Nape Moses Mnauye) na waliomzunguka. Angalia waliomo ndani ya UVCCM ya sasa, UWT ya sasa na Wazazi. Je, wanaweza kumvutia nani kwa hoja? Kweli tuendako ni kugumu!”
Nimkaribishe Mwenyekiti wa CCM, Katibu wa CCM, watendaji wote na wanachama wa chama hicho, tutafakari kwa pamoja mantiki iliyomo ndani ya ujumbe mfupi huo wa msomaji wangu kwa kujibu swali lake hilo.
Wanaomzunguka Nape ni sekretarieti ya Kamati Kuu ya CCM. Waliomo ndani ya UVCCM, UWT na Wazazi, wanajulikana. Je, wanaweza kumvutia Mtanzania gani kwa hoja, ili Mtanzania huyo aliyekata tamaa na chama hiki, arejeshe matumaini yake upya?
Tuanze na Nape. Mwanasiasa huyu kijana amejipambanua kama mpambanaji wa ufisadi ndani ya CCM. Lakini, inajulikana wazi mafisadi wana nguvu kubwa ndani ya chama hicho na kwa kifupi, ni kama wanakimiliki chama kwa asilimia zaidi 60.
Je, ni sahihi kwa CCM kuendelea kuwa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, ambaye ndani ya chama chake anapingwa, hapendwi na watendaji, wanachama na wafuasi wa chama zaidi ya asilimia 60 wanaofaidika na vitendo vya kifisadi, kwa maana kwamba nafasi zao walizipata na wanaendelea kuwa nazo kutokana na nguvu za ufisadi?
Kwa nini nafasi hiyo asipewe mtu asiye na upande wowote (neutral), anayeweza kuyaunganisha makundi yote mawili ya wapinga vitendo vya ufisadi na wabariki vitendo vya ufisadi?
Nahoji hili kwa sababu, ili CCM iwe na uhakika wa kuendelea kutawala nchi hii kunako majaliwa mwaka 2015 au mwaka 2020, ni ama kiamue kwa nguvu moja kuwatosa mafisadi au kiamue kwa nguvu moja kujikabidhi moja kwa moja mikononi mwa mafisadi.
Kwa kufanya hivyo, mwaka 2015 CCM itatarajia kupata ushindi ama utakaotokana na uadilifu wake au utakaotokana na nguvu ya ukwasi wa fedha za mafisadi zitakazotumika kuwanunua wapiga kura kama ilivyotokea mwaka 2005.
CCM Taifa, inatambua kwamba wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Kuu ya CCM, wamegawanyika katika mtazamo huo wa kukomesha vitendo vya ufisadi ndani ya chama hicho. CCM Taifa, inafahamu kwamba baadhi ya wajumbe wa sekretarieti hawawezi kuombana maji ya kunywa kwenye glasi, lakini Chama kiko kimya utadhani hilo si tatizo la kichama, si tatizo la kiuongozi.
Hali ya mgongano na msigano uliomo ndani ya Sekretarieti ya Kamati Kuu ya CCM, ndivyo ilivyo hata ndani ya Kamati za Utekelezaji Taifa za UVCCM, UWT na Wazazi.
Baadhi ya watendaji katika mabaraza ya utekelezaji ya Jumuiya hizo, si waaminifu na watiifu kwa chama chao na viongozi wao wa kitaifa, bali ni waaminifu na watiifu kwa waliowapigania kupata nafasi hizo, ili huko mbele ya safari nao walipe fadhila kwa kuhakikisha wanapata madaraka wanayoyataka.
Chanzo:- Raia Mwema
No comments:
Post a Comment