Social Icons

Sunday, 17 November 2013

WARAKA MAALUMU KWA WABUNGE


MWEZI Mei, mwaka 2013, Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli wakati akijibu hoja za wabunge, Andrew Chenge na Ibrahim Sanya waliochangia hotuba ya  makadirio ya wizara yake, alitumia cheo cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwashawishi wabunge waamini maelezo yake bungeni.

Wabunge hao walitaka wananchi ambao nyumba zao zitabomolewa katika ujenzi wa barabara ya Usagara-Kisesa na wale wanaomiliki kihalali ardhi, wenye hati miliki, vibali vya ujenzi, katika ardhi anayoiita kuwa ni “hifadhi za barabara walipwe fidia.

Akijibu hoja hizo Magufuli aliliambia Bunge wananchi hao hawatalipwa fidia kwa kuwa barabara husika ni ya enzi za Mjerumani na wamejenga katika hifadhi ya barabara.

Alisisitiza akisema; “...sheria hizi mlizitunga wabunge wenyewe  kutokea 1932, mkazifanyia mabadiliko mwaka 1940, 1942, 1949, 1957,1959, 1967 na 2007.  Katika majibu yake, Magufuli alitamba wizara yake imewahi kushtakiwa na kupata ushindi mahakamani na kunukuu shauri namba 39 la 1997 la Baus na wenzake, akamuingiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika hoja hiyo katika namna ya kutaka kuwashawishi wabunge waamini kauli zake ambazo ukweli wake unatia shaka.

Magufuli alimalizia kwa kuwataka wananchi wote ambao wanaamini wanaonewa kwenda Mahakamani kwani huko ndiko ambako sheria hutafsiriwa vizuri.

Siku chache baada ya kutoa kauli hiyo, Mei 31 mwaka 2013, Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi ilitoa hukumu katika shauri namba 80 la 2005, lililofunguliwa na Proches Tarimo na wenzake wakipinga amri iliyotolewa na Wizara ya Ujenzi, Agosti mwaka 2004, kupitia Wakala wa Taifa wa Barabara (TANROADS), iliyowataka wabomoe nyumba zao zilizoko mita 120 kutoka katikati ya barabara kuu ya Morogoro  pande zote mbili, eneo la Mbezi Mwisho (Dar es Salaam) kwa madai eti ziko ndani ya hifadhi ya barabara.

Katika hukumu yake Mahakama Kuu ilitamka kuwa sheria iliyotumika kutoa maagizo ya kubomoa nyumba hizo (The Highway Ordinance Cap 167, Government Notice No 161 of 5/5/1967 is invalid by being inconsistency with sections 15 and 16 of the Village Land Act No 5 of 1999) ni batili kwa kupingana na vifungu vya 15 na 16 vya Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba tano ya 1999.

Mahakama Kuu ilisisitiza ardhi inayodaiwa na walalamikiwa (Wizara ya Ujenzi) kuwa ni hifadhi ya barabara  kwa mujibu wa sheria hiyo waligawiwa walalamikaji kihalali kwa mujibu wa sheria za nchi wakati wa opereshani vijiji ya 1970, hivyo Mahakama Kuu ikatamka kuwa, kwa mujibu wa vifungu vya 15 na 16 vya Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba tano ya 1999, ardhi hiyo ni mali halali ya wananchi waliofungua malalamiko.

Kwa kuwa sheria hiyo ilikuwa na kipengele maalumu kinachotamka upana wa hifadhi ya barabara ya Morogoro utakuwa mita 120 kila upande, ambao ni tofauti na barabara zote hapa nchini. Mahakama Kuu ilitamka kuwa kwa mujibu wa sheria ya mipango miji, hifadhi ya barabara katika Jiji la Dar es Salaam ni mita 30 tu kila upande na huo ndio utakuwa upana wa hifadhi ya barabara ya Morogoro pia.

Mahakama ikamalizia kwa kuelekeza utaratibu wa kisheria wa kufuatwa na Wizara ya Ujenzi kwa mujibu wa kanuni za Sheria ya Ardhi ya Vijiji za 2002, ili kuwalipa fidia wamiliki wa ardhi na maendelezo yaliyomo ndani ya hizo mita 60 zilizotamkwa ili  zipate kuhamishwa kutoka kuwa ardhi ya “kijiji” na  kuwa  “ardhi iliyohifadhiwa kwa maana ya hifadhi ya barabara.”

Mahakama Kuu ilitamka katika kufikia uamuzi wake kwamba imezingatia mambo mbalimbali kubwa ikiwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi, Rais wa nchi ndiye (Trustee) mtunzaji kwa niaba ya wananchi wa ardhi yote ya Tanzania na kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi namaba nne ya 1999, pia ndiye mtunzaji wa  ardhi zote za umma zilizohifadhiwa ikiwa ni pamoja na hifadhi za barabara.

Machi 15, mwaka 1999, Rais wa nchi aliweka sahihi Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba tano ya 1999 ianze kutumika ikiwapa wananchi nguvu za kisheria, juu ya ardhi waliyogawiwa katika Operesheni Vijiji miaka ya 1970 na ikifuta haki zote zinazopatikana juu ya ardhi hiyo kupitia sheria zingine zote. Hii ikiwa na maana kuwa hata sheria, kanuni na amri za kikoloni za barabara zilizotungwa na kutolewa kati ya 1932-1967 pia zilipoteza nguvu juu ya ardhi ya vijiji (alizozitaja Waziri Magufuli bungeni, Mei 2013).

Ni wazi kuwa kuna jambo maalumu ndani ya taifa hili  lililoisukuma serikali na Bunge kutunga Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba tano ya 1999, ikitoa ulinzi mkubwa kwa ardhi ya kijiji na jambo lenyewe ni Operesheni Vijiji iliyotekelezwa na serikali hii hii kati ya 1970-1975. Wanavijiji wengi walijikuta walipo sasa si kwa hiari yao bali kwa kuhamishwa kwa nguvu kutoka walipokuwa wakiishi (maporini) na kubwagwa katika vijiji vya ujamaa, vingi vikiwa vimeanzishwa kandokando ya barabara mbalimbali.

Ni kwa mantiki hiyo, ndio maana taasisi yenye dhamana ya kutunza ardhi yote ya Tanzania (sasa ni Rais Jakaya Kikwete)  mara kwa mara amekuwa akimtaka Magufuli kuzingatia utu, ubinadamu na historia ya eneo husika kabla ya kuchukua uamuzi wa kuziwekea alama X na kubomoa nyumba za wananchi wanyonge na kutoa kipaumbele katika kuipunguzia serikali mzigo wa kulipa fidia tu.

Kwa bahati mbaya sana kila mara Magufuli anapopatiwa maelekezo kama hayo na wakubwa zake kikazi hutoa matamshi yenye mwelekeo wa kupingana nao, pengine kwa sababu ya kujiamini ‘kisiasa’ kupita kiasi.

Rai za mara kwa mara za Rais ni uthibitisho anatambua kuwa si kweli kila aliyejenga katika eneo la hifadhi ya barabara ni mvamizi wa hifadhi husika kama anavyodai mara kwa mara Magufuli.

Ibara ya 107 A ya Katiba ya Tanzania inatamka mhimili wa Mahakama ndio wenye kauli ya mwisho katika utoaji wa haki ndani ya Tanzania.  Na mara baada ya hukumu ya Mahakama kutolewa hutengeneza kitu kinachojulikana kama Judicial Precedent  ambayo ni moja ya vyanzo vya sheria vinavyokubalika hapa nchini.

Kwa mujibu wa kamusi za kisheria “judicial precedent” ni hukumu au uamuzi wa mahakama unaoweza kunukuliwa kama mamlaka ya kufanya uamuzi katika mashauri yanayofanana, kushabihiana au kuwa na mweleko mmoja.

Mazingira ya mgogoro uliokuwepo baina Wizara ya Ujenzi na wananchi katika barabara ya Morogoro juu ya hifadhi za barabara eneo la Mbezi Mwisho, jijini Dar es Salaam, kuamuliwa na mahakama kupitia shauri namba 80 la 2005, yanafanana kabisa na mazingira ya migogoro ya hifadhi za barabara iliyopo nchi nzima kutokana na ukweli kwamba, kati ya 1970-1975, Serikali ya Tanzania ilitekeleza mpango kabambe nchi nzima wa kupanga upya makazi ya wananchi wake hususan waliokuwa wakiishi sehemu za mashambani, kila kaya kivyake maporini. Hivyo karibu sehemu kubwa ya ardhi ya Tanzania vilianzishwa vijiji vya ujamaa.

Hivyo kwa mujibu wa “Judicial Precedent” hukumu na uamuzi wa shauri namba 80 la 2005 unaweza kutumika na mahakama zingine hapa nchini kama mamlaka (authority) katika kuamua mashauri mengine lukuki yanayoweza kufikishwa mbele ya mahakama hizo, kutokana na ubabe wa Waziri Magufuli kung’ang’ania kutumia sheria, kanuni na amri za kikoloni zilizotungwa kati ya 1932-67 katika kutekeleza  majukumu ya Wizara ya Ujenzi badala ya sheria zilizotungwa na Bunge, zinazotambua haki ya wananchi kulipwa fidia ya ardhi au majengo yao vinapotwaliwa kwa ajili ya maslahi ya taifa kama vile ujenzi wa barabara .

Moja ya vitendo ambavyo wananchi nchi nzima wanaweza kuvilalamikia mahakamani na kupata ushindi kirahisi ni kitendo cha Waziri Magufuli kuiagiza TANROADS kuingia katika ardhi na makazi ya wananchi kuweka alama mbalimbali zinazowazuia kutumia ardhi na majengo yao kujikimu kimaisha, kabla ya Wizara ya Ardhi kukamilisha taratibu za kuhifadhi ardhi hiyo kama “hifadhi ya barabara” kwa kuwalipa fidia.

Kitendo chochote cha kuwazuia wananchi kuendeleza au kutumia ardhi na majengo yao wanayomiliki kihalali kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi namba nne na tano za 1999 kabla ya kulipwa fidia ni uvunjaji wa haki zao za kikatiba na kisheria.

Ikumbukwe, tangu 1999 hapakuwepo sheria yoyote ya barabara iliyokuwa na nguvu juu ya ardhi za vijiji hadi mwaka 2007 ilipotungwa na kupitishwa Sheria ya Barabara namba 13 ya 2007, inayotaka kwanza Wizara ya Ardhi ifanye machakato wa kuhifadhi ardhi husika na fidia kulipwa, ndipo TANROADS waingie katika ardhi ya mwananchi yeyote.

Kama ikijitokeza kuwa TANROADS imeingia katika ardhi au jengo la mwananchi yeyote bila ya kuzingatia utaratibu huu wa kisheria, kitendo hicho ni uingiaji haramu (Trespass) kisheria na yote yaliyofanyika ni batili na wananchi wanatakiwa kuchukua hatua za kuifikisha TANROADS mbele ya vyombo vya sheria, kudai fidia za upotevu wa faida kwa kuzuiwa kutumia ardhi na majengo yao kiuchumi.

Tanzania ni yetu sote na barabara zinazojengwa ni kwa faida yetu sote kwa nini tugombee fito katika ujenzi huu kiasi cha kuburuzana mahakamani? Kama nchi, je hatuna taratibu nzuri za kiutawala zinazoweza kutumika kumaliza migogoro hii?

Naamini taratibu hizo zipo, lakini tatizo ni baadhi ya viongozi wanaojihisi maarufu sana kwa wananchi, hawawezi kukaa meza moja na viongozi wenzao kutafuta njia bora zaidi ya kisheria ya serikali kupata ardhi ya kufanya maendeleo ya barabara hapa nchini.

Ni kutokana na udhaifu huo, Waziri Magufuli kati ya mwaka 2000—2002 aliiagiza TANROADS kuingia mita kati ya 31 na 120 kutoka katikakati ya barabara ya Morogoro pande zote mbili eneo lote kati ya Ubungo hadi Kiluvya, pasipo kupata taarifa yoyote kutoka kwa kiongozi au ngazi yoyote ya uongozi na kuweka mabango, mawe na miti vinavyoonyesha mwisho wa hifadhi ya barabara.

Ghafla wapangaji wote waliokuwa katika nyumba hizo  wakahama kwa kuogopa kuharibiwa vitu vyao katika bombaboma iliyotangazwa, wakashindwa tena kupata wapangaji wapya labda kwa bei ya chini mno anayotaka mpangaji kwa kuwa tayari nyumba zina alama za X, hawakuweza tena kujenga chochote kwani kila ukijaribu kujenga wanawekewa alama ya X na wanashuhudia majirani zao wakibomolewa.

Kutokana na kutoweza kutumia ardhi na majengo yao kiuchumi, wengi walishindwa kumudu familia zao, watoto walishindwa kuendelea na masomo.

Hadi leo eneo lote kati ya Ubungo hadi Kibaha  limebaki nyuma kimaendeleo wananchi hawakuweza kujenga majengo makubwa pembezoni mwa barabara kuu, hivyo hakuna huduma za kibenki, ATM au maduka makubwa,  ambavyo vingechangia kukuza ajira na vipato vya wananchi.

Miaka 13 tangu uamuzi huo wa kibabe kutekelezwa, sasa Mahakama, baada ya kusikiliza pande zote imeamua kuwa yote aliyotenda Magufuli kuhusu hifadhi za barabara, kupitia Wizara ya Ujenzi na TANROADS, yalifanyika isivyo halali na kinyume cha sheria.

Je, nani wa kuwalipa fidia kwa matatizo yaliyowasibu wahusika? Je, kama kanuni za utawala bora na ushirikishwaji zingezingatiwa kwa viongozi wa ngazi zote kushirikishwa, wananchi hawa wasingeweza kupunguziwa madhara ya kijamii, kisaikolojia na kiuchumi? Nani atarejesha roho za marehemu waliopoteza maisha kwa hofu ya kupoteza ardhi, nyumba na vipato?

Ni ubabe tu uliotumiwa na TANROADS kuingia zaidi ya mita 90 ndani ya ardhi na makazi ya wananchi bila ya mashauriano au kuwashirikisha viongozi wa ngazi za mkoa, wilaya, manispaa, tarafa, kata na hata mitaa ambao wangetoa maoni ya namna bora ya serikali kupata ardhi kwa ajili ya hifadhi ya barabara bila ya kuathiri ustawi wa wananchi.

Chanzo:- Raiamwema

No comments:

 
 
Blogger Templates