NELSON Mandela aliyeingia jela mwaka 1964, sie yule aliyetoka jela mwaka 1990. Kutokana na ‘balaa’ la kuhukumiwa kifungo cha maisha, Mandela aligeuza balaa hilo kuwa ‘fursa’, akatulia, akajielimisha, akatafakari, akabadilika na kutoka akiwa tofauti na bora kiutu kuliko alivyoingia.
Matokeo yake, Mandela leo hii ana sura nyingi, akiwakilisha falsafa na mitazamo tofauti ya vipindi tofauti vya maisha yake. Ni kwa sababu hii, Barack Obama na Raul Castro, wanaowakilisha mitazamo kinzani ya kisiasa, kiuchumi na huenda hata kijamii - walikutana katika mazishi ya Mandela, huku kila mmoja akimmwagia sifa (Mandela).
Kwa mtazamo wa nchi za Magharibi, Obama na wenzake, ushujaa wa Mandela unatokana na maisha yake ya kuanzia 1990, baada ya kuachiwa kutoka kifungoni na kuiongoza Afrika Kusini katika mabadiliko ya kisiasa yaliyohitimisha utawala wa ubaguzi wa rangi.
Kuiongoza nchi haikuwa kazi kubwa kuliko kusimamia mabadiliko hayo yaende kwa amani, mapatano, na kuridhisha pande hasimu na mwisho kujenga taifa moja. Huu ni mtazamo uliotawala katika nchi za Magharibi.
Mandela wa miaka ya 1960, ambaye yeye na wenzake waliunda jeshi la Umkhonto we Sizwe la ANC lililohujumu serikali, alionekana gaidi, muuaji asiyestahili heshima yoyote na ndio maana mpaka mwaka 2008 aliorodheshwa miongoni mwa magaidi wasiotakiwa Marekani.
Ingawa Obama katika hotuba yake ya siku ya kumbukumbu ya Mandela katika uwanja wa FNB, alimsifia na kumfananisha na Mahatma Gandhi na Martin Luther King, ukweli ni kwamba Mandela hawezi kuwa kama Gandhi na King, ambao waliongoza harakati za amani. Mandela aliongoza mapambano ya silaha. Ulinganisho huo, hata hivyo unaonyesha jinsi gani nchi za Magharibi zinavyojaribu kuiandika upya historia.
Lakini ni huyu Mandela wa miaka ya 1960 ndie ambaye Castro alienda kumzika, mpiganaji aliyepambana na mfumo kandamizi wa ubaguzi wa rangi ulioungwa mkono na mabeberu. Ni Mandela huyu ambaye Tanzania, kupitia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete katika mazishi ya Madiba kule Qunu, inajivunia ingawa pamoja juhudi za kupuliza tarumbeta letu ili mchango wetu usikike, ni kidogo sana kilichoripotiwa katika vyombo vya habari vikubwa duniani, ambavyo vinatukuza kumbukumbu ya Mandela wa miaka ya 1990 kwenda mbele.
Baadhi ya Watanzania hata nimeona katika mitandao ya kijamii wakilalamika kuwa baadhi ya vyombo vya kimataifa vilihamia katika mijadala na kuacha kuirusha hotuba ya Kikwete, ingawa hili sijalithibitisha.
Ni kipimo cha mchango wa Mandela huyu wa miaka ya 1960 ndicho ambacho wengi wanatumia kumlinganisha na mashujaa wengine wa Afrika na kwingine duniani, akiwemo Nyerere na Mao Zedong wa China, na kufikia hitimisho kuwa amepaishwa mno.
Hapa China, wanaojiita wafuasi wa Mao walikosoa vyombo vya habari kwa kumsifu mno Mandela, ambaye hana mchango katika fikra za mapinduzi, ukilinganisha na Mao, aliyekomboa Wachina, kuwaunganisha na kuwasaidia kusimama wenyewe. Wahafidhina hawa wa Kimao, wanasema Mandela hakumaliza kazi yake vizuri hasa katika kuwanyanyua weusi kiuchumi.
Baadhi ya ndugu zangu Watanzania nao wanaona Nyerere ni bora kwa kuwa alihangaika kulikomboa Bara la Afrika wakati Mandela akiwa kifungoni. Watanzania wanahoji kama kufungwa, Mandela hakuwa mfungwa pekee na kwamba Nyerere akiwakilisha Tanzania alikuwa mstari wa mbele katika harakati za ukombozi na kuifanya Tanzania kuwa makao makuu ya harakati hizo.
Wapo watu kama Emmanuel D. Tayari, ambao wanasema Nyerere alimtengeneza Mandela na kwamba mafanikio ya Mandela yasingekuwapo bila ya msaada wa Nyerere. Katika makala yake ya 2009, Tayari anasema Nyerere kwa kushirikiana na Askofu Mkuu Trevor Huddleston mwaka 1959, walizindua harakati huko Uingereza ambazo ndio msingi wa mafanikio karibu yote ya mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Mjadala huu haujaishia Tanzania na China pekee, makundi ya watu katika nchi nyingine kadhaa yamehoji kutukuzwa kwa Mandela. Wapo Waafrika waliohoji kwa vigezo gani Mandela anaitwa shujaa wa Afrika.
Vyombo vya habari vya Magharibi vimelaumiwa kwa kumpaisha Mandela na kudidimiza mashujaa wengine. Fadhy Mtanga, kupitia Facebook, alikosoa gazeti la Daily Mail la Uingereza lililoweka picha maarufu 40 za Mandela bila ya kuweka hata moja akiwa na Nyerere, ingawa zipo alizopiga na watu wasio na ‘uzito’ kama Spice Girls.
Jambo ambalo Mtanga hakulizingatia ni kuwa Mandela ana sura tofauti zinazokubalika sehemu tofauti na watu tofauti kwa sababu ya tofauti ya falsafa za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Mandela wa gazeti hilo ni wa mwaka 1990 na kuendelea. Ni Mandela huyu, mwenye kusamehe, aliyesahau yaliyopita na kuganga yajayo, ndie ambaye kumbukumbu yake ina nguvu kwa sababu ya nguvu ya vyombo vya habari vya Magharibi na ni miaka 27 ya kifungo ndio iliyombadilisha Mandela kutoka mpiganaji hadi mpatanishi, kama alivyojieleza katika mahojiano yake na Oprah Winfrey.
Miaka ya kifungoni
Mandela alimwambia Oprah Winfrey kama asingefungwa asingefanikiwa kutimiza kazi ngumu zaidi iliyomkabili maishani, nayo ni kujibadili yeye mwenyewe. “Nikiwa jela, nilikuwa na muda wote wa kufikiri. Nilikuwa na taswira kamili ya maisha yangu ya zamani na sasa, na niligundua maisha yangu ya zamani yalikuwa na walakini mwingi katika uhusiano wangu na watu na kitabia”.
Mandela alijifunza nidhamu mpya ya maisha, akijitahidi kujisomea na kuhimiza wenzake wajisomee akiamini kwa kusoma walikuwa wakijipatia silaha yenye nguvu zaidi ya kutafuta uhuru, elimu. “Nilitoka jela nikiwa nimepunguza upumbavu kuliko nilivyoingia”.
Akiwa jela kupitia tafakuri na vitabu, Mandela anasema aliweza kuvunja kiburi cha enzi za ujana na kuwa mnyenyekevu. Kadri unavyoelimika zaidi, ndivyo kiburi na ugomvi vinavyopungua”, Mandela alisema na kuongeza kuwa aliazimia akiwa jela kuwa akitoka atatafuta mapatano na wengi aliowakosea katika maisha yake binafsi.
Dhamira hii binafsi ya kutafuta mapatano, haikuishia katika kutafuta mapatano ya nafsi yake, bali ilimsukuma kutafuta muafaka wa taifa zima, kati ya wazungu na weusi, na miongoni mwa makundi yaliyokuwa yakiuana ya weusi.
Ni Mandela mpya aliyetoka jela akiwa amejipanga kupatanisha ndio ambaye dunia leo hii inasheherekea maisha yake.
Mandela aliyebadilika anayesherekewa maisha yake na nchi za Magharibi ni yule ambaye kiongozi wa dini ya kiyahudi Dk. Warren Goldstein alimfananisha na mtume Yusufu ambaye aliyesamehe na kuiunganisha familia yake baada ya kukamata madaraka makubwa licha ya kutupwa kisimani na ndugu zake na kupitia mambo mengi machungu, ikiwamo kufungwa.
Ni Mandela ambaye, hata baada ya miaka 27 ya kifungo, baada ya kukamata madaraka hakufanya visasi, alitafuta maridhiano na mapatano, alisimika misingi ya demokrasia ya vyama vingi na utawala bora, pamoja na uhuru wa vyombo vya habari. Mandela huyu ni yule ambaye alitetea haki za wanawake za kutoa mimba na haki za mashoga kutobaguliwa.
Misimamo hii ya Mandela ilimkosanisha na kukusolewa na viongozi wa dini likiwemo Kanisa Katoliki na misimamo hii itachukua muda mrefu kukubalika miongoni mwa viongozi wahafidhina, kama Barack Obama wa Marekani na hata miongoni mwa waafrika wengi.
Muhimu zaidi, Mandela hakutaka kufanya majaribio ya kuleta uchumi wa kijamaa na kupambana na mfumo wa kibepari ulioota mizizi uliounganisha uchumi wa Afrika ya Kusini na soko la dunia, pamoja na kuwa mwongozo wa ANC ulioitwa Freedom Charter ulioandikwa miaka ya 1950 ulielekeza hivyo.
Mwongozo huo, uliokuwa dira ya mapambano, unaelekeza kutaifishwa kwa njia kuu za uchumi kama benki, migodi na kugawa ardhi upya ili kuwasaidia weusi waliokandamizwa kwa muda mrefu. Ni dira hii ambayo iliwapa wazungu homa wakihofia Mandela angeenda kuigeuza Afrika Kusini kuwa Cuba nyingine.
Hilo halikufanyika na Mandela amelaumiwa kwa kuwauza weusi wenzake kwa kutenganisha majadiliano ya maridhiano ya kisiasa mbali na uchumi. Na kwa sababu hii pamoja na uhuru wa kisiasa, watu weusi bado wana maisha duni. Mabadiliko pekee ya kiuchumi ni kuibuka kwa kundi la mamilionea wachache weusi waliojiunga na mamilionea weupe.
Mandela alikuwa na bahati sana kwani aliongoza nchi yake wakati tayari wenzake washaujaribu ujamaa na kuonekana wazi kuwa ni mradi ulioshindwa na bila shaka, baada ya kusoma hali ya dunia Mandela alijua kuwa hana uchaguzi zaidi ya kukubali kuachana na fikra za ujamaa.
Mandela alijua mpango wowote wa kubadili mfumo uliopo kwa kutapelekea nchi hiyo kutengwa na kuvurugika kwa uchumi, na kupelekea Afrika ya Kusini kuwa Zimbabwe nyingine. Ikumbukwe kuwa wakati ikipata uhuru 1980, Zimbabwe ilikuwa ni moja ya mataifa yenye hali nzuri kiuchumi, ingawa kulikuwa na tatizo la mgawanyo wa rasilimali usio wa haki wa rasilimali kama ilivyo Afrika Kusini. Kwenye ardhi kwa mfano inaelezwa kuwa wazungu ambao ni asilimia moja walimiliki asilimia 70 ya ardhi ya kilimo.
Utaifishaji na jaribio la kurekebisha mgawanyo usio sawa wa ardhi bila utaratibu mzuri, ambapo wmaveteran wa vita ya ukombozi walivamia mashamba ya wazungu na kuyakalia kwa nguvu, umepelekea uchumi wa Zimbabwe kuanguka na kuongezeka kwa umaskini, ukosefu wa ajira na matatizo mengine lukuki.
Mandela hakutaka kupita njia hiyo na alifikia maamuzi haya kwa nia safi, sio kuwasaliti watu wake au kuwafuirahisha wazungu, kwa maslahi ya nchi. Lakini uamuzi wake huu umempatia heshima kubwa duniani leo hii.
Mandela anaweza kuwa na hadhi sawa au kuzidiwa na Mugabe, Nyerere, na wengineo kwa kigezo cha mchango wao katika mapambano dhidi ya mifumo kandamizi – lakini tofauti inajitokeza wazi katika jinsi Mandela na hao wanaolinganishwa walivyoongoza nchi zao baada ya kuingia madarakani.
Tofauti hizo, pamoja na unyenyekevu, uadilifu, subira, hekima, upendo, huruma - ndio kunaomfanya awe bora kuliko Nyerere na yoyote mwingine.
Swali la msingi, hata hivyo ni je hali itabaki ilivyo baada ya kufariki Mandela? Tayari sauti zinasikika zikidai utekelezwaji wa ahadi hizo za wakati wa mapambano hasa zinazohusu kuinua uchumi wa weusi. Hawakukosea wachambuzi waliosema mafanikio ya Mandela ya kisiasa na kuibuka kuwa shujaa duniani, kumeficha kushindwa kwake katika kutimiza malengo ya mapambano yake.
Chanzo:- Raia Mwema

No comments:
Post a Comment