Social Icons

Tuesday, 12 November 2013

WINNIE MANDELA NA TUHUMA ZA MAUAJI YA KUTISHA 2

WINNIE alikanusha kuhusika na vitendo hivyo na kuomba asilaumiwe kwa makosa hayo. Katika hali iliyotafsiriwa kuwa ya kiburi akasema; “...hawa watu, yote waliyosema dhidi yangu ni ujinga mtupu.”

Winnie alikuwa akizungumzia tuhuma zilizotolewa dhidi yake na mmoja wa wanachama wa kundi lake lililokuwa likijulikana kwa jina la Mandela United Football Club.

Jerry Musivuzi Richardson "The Coach"Mmoja wa wanachama wa Mandela United Football Club, Jerry Musivuzi Richardson, maarufu kwa jina la The Coach, ndiye alivunja ukimya dhidi ya Winnie.

Kwa mujibu wa The Coach, Winnie ndiye aliyekuwa akiwaagiza kuwateka nyara na kuwatesa raia waliohisi ni mashushushu waliokuwa wakitumiwa na polisi kumchunguza yeye na kundi lake.

The Coach naye alikuwa akidaiwa kushiriki mauaji ya kijana wa miaka 14, mwanaharakati wa kupinga ubaguzi, Stompie Seipei mwaka 1989. Tayari The Coach alikwishahukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la mauaji ya Stompie Seipei.

Akiwa amesimama mbele ya Tume ya Maridhiano, wiki chache zilizopita kabla Winnie Mandela kuitwa katika tume hiyo, The Coach  alijikuta akitokwa machozi wakati akisimulia.

“Nilimuua Stompie kwa maelekezo ya Mummy (jina walilokuwa wakimuita Winnie Mandela). Hakuwahi kuuwa mtu yeyote, lakini alikuwa akitupa maelekezo ya kuuwa na tuliuwa watu wengi sana,” alisimulia Richardson au The Coach.

Stompie SeipeiAkieleza jinsi alivyomuua Stompie kwa kumchinja kama mbuzi, Richardson alisema; “Mikono yangu imelowa damu kutokana na mauaji tuliyoyafanya. Vitendo tulivyovifanya chini ya mwavuli wa Mandela United Football Club vilikuwa ni vya kutisha na vya kishenzi.”

Hata hivyo ushahidi wa Richardson ulitofautiana na shahidi mwingine, Katiza Cebekhulu. Akitoa ushahidi wake mbele ya tume hiyo, Cebekhulu alidai kwamba, Winnie alishiriki katika kumuua Stompie na si kwamba aliagiza tu Stompie auawe.

Huku akimnyooshea kidole Winnie, Cebekhulu alisema: “Nilimuona akimuuwa Stompie.”

Cebekhulu aliendelea kumtuhumu Winnie kwamba pia alishiriki katika mauaji ya mganga mmoja Abu-Baker Asvat, ambaye ndiye aliyeufanyia mwili wa Stompie uchunguzi.

Cebekhulu pia alidai kwamba, hata yeye alitekwa nyara na wanachama wa ANC (The African National Congress- chama ambacho Mzee Nelson Mandela alikuwa ndiye kiongozi wake), akasafirishwa na kwenda kufungwa nchini Zambia ili kumzuia asitoe ushahidi dhidi ya Winnie Mandela kuhusu mauaji ya Stompie.

Hata hivyo ushahidi wa Cebekhulu ulishabihiana na ushahidi uliotolewa na Thulani Dlamini, ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 25 jela kwa kuhusika katika mauaji ya Mganga Asvat.

Dlamini aliiambia tume hiyo ya maridhiano kwamba, alikodishwa kwa mkataba ili kutekeleza mauaji hayo ya Mganga Asvat, na makubaliano hayo yalifanywa baina yake na Winnie Mandela nyumbani kwake.

“Huyu mwanamke alituambia, iwapo tutatekeleza mauaji hayo (ya kumuua Mganga Asvat) atatulipa Dola za Marekani 4,115, pia alitaka kujua kama tunazo taarifa sahihi zinazomhusu mganga huyo,” alidai Dlamini.

Pamoja na Winnie Mandela kukanusha tuhuma hizo, lakini mwanachama mwingine wa kundi lake hilo la Mandela  United Football Club, Gift Ntombeni alidai kwamba, alishiriki katika kuwapiga na kuwatesa watu watano nyumbani kwa Winnie katika kitongoji cha Soweto.

Ntombeni aliendelea kuiambia tume hiyo ya maridhiano kwamba, wakati fulani, Winnie Mandela alimtuhumu kuwa ni shushushu anayetumiwa na polisi wa serikali ya makaburu  kutoa siri zao na hivyo akamuagiza mmoja wa watu wake ambaye alikuwa ni rafikiye, amuuwe.

Hata hivyo rafikiye huyo alimweleza kuhusu maagizo aliyopewa ya kumuua hivyo alimtaka atoweke, akajifiche. Ntombeni pia alikiri kumuona Winnie katika moja ya matukio ya mauaji yaliyofanywa na kundi lake (hakufafanua yalikuwa ni mauaji ya nani) na pia alidai kumuona akishiriki katika matukio mengi ya kuwapiga na kuwatesa watu mbalimbali walioonekana kuwa na uhusiano na polisi wa makaburu au kwenda kinyume cha maagizo yake.

“Winnie ni mwanamke jasiri, alikuwa na uwezo wa kufanya chochote,” alisema Ntombeni akimsifu mama huyo.

Winnie Mandela ambaye awali kutokana na sifa alizojijengea za uanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi nchini humo, alipewa jina la Mama wa Taifa (Mother of National), lakini baada ya kuitwa katika tume hiyo na kutuhumiwa kuhusika na vitendo vya utekaji nyara, utesaji na mauaji ya watu wake mwenyewe na kutoonyesha hali yoyote ya kujutia makosa yake, watu walibadili jina hilo la Mama wa Taifa na kumwita Jambazi la Taifa (Mugger of the National).

Katiza CebekhuluNi mara chache alionekana akitikisa kichwa kwa ishara ya kupinga kinachosemwa dhidi yake mbele ya tume hiyo au kuonyesha hali ya kutoamini kile kinachosemwa dhidi yake. Akiwa amekaa mbele ya bango kubwa lililokuwa na maandishi yanayosomeka; “Truth Hurts-Violence Kills,” Winnie aliuelezea ushahidi wa Richardson kama  wa “kipuuzi na wa kiwendewazimu,” na pia aliuelezea ushahidi wa Cebekhulu kuwa “umetengenezwa na mgonjwa wa akili.”

Pia alikanusha tuhuma nyingine zilizoelekezwa kwake kwa kudai kwamba ni sehemu ya, “taarifa zisizo sahihi na kampeni iliyoandaliwa mahsusi na utawala uliopita wa kibaguzi” ili umchafue yeye binafsi na chama chake cha ANC.

Akipinga kujibu maswali yaliyoelekezwa kwake na mmoja wa wanasheria wa tume hiyo Hanif Vally, Winnie Mandela alihamaki akisema; “Siweza kuvumilia, jinsi unavyoongea nami.”

Kuna wakati pia alionekana kupatwa hasira katika hizo siku tisa alipokuwa akihojiwa na tume hiyo.

Nje ya ukumbi uliokuwa ukitumiwa na tume hiyo, aliulizwa na waandishi wa habari wakati akitoka kwamba hadhani kuwa anaweza kushitakiwa kwa kosa la kuhusika na mauaji ya Stompie Seipei? Lakini Winnie alijibu swali hilo kwa hamaki; “Huo utakuwa ni upumbavu.”

Ili kukanusha tuhuma hizo dhidi yake, Winnie aliandaa mashahidi kadhaa ili kumsaidia kupinga tuhuma zilizoelekezwa kwake. Wafuasi wake hao waliieleza tume hiyo jinsi mama huyo alivyokuwa shujaa kwa kupambana na utawala wa kibaguzi kwa muda mrefu, bila kutetereka na juhudi zake za muda mrefu za kuhakikisha jamii ya wananchi masikini wa Afrika Kusini inapata maisha mazuri.

“Winnie hakuwa mbaya ukilinganisha na vitendo vilivyofanywa na wazungu ambao waliua watoto wengi weusi wakati wa utawala wao wa kibaguzi,” alisema Gift Mbatha, muuza bidhaa dukani katika viunga vya Soweto.

Hata hivyo tume hiyo ya ukweli na maridhiano ilikuwa na shaka kidogo kuhusu maelezo ya Winnie, kwamba, kuna kitu anachokificha.

“Tumesikia uongo. Nusu uongo, nusu ukweli, katika yote aliyozungumza,” alisema Alex Boraine, aliyekuwa Mwenyekiti Msaidizi wa tume hiyo. Aliendelea kusema kwamba, uamuzi wa mwisho ya tume hiyo dhidi ya Winnie Mandela hautatangazwa mpaka mwaka 1998, wakati ripoti ya tume hiyo itakapokabidhiwa kwa Rais Mandela.

Alex Boraine aliongeza kwa kusema kwamba, tume hiyo ya ukweli na maridhiano haina mamlaka ya kisheria kumfungulia mtu mashitaka, lakini kukifichuliwa ushahidi mpya dhidi ya Winnie Mandela, tume hiyo ina uwezo wa kufikisha ushahidi huo kwa mwanasheria mkuu wa serikali kwa hatua zaidi.

Pamoja na kukanusha tuhuma zote, Winnie alijiweka katika nafasi finyu ya kupata kinga ya kushitakiwa kama walivyofanyiwa watu wote waliojitokeza katika tume hiyo ya maridhiano na kutoa ushahidi wao.

Baada ya kumalizika kusikilizwa kwa tuhuma dhidi yake, aliyekuwa kamanda wa polisi nchini humo, George Fivaz aliahidi kuanza uchunguzi upya wa watu walioripotiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha huku jina la Winnie lilitajwa kuhusika.

Mpaka kumalizika kusikilizwa kwa tuhuma dhidi yake, Winnie Mandela aliendelea kuwa maarufu na kujikusanyia mashabiki na wafuasi wengi katika maeneo yanayokaliwa na watu weusi nchini humo.


Chanzo:- Raia Mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates