Social Icons

Thursday, 28 November 2013

CHADEMA SIKIO LA KUFA?

WAKATI mazingira ya mgogoro uliopo ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kusimamishwa uongozi kwa Naibu Katibu Mkuu wake, Kabwe Zitto na mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo yakielekeza umma kujiuliza kama chama hicho ni sikio la kufa kwa sasa, vyama vitatu vya siasa hapa nchini vimemkaribisha mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA),  Zitto (pichani kushoto), kujiunga navyo endapo atafukuzwa katika chama chake cha sasa, Raia Mwema linafahamu.

Taarifa hii mpya inakuja katika kipindi ambacho chama hicho kikuu cha upinzani nchini kikiwa, labda, katika mgogoro mkubwa zaidi kuwahi kukikuta tangu kilipoanzishwa miaka 20 iliyopita.

Gazeti hili limezungumza na baadhi ya viongozi wa vyama hivyo na wamethibitisha kwamba wako tayari kumpokea mwanasiasa huyo, endapo chama chake kitamfukuza kama dalili zinavyoonyesha kwa sasa.

Kamati Kuu ya CHADEMA imempa Zitto na mjumbe wa kamati hiyo, Dk. Kitila Mkumbo, muda wa siku 14 kuanzia Ijumaa iliyopita wajieleze kwa nini wasifukuzwe kutoka kwenye chama hicho kutokana na kutuhumiwa kufanya uhaini.

Vyama ambavyo gazeti hili linafahamu kuwa viko tayari kumpokea Zitto ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama Cha Wananchi (CUF) na chama cha NCCR-Mageuzi; ambavyo pia ndiyo vyama vinara kwa siasa za hapa nchini, kama ilivyo kwa CHADEMA.

Ingawa jitihada hizo hazijawa rasmi, haswa kwa upande wa upinzani kwa sababu ya heshima baina ya vyama husika, angalau baadhi ya viongozi wamekuwa wazi na kueleza kwamba suala hilo lipo hata kama halijatangazwa.

Kiongozi wa kwanza wa kisiasa kutoa kauli baada ya hatua ya CHADEMA kumvua Zitto na Kitila vyeo vyao vyote vya kisiasa walivyokuwa navyo ndani ya chama chao alikuwa ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba.

Akiandika katika mitandao mbalimbali ya kijamii, Mwigulu alieleza kwamba kilichomkuta Zitto na Kitila ni matunda ya kuwemo katika chama ambacho hakiendani na kaliba yao kwa sasa.

“Kwenye CHADEMA, wale wote wenye akili wako nje ya uzio wa chemichemi ya mawazo. Mfano ni bungeni, wana CHADEMA waliowahi kufundisha vyuoni hawapewi hata unaibu waziri kivuli kwa kuwa wanatumia zaidi akili badala ya nguvu.

“Lakini, walioishia kidato cha kwanza, pili, tatu na sifuri ndiyo majembe ya chama wanaopewa fursa zote kwa kuwa wao badala ya kutumia akili wanatumia nguvu na mabavu.

“Nawafahamu Zitto na Kitila tangu nikiwa Chuo Kikuu na nawajua kama watu mahiri wanaoweza kutoa mchango popote,” aliandika Mwigulu.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Mwigulu ni tofauti kwa kiasi kikubwa na michango yake bungeni kila anapokosoa hotuba ya bajeti kutoka kwa Wizara (kivuli) ya Fedha inayoongozwa na Zitto, akiamini imekuwa ikifanywa bila umahiri wa kutosha.

Katika mazungumzo na gazeti hili wiki hii, Mwigulu alisema “Sisi hatuna tatizo na Zitto. CCM ni chama cha Watanzania wote kisichobagua watu kwa kutumia dhana za ukanda, udini wala ukabila.

Akitaka kuja, anakaribishwa kwa mikono miwili,” alisema Mwigulu.

Kwa upande wa CUF, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Julius Mtatiro, alisema wanafuatilia kwa karibu kila kinachoendelea ndani ya CHADEMA kwa vile ni chama mwenza katika upinzani na lolote linalotokea litakuwa na athari katika ulingo wa kisiasa hapa nchini.

“Sitakuwa nasema ukweli kama nikisema CUF haimuhitaji Zitto, Kitila au mwanasiasa yeyote mahiri kutoka chama chochote cha siasa hapa nchini.

Hata hivyo, si vizuri pia kwangu kusema tunamtaka mwanachama wa chama kingine maana hilo linaweza kumaanisha tunachochea machafuko,” alisema Mtatiro.

Hata hivyo, Raia Mwema linafahamu kwamba baadhi ya viongozi wa juu wa CUF walikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kutafuta mawasiliano na Zitto mara baada ya kuvuja kwa taarifa za mwanasiasa huyo kuvuliwa madaraka.

Mmoja wa viongozi wa juu wa CUF aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema kama Zitto atahamia katika chama chao, watakuwa wamepata kitu kimoja tu ambacho walikuwa wakikikosa kwa muda mwingi.

“Unajua CUF Zanzibar wana Maalim Seif. Watu wanapenda sana chama chao lakini pia wana mtu ambaye wanampenda na anakiwakilisha vizuri. Mwenyekiti (Profesa Ibrahim Lipumba), amefanya kazi nzuri lakini haonekani kama anaweza kuongeza idadi ya wanachama na wapenzi wa CUF. Hana ule mvuto kama wa Maalim au alionao Zitto.

“Tunachohitaji ni mtu mmoja ambaye anaweza kuleta wanachama wapya na msukumo mpya kwenye chama.

“Bila shaka, Zitto anaweza kuleta hilo na ndiyo maana atakaribishwa kwa mikono miwili. Hata kama atatoa masharti ya kupewa cheo fulani, hilo litawezekana pia,” alisema kiongozi huyo.

Akizungumzia suala la Zitto, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema binafsi hawezi kuwa na tatizo iwapo mwanasiasa huyo ataamua kuhamia kwenye chama chake ingawa alisema hajafanya mazungumzo na mbunge mwenzake huyo kuhusu kuhamia chama chake.

Mimi kama James, sijazungumza na Zitto kumshawishi ahamie NCCR. Hata hivyo, NCCR si James Mbatia, ni taasisi ambayo ina watu wengi. Kama umesikia kuwa chama changu kinamtaka basi inawezekana juhudi hizo akawa amefanya mtu mwingine lakini si mimi,” alisema.

Kama ilivyo CHADEMA kwa sasa, NCCR kiliwahi kuwa chama kikuu cha upinzani hapa nchini lakini kikakumbwa na migogoro iliyosababisha kushuka umaarufu wake ingawa sasa Mbatia anakijenga upya.

Mbatia alizungumzia pia mgogoro wa CHADEMA na kusema kutokana na uzoefu wa NCCR, anaamini kwamba namna pekee ya kushughulika na migogoro ni kuzungumzia kuhusu hoja na si watu binafsi na badala ya kutumia sana Katiba na sheria, viongozi watumie zaidi hekima na busara.

“Migogoro inaweza ikakijenga chama kama watu wataichukulia kwa njia chanya. Kama unapokea vibaya kutofautiana, lazima kutakuwa na matatizo. Jambo la msingi kwa CHADEMA kwa sasa ni kujibu hoja zilizotolewa na Zitto na si kumshughulikia yeye na mwenzake,” alisema Mbatia.

Hoja ya Zitto kuhamia NCCR inachochewa pia na ukweli kwamba ndiyo chama chenye nguvu zaidi mkoani Kigoma anakotoka kwa sasa na tayari baadhi ya maswahiba wake wa kisiasa kama Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, wamehamia huko wakitokea CHADEMA.

Kamati Kuu CHADEMA

Taarifa za ndani ya kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA zimedai kwamba kambi ya Zitto na Kitila ilimtuhumu mke wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa, Josephine, kuwa ndiye aliyesambaza ulioitwa Waraka wa Siri –ambao pamoja na mambo mengine ulidai kuwa mbunge huyo anapokea fedha kutoka Idara ya Usalama wa Taifa na kuzihifadhi katika akaunti zake za nje ya nchi.

Raia Mwema limeelezwa kwamba Zitto ndiye aliyetoa madai hayo kuhusu Josephine ambaye katika siku za karibuni amekuwa miongoni mwa wachangiaji maarufu wa masuala ya CHADEMA katika mitandao ya kijamii.

Mpaka sasa haijulikani ni nani haswa aliyeusambaza waraka huo uliosababisha Zitto aende kushitaki polisi, lakini inajulikana kuwa Slaa ni miongoni mwa waliovutiwa na maudhui yake kiasi cha ku-like waraka huo mtandaoni.

CHADEMA kimekana kuhusika na waraka huo lakini malalamiko ya Zitto yalikuwa kuhusu hatua ya bosi wake (Slaa) ‘kuupenda’ waraka huo wakati ulikuwa ukimkashifu na kumvunjia heshima mmoja wa viongozi wa juu kabisa wa chama chao.

Gazeti hili linaarifiwa katika kikao hicho, Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu pamoja Mwenyekiti wa chama hicho katika mikoa ya Kanda ya Kusini, Matare Matiko, ndiyo walioongoza mashambulizi dhidi ya Zitto kwenye kikao hicho huku Msafiri Mtemelwa, akiongoza katika watetezi wa Zitto.

Ni Lissu ambaye baada ya Zitto na Kitila kutoa hoja ya kujiuzulu nyadhifa zao ndani ya chama – aliibua hoja ya kutaka wasikubaliwe kujivua wenyewe bali wavuliwe na chama na watakiwe kujieleza kwa nini wasifukuzwe chamani.

Hoja hii ya Lissu ndiyo iliyopitishwa na kamati kuu ya chama hicho.

Chanzo:- Raia Mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates