Social Icons

Saturday, 21 December 2013

ANC YA MANDEL NI ZAIDI YA CCM YA NYERERE

CHAMA cha African National Congress (ANC) cha Nelson Mandela na Chama cha Mapinduzi (CCM) cha Mwalimu Julius Nyerere ni vyama vyenye kufanana kwa mengi.  Moja ni hilo kwamba wakati mmoja vyama hivyo vikiongozwa na watu wa kupigiwa mfano kiasi cha  vyama hivyo kunasibishwa na viongozi hao.

Hawa ni viongozi ambao wanatukuzwa na kufikishwa mbinguni na baadhi ya wafuasi na washabiki wao wa ndani na nje ya nchi zao. Kuna wenye kusema kwamba wawili hao, yaani Mandela kwa ANC na Nyerere kwa CCM, ni watakatifu.

Ingawa Mandela alikuwa mara kwa mara akikanusha kwamba yeye si mtakatifu, nchini Tanzania kuna juhudi zinazofanywa za kulitaka Kanisa la Katoliki huko Vatican limtangaze rasmi Mwalimu Nyerere kwamba ni Mtakatifu.

Jingine linalovifanya vyama hivyo vifanane ni jinsi vilivyoweza kuzidhibiti nchi zao, ingawa udhibiti wao siku hizi si madhubuti kama ulivyokuwa awali viliposhika hatamu za uongozi wa serikali zao katika nchi zenye katiba za kidemokrasia. Ninaamini kwamba kwa sababu zina katiba za aina hiyo nchi zao zinaweza kujikokota zisisambaratike.

Pamoja nakuwa na katiba hizo nchi hizo pia zina jumuiya na asasi za kiraia zenye nguvu, zina vyama vya upinzani vilivyo madhubuti, vyombo vya habari vilivyo macho. Afrika ya Kusini, kwa upande wake, ina zaidi ya hayo.Ina vyama vya wafanyakazi vyenye nguvu,mfumo wa kisheria ulio huru na imara pamoja na makampuni ya kibiashara yalio makubwa na yenye nguvu.

Zipo bila ya shaka tafauti baina ya vyama hivyo.Ya kwanza ni kwamba vyama hivyo viliasisiwa kwa madhumuni ya kupigana na maadui tafauti waliokuwa na mifumo tafauti ya kiutawala ingawa yote ilikuwa ikiwadhalilisha Waafrika. Na zaidi viliendesha harakati zao za ukombozi katika mazingira yaliyokuwa tofauti.

Tofauti nyingine ni kwamba kinyume na CCM, chama cha ANC ni chama kilicho kama mwamvuli, chini yake mna vyama vingine vizito vyenye kukiunga mkono.  Miongoni mwavyo ni Chama cha Kikomunisti cha Afrika ya Kusini (SACP) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi vya Afrika ya Kusini (Cosatu). Baadhi ya mawaziri wa serikali inayoongozwa na ANC ni viongozi au wanachama wakuu wa vyama hivyo.  Na hata Mandela mwenyewe pamoja na kuwa kiongozi wa ANC alikuwa pia mwanachama wa siri na mjumbe wa kamati kuu ya Chama cha Kikomunisti. 

Chama cha CCM na serikali yake, kwa upande wao, havina umbile kama hilo.  Na wala havikuwahi kuwa na umbile kama hilo tokea asili yake huko kilikotoka.

Tukiizungumzia CCM katika enzi hizo tunakuwa hasa tunaizungumzia TANU. Na tofauti kubwa ni ile ya kwamba ijapokuwa chama cha ANC kimekipita sana kile cha CCM kwa umri — ANC kilizaliwa Januari 8, 1912 na ndicho chama kikongwe kabisa barani Afrika — hata hivyo hakina uzoefu mkubwa wa kuendesha serikali kama kilionacho chama cha CCM.

Vyama vyote hivyo viwili vimefanikiwa katika lengo lao kubwa la kuleta ukombozi kwa kuushinda ama ukoloni wa Kiingereza nchini Tanganyika au utawala wa kibaguzi wa makaburu huko Afrika ya Kusini.

Juu ya mafanikio hayo kubwa pamoja na mengine ya kimaendeleo kwa jumla vyama hivyo vimeshindwa kuwatoa kwenye umasikini wengi wa wananchi wa nchi zao. Nchini Afrika ya Kusini hali ni mbaya zaidi. Utawala wa kibaguzi na ubaguzi wa rangi ulikomeshwa nchini humo baada ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia mnamo mwaka 1994.

Hayo, bila ya shaka, yalikuwa mafanikio makubwa lakini hayakuweza kuwatoa kutoka kwenye umasikini mamilioni ya Waafrika weusi nchini humo.  Kwa hakika, hali zao zilizidi kuwa duni kwa kuzuka kwa ubaguzi wa kiuchumi.

Ubaguzi huu haukuwa na rangi kwa sababu kuliibuka kundi la mabepari wa Kiafrika, miongoni mwao wakiwa viongozi wa ngazi za juu wa ANC, wa Cosatu na wa Chama cha Kikomunisti. Hawa walizitumia nyadhifa zao ndani za  vyama vyao au serikalini kujitajirisha. Niutaje mfano mmoja tu wa Bibi Joyce Moloi-Moropa ambaye ni mbunge wa ANC na mshika hazina wa Chama cha Kikomunisti.

Bibi huyu Mheshimiwa Mkomunisti ni mkurugenzi pia wa kampuni ya uwekezaji ya Masincazelane Investments iliyoundwa na chama cha Kikomunisti. Isitoshe ana hisa za asilimia 19 katika Chuo cha kibinafsi Letsatsi Solutions na ni mkurugenzi wa kampuni moja ya matufali iitwayo Zebediela Bricks.

Bibi Moloi-Moropani ni mmoja tu wa viongozi wakuu wa ANC wenye kujishughulisha na mambo ya biashara kubwa kubwa. Inasemekana kwamba kampuni ya Zebediela Bricks peke yake kila mwaka inaingiza faida ya mamilioni ya dola za Marekani.

Hivi majuzi katibu mkuu wa chama cha Kikomunisti cha SACP, Blade Nzimande, ambaye pia ni waziri wa elimu ya juu alitoa mwito kutaka viongozi wa chama cha wafanyakazi cha Numsa wakaguliwe kwa namna wanavyoishi. Alisistiza kwamba kampuni ya uwekezaji ya chama hicho pia ikaguliwe.  Na kuna wenye kukumbusha kama miaka sita iliyopita kulitolewa miito ya kutaka Nzimande mwenyewe akaguliwe.

Siku hizi ni kawaida kuwaona waheshimiwa hawa walioichovya mikono yao katika biashara — au watoto wao — wakikodi ndege za aina ya jet za watu binafsi kuwapeleka katika miji ya Ulaya kama ya Paris au London mwishoni mwa wiki kwa matembezi. Ninaweza kuwataja wawili watatu ambao wakifika Ulaya hutumia si chini ya dola za Marekani 75,000 kununua nguo na uturi.

Maisha wanayoishi hayasemeki; hafla wanazozifanya majumbani mwao ni za kashfa tupu; mengine hata ukielezewa hutoyaamini.  Kwa ufupi, watu hawa wanaishi maisha ambayo ni kama mbingu na ardhi ukiyalinganisha na ya Waafrika wa kawaida. Na ni juzi tu watu hawa wakijigamba kwamba wao ni wakombozi wa Afrika ya Kusini.

Cyril Ramaphosa, ambaye Desemba mwaka jana alichaguliwa kuwa naibu wa rais wa ANC, na aliyekuwa kwa muda mrefu kiongozi wa chama kikubwa cha wachimba migodi ya NUM, hivi sasa ni mmoja kati ya matajiri wakubwa wa Afrika ya Kusini.  Inakisiwa kwamba utajiri wake una thamani ya dola za Marekani milioni 675.  Na hata haoni haya wala aibu kwamba anaendelea kujidanganya ya kuwa eti yeye ni mjamaa.

Tumeusikia utajiri wa Julius Malema, aliyekuwa kiongozi wa tawi la vijana la ANC kabla hajafukuzwa kwa utovu wa adabu, na nyumba aliyokuwa akiijenga.  Na tumesikia vipi Rais Jacob Zuma alivyochota mamilioni ya fedha za umma zenye thamani ya dola za Marekani milioni 21 kutengeneza nyumba yake ya binafsi ya Nkandla. Watu watasema mpaka watachoka; kwani kwa kawaida mafisadi huwa hawajali.

Waheshimiwa hawa nao wana mtindo wa kulindana. Inabidi walindane kwa sababu wana fursa kubwa za kuchota kwenye makampuni ya uwekezaji ya baadhi ya vyama vya wafanyakazi vinavyoshirikiana na ANC.

Wale wanaojitolea kuupinga mtindo huo wa ufisadi na wa kulindana hubandikwa majina ya ajabuajabu.  Huambiwa, kwa mfano, kwamba wao ni wapinga mapinduzi au kuwa wanatumiwa na ubeberu na shutuma kama hizo zisizo msingi na zenye lengo la kuwapaka tope tu wapinzani wa ufisadi.

Kwa muda sasa wanachama wa kawaida wa ANC na wa vyama vya wafanyakazi wamekuwa wakisisitiza kwamba viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wanasiasa lazima wawajibike.

Tangu jana Jumanne chama cha Numsa, ambacho kinamuunga mkono katibu mkuu wa Cosatu aliyesimamishwa kazi, Zwelinzima Vavi,  kimekuwa na mkutano mkuu maalumu.  Jambo kubwa linalozungumzwa ni iwapo chama hicho kiendelee kukiunga mkono chama cha ANC katika uchaguzi mkuu ujao. Kikikata uamuzi huo basi utakuwa ni pigo kubwa kwa ANC.


Chanzo :- Raia Mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates