KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana anatarajiwa kukutana na wabunge wa CCM mwishoni mwa wiki hii mjini Dodoma. Mkutano huo kati ya Kinana na wabunge wa chama chake, utatanguliwa na kikao cha Kamati Kuu (CC), itakayokutana Ijumaa chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka ndani CCM na kuthibitishwa na watendaji wa ngazi ya juu, kilisema mkutano wa Kinana na wabunge hao umelenga kuwapa meno ya kuibana Serikali na mawaziri mizigo ambao wamekuwa wakilalamikiwa na wananchi.
“Kamati Kuu ya CCM itakutana Ijumaa wiki hii, chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete, Jumamosi Kinana atakutana na wabunge wote wa CCM ambao wengi wapo hapa mjini Dodoma wakiendelea na vikao vya Bunge.
“Ndugu yangu unajua Kinana amebadili sura ya CCM, kuna hofu huenda katika kikao cha CC mambo mazito yakaibuka ikiwemo kuwajibishwa kwa baadhi ya mawaziri ambao wameonekana wakiiangusha Serikali kutokana na utendaji wao kuwa duni,” kilisema chanzo hicho.
Kutokana na hali hiyo, RAI ilimtafuta Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ambaye alithibitisha kuwepo kwa kikao hicho.
“Ni kweli CC itakutana wiki hii mjini Dodoma na itajadili masuala mbalimbali, ila kinachojadiliwa ni siri ya kikao kwa sasa, kwani hakiwezi kuwa wazi kwa kipindi hiki.
“Suala tunajadili nini subiri baada ya kikao, mambo yote tutayaweka wazi, CCM hatuna utamaduni wa kuwaficha mambo,” alisema Nape.
Hata hivyo alipoulizwa kuhusu kuhojiwa kwa mawaziri ‘mizigo’ na CC alisema hayuko tayari kuzunngumzia jambo hilo ila sekretarieti ndiyo yenye wajibu wa kuandaa ajenda ambazo zitawasilishwa.
Hivi karibuni, Kinana alitangaza kuwajibishwa kwa mawaziri watatu ambao huenda wakawajibishwa na CC kutokana na kushindwa kutatua kero za wananchi.
Mawaziri wanaolalamikiwa ni pamoja na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza na Naibu wake, Adamu Malima, Waziri wa Fedha, Dk. Wiliam Mgimwa.
Wengine ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe.
Hata hivyo, Waziri Chiza na naibu wake, Adamu Malima wanadaiwa tangu walipoteuliwa kushika madaraka hayo, wameshindwa kutekeleza wajibu wao wa kuongoza wizara hiyo ambapo inaelezwa kuwa hawajawahi kutembelea Mkoa wa Ruvuma ambao ni ghala la chakula.
Chanzo:- Mtanzania

No comments:
Post a Comment