NAKUMBUKA vema kana kwamba ilitokea jana tu. Takribani miaka kumi iliyopita, kijana mmoja mwembamba alisimama katika mojawapo ya kumbi zilizopo ndani ya viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam. Alikuwa akiomba nafasi ya kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la CHADEMA.
Baadaye aliniambia kwamba hadi wakati ule hakuwahi kuvaa suti maishani mwake. Suti kwake ilikuwa ishara ya ubepari. Watu aliokuwa akiwapenda wakati akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM); Profesa Chachage Seith Chachage, Profesa Issa Shivji na Dk. Azaveli Feza Lwaitama hawakuwa wapenzi wa suti.
Lakini kwenye siku hiyo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alijitolea kununua suti mpya ili walau kijana wake huyo kipenzi wakati huo aonekane vema mbele ya wajumbe.
Kijana huyo akaja baadaye kupata ujumbe wa Baraza Kuu. Baadaye, akifanya kazi kwa karibu sana na Mbowe, alipanda ngazi hadi kufikia kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho. CHADEMA haikuwahi kuwa na kijana mdogo namna ile kwenye nafasi kubwa namna hiyo.
Kijana huyo ndiye huyu Zitto Kabwe ambaye leo hii yuko kwenye mgogoro mzito na chama hicho ambacho alijiunga nacho tangu akiwa na umri mchanga wa miaka 16.
Unaweza kudhani kwamba pengine ujumbe huo na unaibu ndiyo pengine matukio yaliyombadilisha Zitto na kumfanya afikie alipo leo. Hapana, mwanasiasa huyu alianza kupata heshima kutokana na tukio moja la kihistoria.
E pluribus unum ya Zitto
Neno hili la kilatini linatumika kwa maana nyingi. Katika ngao ya Serikali ya Marekani maandishi haya humaanisha “Mmoja Kutoka Katika Wengi” kwamba taifa hilo limeundwa na muunganiko wa majimbo mengi.
Hata hivyo, maana ninayoipenda zaidi ni ile nyingine, inayozungumzia tukio au wakati mmoja katika maisha ya mtu ambayo hubadilisha maisha yake.
Kwa mfano, E pluribus unum ya Rais Jakaya Kikwete ilikuwa ni wakati ule alipoamua kwenda kufanya kazi katika chama badala ya kutafuta ajira serikali ilhali tayari akiwa msomi wa shahada ya kwanza katika kipindi ambacho wasomi walikuwa haba.
Leo hii, Kikwete amepanda na kufanikiwa kuwa rais kwa sababu ya maamuzi aliyoyafanya wakati huo.
Kwa Zitto, E pluribus unum yake ni hoja ya Buzwagi. Julai mwaka 2007, Mbunge huyu wa Kigoma Kaskazini alihoji sababu za aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, kwenda kusaini mkataba mpya wa mgodi wa Buzwagi katika kipindi ambacho taifa lilikuwa likifanya mapitio ya sheria zake.
Hoja hii ilizua mjadala mkali ambao ulidakwa na taifa zima. Tangu hapo, Zitto akawa ameingia katika nyoyo za Watanzania na kuanzia hapo, hoja zake nyingi zikawa zinafuatiliwa kwa makini na wahusika.
Kuanzia hapo ameibuka na masuala mbalimbali ambayo yameibua mijadala mingi ya kitaifa. Alikwenda kinyume na msimamo wa chama chake baada ya kukubali kuingia kwenye Tume ya Madini iliyoteuliwa na Kikwete na ambayo imeleta mabadiliko makubwa katika sekta ya madini hapa nchini.
Yeye ndiye mtoa hoja ya kusaka mali na fedha zilizofichwa nje ya nchi, mtoa hoja ya kutokuwa na imani na serikali iliyosababisha kufanyika kwa mabadiliko katika Baraza la Mawaziri na sasa anashiriki sana katika kutafuta haki kwa nchi masikini kwenye masuala ya ukwepaji kodi wa makampuni makubwa.
Mgogoro wake mkubwa kabisa na chama chake ulikuja mwaka 2009 wakati alipotangaza nia ya kutaka kuwania uenyekiti wa chama hicho dhidi ya Mbowe. Nia yake hiyo ndiyo msingi wa matatizo yake yote yanayomkuta sasa ndani ya chama chake.
Wakosoaji wake wanasema kosa la kwanza la Zitto kisiasa lilikuwa ni kuwania uenyekiti na Mbowe ambaye ni mtu aliyemlea ndani ya chama. Uamuzi huo wa Zitto umemletea madhara kwa sababu umempotezea marafiki ambao walifukuzwa kwa kumuunga mkono lakini pia kupoteza sapoti ya Mbowe. Hii ni kasoro ya kutokuwa na subira.
Katika miaka ya nyuma, Zitto angeweza kufanya chochote na asihofu kwa vile alijua Mbowe angemtetea. Lakini, kwa uamuzi wake huo, akawa amekata kamba iliyokuwa ikimuunganisha na bosi wake huyo chamani.
Kama angeweza kusubiri kidogo pengine hadi wakati huu, huenda Zitto angeweza kupata uenyekiti pasipo kutumia nguvu nyingi na kuwa si Mwenyekiti wa chama hicho pekee, bali pia mwanasiasa wa upinzani mwenye nguvu kuliko mwingine yeyote kimamlaka hapa nchini.
Pia, tofauti na wanasiasa wengi wa upinzani hapa nchini, Zitto ana mahusiano ya karibu na baadhi ya viongozi wa juu wa CCM, serikali na vyombo vya dola na hivyo amekuwa mwathirika wa mara kwa mara wa tuhuma za kutumiwa na taasisi hizo.
Hata hivyo, kwa jicho lingine, hii pia inaweza kuelezwa kama mojawapo ya nguvu za mwanasiasa huyu.
Dk. Slaa na orodha ya mafisadi
Huyu ni miongoni mwa wabunge walioingia bungeni katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 akipitia jimbo la kwao Karatu. Hakuwa maarufu sana kwenye miaka ya 1990 na watetezi wake wanasema utawala wa kiimla wa aliyekuwa Spika wa Bunge, Pius Msekwa, ulichangia zaidi hali hiyo.
Kwa upande wake, E pluribus unum yake ilitokea siku moja ya Septemba 15, mwaka 2007 katika viwanja vya Mwembeyanga vilivyopo wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam pale alipotangaza iliyokuja kufahamika sana kama “Orodha ya Mafisadi.”
Habari hiyo ilipata sapoti kubwa kutoka kwenye vyombo vya habari kwani, kwa mara ya kwanza katika historia ya siasa za Tanzania, vyama vya upinzani vilitaja hadharani majina ya watu wanaotajwa kuwa vinara wa rushwa hapa nchini.
Mafisadi hao walikuwa muhimu kipindi hicho kwani tayari CHADEMA ilikuwa imeanza kujenga hoja kama chama kuhusu upotevu wa mabilioni ya shilingi katika iliyokuwa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Katika Bunge lililopita chini ya Spika Samuel Sitta, Slaa alijipambanua kama mmoja wa wapinga ufisadi na nafasi yake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, ulimpa fursa ya kuibua ufisadi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Akiwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk. Slaa alikuwa kivutio kwa wengi kutokana na tabia yake ya kupenda kuzungumza kwa kutumia takwimu na kuongoza chama ambacho kilikuwa kinaonyesha ujana, staili na mawazo ya mbali kisiasa.
Wapo wanaoamini kwamba CHADEMA kilipata wabunge wengi kuliko katika wakati mwingine wowote tangu kianzishwe kutokana na mvuto au ufuasi aliokuwa nao mgombea huyo kwa wananchi.
Kuna kipindi, kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2011, Dk. Slaa alikuwa ndiye mwanasiasa mwenye ushawishi zaidi ndani ya chama hicho kuliko mwingine yeyote.
Hata hivyo, kwa sababu mbalimbali, umaarufu wa Dk. Slaa umeshuka katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu hadi miwili iliyopita. Kutokuwepo kwake ndani ya Bunge kumeondoa eneo lake moja muhimu la kujieleza.
Wakosoaji wa Slaa wanaeleza kwamba amekuwa na tatizo la kutotaka kushaurika na pia mara nyingi si mtu wa kuonekana kwenye matukio makubwa ambayo huwa yanawasaidia wanasiasa kuonekana.
Mfano unaotolewa mara kwa mara ni kukosekana kwake hivi karibuni katika tukio la kuaga mwili wa marehemu Dk. Sengondo Mvungi lililofanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam –tukio lililohudhuriwa na watu wengine maarufu kutokana na umaarufu wa marehemu.
Kwamba kama hana hoja ya kuzungumza, ni rahisi sana kwa Slaa kupotea kwenye jamii kwa vile si mtu anayependa kujichanganya. Tabia hii, wanasema, watu wanaomfahamu kwa karibu, pengine inatokana zaidi na malezi yake kilei aliyoyapata wakati akiwa padre wa Kanisa Katoliki.
Wanasiasa mahiri hutafuta njia za kuonekana mara kwa mara ili wasipotee. Rais Kikwete anaweza asiwe na habari kubwa ya kufanya lakini anaweza kuonekana akiwa msibani, mpirani, mkutanoni na au safarini. Ni sanaa ambayo Dk. Slaa ameshindwa kuimanya.
Freeman Mbowe
CHADEMA hii inayoonekana leo ina mkono wa Mbowe katika eneo zaidi ya moja. Katika wakati wake, CHADEMA imepata mafanikio makubwa ambayo wengine hawayakuwazia wakati alipopewa madaraka.
Mbowe alipokea uenyekiti wa CHADEMA wakati chama kikiwa na wabunge wasiozidi watano na kikiwa na kila dalili ya uchovu. Aliyemwachia madaraka alikuwa ni Bob Nyanga Makani aliyewahi kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania ambaye naye alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Edwin Mtei, aliyewahi kuwa Gavana wa BoT.
Ingawa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, tayari alikuwa ameonyesha kuvutiwa na sera za CHADEMA, lakini kilionekana ni chama cha wastaafu, wasiotaka ugomvi na serikali na wasio na shida. Matajiri. Yote yakabadilishwa na Mbowe.
Kubwa kuliko yote ambalo Mbowe amelifanya kwa CHADEMA ni namna alivyoweza kuwaamini vijana na kuwapa majukumu mazito.
Huwezi kutaja vijana kama Zitto, John Mnyika, John Mrema, Halima Mdee, David Kafulila na Muhonga Said Ruhwanya pasipo kutaja mchango.
Hata kama vijana hawa wana akili za kutosha vichwani mwao, walihitaji fursa kuweza kuonyesha umahiri na ni Mbowe pekee, miongoni mwa viongozi wa vyama vyote vya siasa nchini, ndiye aliyeweza kucheza kamari na vijana na amevuna matunda ya uamuzi wake huo.
Kwa sasa, CHADEMA, pengine, ndiyo chama kinachoweza kujivunia kama tumaini la vijana wengi hapa nchini ambao wanaamini watapata fursa endapo tu watajiunga au kujihusisha na chama hicho.
Freeman pia ni miongoni mwa wanasiasa ambao wamejaaliwa uwezo mzuri wa kuzungumza kwenya majukwaa ya kisiasa.
Ni wanasiasa wachache hapa nchini wenye uwezo wa kushindana naye pindi anapopanda kuzungumza na wananchi.
Ni Mbowe huyuhuyu ambaye utaratibu wake wa kutumia helikopta wakati wa kampeni za uchaguzi umebadili kabisa namna ya ufanyaji wa kampeni. Sasa karibu vyama vyote vimeona umuhimu wa kutumia chombo hicho katika kampeni zake.
Pia, CHADEMA ni chama pekee nchini ambacho kina ubunifu wake wa mavazi na hili pia linahusishwa naye kwa vile limetokea chini ya utawala wake.
Hata hivyo, wakosoaji wa Mbowe wanataja kasoro zake kubwa mbili. Mosi ni ile ya kutokuwa na uwezo wa kuibua hoja binafsi zitakazomtambulisha yeye binafsi. Wakati Slaa anaweza kujigamba kwa mambo ya EPA na Orodha ya Mafisadi, huku Zitto akijitapa kwa Buzwagi na mabilioni ya Uswisi, Mwenyekiti huyu hadi sasa hana hoja ya binafsi anayoweza kuisimamia kwamba ni yake.
Matokeo yake ni kwamba amekuwa mwanasiasa wa matukio. Jina la Mbowe limekuwa likitajwa sana kwenye matukio ya fujo, purukushani za kisiasa na mikutano ya kisiasa bila ya kuwa na hoja anayoisimamia.
Kasoro ya pili imetajwa kuwa ni tabia yake ya kuhofia upinzani kutoka ndani ya chama chake au jimboni. Wakosoaji wake wanasema hata tofauti zake na Zitto zimesababishwa zaidi na kilichotokea mwaka 2009 kuliko kitu kingine chochote.
Watetezi wake wanasema tabia hii huenda inatokana na ukweli anatoka katika familia ya kitajiri na hivyo ubongo wake umetengenezewa dhana ya kumiliki na ndiyo maana si rahisi kwake kuvumilia upinzani.
Huo ndiyo utatu wenye utata ulio kwenye CHADEMA.
Chanzo:- Raia Mwema
No comments:
Post a Comment